http://www.swahilihub.com/image/view/-/4890032/medRes/2194553/-/xcsjbwz/-/maria.jpg

 

Aina mbalimbali za uundaji msamiati katika Kiswahili

Mary Wangari

Mwandishi Mary Wangari. Picha/MAKTABA 

Na MARY WANGARI

Imepakiwa - Friday, January 11  2019 at  14:25

Kwa Muhtasari

Kuna njia mbalimballi za uundaji wa istilahi katika lugha ambazo ni pamoja na kubadili mpangilio wa herufi, kuambatanisha maneno, kutohoa maneno ya lugha nyingine, uambishaji wa maneno na kufanikisha sauti, umbo, mlio na sura.

 

BAADA ya kujifahamisha kuhusu historia ya uundaji wa istilahi pamoja na mchakato wa uundaji istilahi, ni vyema sasa tujifahamishe kuhusu aina mbalimbali ya uundaji wa maneno katika Kiswahili. Jinsi tunavyofahamu, mojawapo wa sifa za lugha ni kwamba lugha ni hai na hukua na kubadilika kila wakati kadri  ya mabadiliko katika jamii.

Bila shaka, sifa mojawapo inayodhihirisha kukua na kubadilika kwa lugha ni kuongezeka kwa istilahi na kupanuka kwa msamiati katika lugha husika. Hata hivyo, ili istilahi au msamiati wa lugha uongezeke, ni sharti kuwe na mchakato wa uundaji wa maneno mapya.

Kuna njia mbalimballi za uundaji wa istilahi katika lugha kama zilivyoainisha ifuatavyo:

i. Kubadili mpangilio wa herufi.

ii. Kuambatanisha maneno

iii. Kutohoa maneno ya lugha nyingine.

iv. Uambishaji wa maneno.

v. Kufanikisha sauti, umbo, mlio na sura.

             

UTOHOZI

Mbinu hii inahusisha kutohoa maneno kutoka lugha chanzi na kuyafanyia marekebisho kwa kufuata kaida au sheria za kifonolojia na kimofolojia za lugha pokezi na hatimaye kuyatumiwa.

Kwa mujibu wa Matinde (2012), neno linapotoholewa hutamkwa na kuandikwa kwa utaratibu wa lugha pokezi.

Hata hivyo, maana ya neno lililotoholewa hubakia ileile ya awali.

Lugha yoyote ile haiwezi kujitosheleza kivyake. Kila lugha huwa na mazoea ya kutwaa maneno ya lugha nyingine ili kukidhi mahitaji yake ya msamiati.

Maneno kutoka lugha chanzi yanapoteuliwa hukarabatiwa na kubadilishwa kimatamshi ili yafuate kanuni au ukipenda sarufi ya lugha pokezi.

Kwa mfano, katika lugha ya Kiswahili, baada ya maneno kutoholewa kutoka lugha chanzi, ni sharti yasanifishwe na Baraza Kiswahili la Taifa (BAKITA) kabla ya kuruhusiwa kutumika rasmi.

Kiswahili kinasheheni maneno kadha yaliyotoholewa kutokana na lugha mbalimbali mathalan: salamu (Kiarabu), dukani (Kihindi) shule (Kijerumani.

 

Mifano ya baadhi ya maneno yaliyotoholewa katika Kiswahili kutokana na lugha ya Kiingereza ni kama vile:

 

Kiingereza

Kiswahili

Budget

bajeti

Lorry

lori

Blouse

blauzi

miniskirt

minisketi

shirt

shati

Agenda

ajenda

Account

akaunti

bank

benki

picture

picha

 

Baruapepe ya mwandishi: marya.wangari@gmail.com

Marejeo:

 

Ndungo, C. & Mwai, W., (1991). Kiswahili: Historical Modern Development in Kiswahili. Nairobi: Nairobi University Press.

Mbaabu, I., (1996). Language Policy in East Africa: A Dependency Theory Perspective. Nairobi: Educational Research and Publications.

Masebo, J.A. & Nyangwine A. D. (2002). Nadharia ya Lugha: Kiswahili 1. Dar es Salaam: Afroplus Industries Ltd.

Je, una swali, maoni au mapendekezo kwa Swahili Hub? Tuandikie kupitia baruapepe: swahilihub@ke.nationmedia.com