Wachawi saidieni

Imepakiwa Monday July 25 2016 | Na MAKILLA

Kwa Muhtasari:

Sifa zenu naamini, zimeenea mjini,

Kadhalika vijijini, pia kote duniani,

SIFA zenu naamini, zimeenea mjini,

Kadhalika vijijini, pia kote duniani,

Kwa kweli twawaamini, ila bado kuwathamini,

Wachawi saidieni, tupate maendeleo.

 

Mtunzi nimebaini, mna mengi kwa yakini,

Mwaweza fanya nchini, uchumi usiwe duni,

mkaongeza thamani, dunia kututhamini,

Wachawi saidieni, tupate maendeleo.

 

Tunataka televisheni, zenye bei afueni,

Mwazitengeza nyumbani, hamuuzi madukani,

Tunachotaka maishani, hizo ziwe mitaani,

Wachawi saidieni, tupate maendeleo.

 

Mwazungumza hewani, ila simu hatuoni,

Nalo hili twaamni, ni biashara auni,

Zije simu za mkononi, tuwe nasi washindani,

Wachawi saidieni, tupate maendeleo.

 

Finland na Marekani, kwa Nokia ni makini,

Matorola nayo ndani, ya kwetu iwe akilini,

Tuuite jina gani, pengine la majinuni,

Wachawi saidieni, tupate maendeleo.

 

Mashine kazi undeni, tupeleke viwandani,

Msukule watumieni, hata nishati wabuni,

 Ili mradi mwakani, nchi iwe namba wani,

Wachawi  saidieni, tupate maendeleo.

 

Na nungo kageuzeni, tupate ndege angani,

Eitisii iufufueni, iende hadi Japan,

Na mizigo tubebeni, tuiuze kwa jirani,

Wachawi saidieni, tupate maendeleo.

 

Elimu yetu ya ndani, mwaisaka ugenini,

Kadhalika mashambani, pamwe yako nyikani,

Vilevile vichakani, yote mnayathamini,

Wachawi tusaidieni, tupate maendeleo.

 

Majongoo geuzeni, wawe wa sasa treni,

Dizeli iacheni umeme tutumieni,

Uchina shirikianeni, mwokoe zetu laini,

Wachawi saidieni, tupate maendeleo.

 

 

Maji huko maziwani, uchawi mtumieni,

Yapande hadi nyikani, tunawesha mashambani,

Tutumie na mijini maana hayaonekani,

Wachawi tusaidieni, tupate maendeleo.

Share Bookmark Print

Rating