Ala za sauti za lugha katika Fonetiki

Na MARY WANGARI

Imepakiwa - Tuesday, December 4  2018 at  13:25

Kwa Muhtasari

Maelezo ya ala za sauti za lugha yametolewa hapa.

 

KATIKA makala iliyopita tulianza uchambuzi wa ala za sauti ambapo tuliangazia viungo mbalimbali vinavyohusika katika mchakato wa sauti.

Hii leo tutaangazia kwa kina alasauti za lugha na kujifahamisha na viungo hivyo vyema zaidi. Hii leo tutaendeleza mada hiyo kwa kuichambua na kuitathmnini kwa kina.

Baada ya kutoka kwa hewa kupitia katika koromeo hewa huelekea katika chemba ya sauti ambayo huishia katika mkondo hewa wa pua au kinywa.Wakati hewa inasafiri huweza kutatizwa katika mkondo wake wa hewa, kutokana na kutatizwa huku katika sehemu mbalimbali za mkondo wa hewa tunapata sauti mbalimbali.

 

Alasauti hizo mbalimbali ni kama zifuatazo:

 

Koromeo

Ni bomba la sauti ambalo huanzia katika kanda za sauti upande wa chini zaidi wa shina la ulimi. Koromeo ina urefu wa sentimita nane kwa wanaume na takribani sentimita saba kwa wanawake. Mwisho wake huwa imegawanyika katika sehemu kuu mbili, ya kwanza ikielekea katika chemba cha kinywa na ya pili katika chemba cha pua.

Kazi ya koromeo katika uzalishajiwa sauti ni kupitisha hewa ambayo hutatizwa sehemu mbalimbali za mkondo wa hewa.

 

Kaa kaa laini

Ni ala sauti ambayo inaonekana katika sehemu inayoruhusu hewa kupika katika chemba ya pua na chemba ya kinywa.Wakati wa utoaji wa sauti, ala hii huinuka ili kuruhusu hewa kupita katika chemba ya kinywa na hivyo kuzalisha sauti za kinywa au hulala na kuruhusu hewa kupita katika chemba ya pua na hivyo kuzalisha sauti za puani.

Vilevile ala hii ni muhimu katika uzalishaji wa sauti kama [k], [g],wakati shina la ulimi linapoinuka na kugusa kaa kaa laini.

 

Kaa kaa gumu au Paa la Kinywa

Husaidia katika kutamka sauti kama vile [∫], ambazo huitwa sauti za kaa kaa gumu.

 

Ufizi

Ni kituta kilichopo kati ya kaakaa gumu na meno ya mbele ya juu unaweza kuhisi maumbile yake kwa kugusa na ncha ya ulimi. Hutumika kuzalisha sauti za ufizi kama, [t], na [d].

 

Ulimi

Ni ala muhimu sana katika matamshi, huweza kujongea sehemumbali mbali za chemba ya kinywa. Umegawanyika katika sehemu kuu tatu ambazo ni ncha ya ulimi, bapa la ulimi na shina la ulimi.

 

Marejeo:

 

Masebo, J.A., Nyangwine A. D., (2002). Nadharia ya Lugha: Kiswahili 1. Dar es Salaam: Afroplus Industries Ltd.

Massamba, D.P.B., (2002). Historia ya Kiswahili 50 BK., Nairobi: Jomo Kenyatta Foundation.

Ipara, I. O., Waititu, F.G., (2006). Ijaribu na Uikarabati. Nairobi: Oxford University Press.

Habwe, J., (2006). Darubini ya Kiswahili. Nairobi: Phoenix Publishers.