Washairi Tanzania

Imepakiwa Monday March 4 2019 | Na Nyembo Atwai Nyembo

Hadi hodi gazetini, kwenu naja kurasani,

Niweke japo pembeni, nisomeke hadharani.

Niyatowe ya moyoni, kwa washairi nchini,

Washairi Tanzania, tengenezeni umoja.

Ni ukweli usopingika, kutengeneza kikundi,

Washairi kuunganika na kutoweka kilindi,
Mwisho tutanufaika, kwa kupitia  kikundi,

Washairi Tanzania, tengenezeni umoja.

Mbetumbetu tuwe moja, shime na tubebe dhima,

Nguvu yetu kuwa moja, tujenge yaliyo mema,

Kikundi ni nguvu moja, kwa kauli ya Karima,

Washairi Tanzania, tengenezeni umoja.

Wa bara na visiwani, wote tuwe kundi moja,

Tukitoka hadharani, na tulonge lugha moja,

Jahazi litoke chini, kwa nguvu jasho kuvuja,

Washairi Tanzania, tengenezeni umoja.

Watunzi wale watangu, na hawa wa zama hizi,

Katu tusiwe  mafungu, kama jani na mizizi,

Tushiriki ndugu zangu, kwa ukweli na uwazi,

Washairi Tanzania, tengenezeni umoja.

Vyama vimekuwa vingi, wakati dhana ni moja,

Vingine siyo msingi, ushairi vinatija,

Twajiwekea vigingi, kutokuivuka moja,

Washairi Tanzania, tengenezeni  umoja.

Umoja ni nguvu sana, waliyasema wahenga,

Watu ni kushikamana, kwa malengo ya kujenga,

Kwa nini tunatengana, kama wachezao vanga

Washairi Tanzania, tengenezeni umoja.

Kalamu naweka chini, naikunja karatasi,

Niiweke bahashani, shairi langu jepesi,

Nitume gazetini nikawatowe ugwasi, 

Washairi Tanzania, tengenezeni umoja.

Share Bookmark Print

Rating