ZAMA ZA HAPA KAZI

Imepakiwa Monday March 4 2019 | Na Shaaban Maulidi maulidishaaban54@gmail.com

Ni zama za Magufuli, John Pombe wa Josefu, 
Kuongoza serikali, ya taifa takatifu, 
Niwa chuma mhimili, kiboko ya wakosefu, 
Ni zama za hapa kazi, wavivu kaeni kando.

Ni rais wa wanyonge, mkombozi Tanzania, 
Msururu tuupange, medai kwenda kuvaa, 
Tukalimiliki tonge, John Pombe ni Shujaa, 
Zama za hapa kazi, wavivu kaeni kando.

Zama za kujenga nchi, kuondoa mafisadi, 
Zama zetu wananchi, nchi yetu kufaidi, 
Zama siyo za wadachi, kujidai yatubidi, 
Ni zama za hapa kazi, wavivu kaeni kando.

Tanzania ya viwanda, ndiyo sasa inajengwa, 
Uchumi nao wapanda, hilo si la kupingwa, 
Rasilimali kulinda, nchi isiwe jangwa, 
Ni zama za hapa kazi, wavivu kaeni kando

Za kujenga barabara, mijini na vijijini, 
Kuijenga reli bora, ya kwenda mikoani, 
Na daraja la Tazara, magari pita hewani, 
Ni zama za hapa kazi, wavivu kaeni kando.

Ndege tatu kwa mpigo, usarifi wa angani, 
Bandari kutega tego, kuwakamata wahuni, 
Na viongozi mizigo, wamekimbia gizani, 
Ni zama za hapa kazi, wavivu kaeni kando.

Zama za kutema rushwa, siyo zama za kuila, 
Uvivu unakomeshwa, kufanya kazi ni kula, 
Ajira za kurithishwa, hivi sasa zimelala, 
Zama za hapa kazi, wavivu kaeni kando.

Siyo zama za Ulaya, ni zama za majimboni, 
Zile posho posho mbaya, kupeana vikaoni, 
Zama za kuchuja chuya, mchele ubaki ungoni, 
Zama za hapa kazi, wavivu kaeni kando.

Siyo zama za kupinga, elimu sasa ni bure, 
Zama mkono kuunga, sote tuwe saresare, 
Kwa pamoja tunapanga, kuyarudi ya nyerere, 
Zama za hapa kazi, wavivu kaeni kando.

Twende mbele rudi nyuma, huo ndiyo mwendo bora, 
Kama baba wa huruma, tena aliye busara, 
Fumbua macho tazama, kisha uchore dira, 
Zama za hapa kazi, wavivu kaeni kando.

Tazama sisi wanao, tuliotumwa kusoma, 
Sikia chetu kilio, tungali bado twahema, 
Hlaafu tega sikio, irudi yetu heshima,
Zama za hapa kazi, wavivu kaeni kando.

Wape vijana ajira, walomaliza kusoma,
Sanaa sio hasara, sisi ni walimu wema,
Tukipata mishahara, kwetu sisi ni salama,
Zama za hapa kazi, wavivu kaeni kando.

Zama za hapa kazi, twaomba mtupe kazi,
Tazama haya machozi, ya BAED yetu kozi,
Sisi ni wachapakazi, tupeni tupige kazi,
Zama za hapa kazi, wavivu kaeni kando.

 

Share Bookmark Print

Rating