Usitanzwe tena na swali lolote la Kiswahili, sasa tuma tu arafa

Na FRED OBONDO

Imepakiwa - Friday, January 26  2018 at  20:24

Kwa Muhtasari

KWA miaka mingi sasa, wapenzi wa lugha ya Kiswahili nchini Kenya wamekuwa wakitafuta jukwaa la kudumu la mtagusano na mashauriano kati yao kuhusu masuala ya lugha hii.

 

Ingawa zimekuwapo jitihada za kutambulika za wataalamu binafsi za kukipigia debe Kiswahili kupitia kwa vyombo vya habari na njia nyinginezo, ni dhahiri shahiri kwamba wasomi na wapenzi wa Kiswahili hawajakoma kutoa mwito wa kuundwa kwa jopo maalum la wataalamu wa lugha hii nchini Kenya.

Sasa tabasamu za furaha hazitaisha nyusoni pa wapenzi wa Kiswahili kutokana na kutimia kwa ndoto yao mwaka huu. Jitihada za ukuzaji na usanifishaji wa lugha ya Kiswahili zimepigwa jeki pakubwa kutokana na uzinduzi wa huduma ya nambari mpya ya ujumbe mfupi wa rununu 20270.

Nambari hii ya arafa inalenga kuwapa wanafunzi, walimu, wazazi, watafiti na wapenzi wengineo wa Kiswahili jukwaa la kutagusana na kushauriana na jopo la wataalamu kutoka nchini Kenya na Tanzania wenye tajriba pana na uzoefu wa utamaduni na ufundishaji wa Kiswahili.

'Kiswa' kwa nambari 20270 

Wahusika wanahitajika tu kutuma ujumbe mfupi wa rununu wakianza na kwa neno; Kiswa kwa nambari 20270 kisha waulize maswali na kutoa mapendekezo ama maoni yoyote kuhusu Kiswahili kwa nambari hiyo ya arafa kisha watapokea jawabu baada ya muda mfupi. Huduma hii inapatikana kila siku kwa muda wa saa 24.

Fauka ya hayo, huduma za nambari hii zitawawezesha wahusika kupata maelekezo na ushauri kuhusu masuala mbalimbali ya lugha ya Kiswahili yakiwamo masuala tata, kupendekezewa marejeleo ya utafiti wa ziada na kujulishwa kuhusu makongamano ya Kiswahili yatakayoandaliwa nchini Kenya, Tanzania ama kokote ulimwenguni.

Uzinduzi huu wenye kauli-mbiu Lugha yetu, hazina yetu umeambatana na ufunguzi wa wavuti maalum kwa jina Kiswahili Solution Centre. Wavuti huu utakuwa hazina kuu ya mkusanyiko wa kazi mbalimbali za utafiti wa Kiswahili.

Wapenzi wa Kiswahili na wasomi wa asasi za viwango mbalimbali vya elimu ya Kiswahili nchini Kenya na Tanzania wameisifu hatua hii wakisema kwamba ni mojawapo ya hatua kuu zaidi zilizowahi kupigwa katika harakati za ukuzaji na uenezaji wa lugha ya Kiswahili.