Asili ya Lugha

Na MARY WANGARI

Imepakiwa - Wednesday, November 21  2018 at  13:49

Kwa Muhtasari

Hakuna maafikiano miongoni mwa wanaisimu kuhusu ni wapi, lini, namna gani na nani hasa aliyeanzisha lugha.

 

TUNAPOANZA uchambuzi wa mada kuhusu chimbuko la lugha, ni muhimu kufahamu kwamba hakuna maafikiano miongoni mwa wanaisimu kuhusu ni wapi, lini, namna gani na nani hasa aliyeanzisha lugha.

Hali hii inatokana na kwamba binadamu alianza kuishi tangu jadi wakati ambao bado haujajulikana.

Hata hivyo, jambo la hakika ni kwamba lugha hutumiwa na mwanadamu ambapo kila jamii ina lugha yake mahususi.

Kuna nadharia mbalimbali zinazoeleza chanzo na asili ya lugha jinsi zilivyofafanuliwa ifuatavyo:

Nadharia ya mtazamo wa kidini au ya Uungu

Nadharia hii inajikita katika msingi kuwa lugha iliumbwa na Mungu na ikapatiwa mwanadamu kwa nguvu za Mola.

Aidha, nadharia hii inaeleza kuwa, haja ya Mungu kuwasiliana na kiumbe wake Binadamu ndiyo iliyomfanya aumbe lugha.

Inaaminika kuwa Mungu ndiye alikuwa wa kwanza kutumia lugha maadamu aliumba ulimwengu kwa kutumia neno, na kwa kupitia neno kila kitu akiwemo mwanadamu kikawa.

Vilevile, inaaminika kwamba lugha zote zilitokana na lugha moja iliyoumbwa na Mungu. Hata hivyo kuna visasili mbalimbali vinavyoeleza asili ya lugha katika nadharia ya Uungu.

Kwanza ni pale Mungu alipompa Adamu uwezo wa kuzungumza kwa kuwatajia majina wanyama wote na pale ndipo lugha ilipoanza.

Visasili vinginevyo ambavyo vimechangia nadharia hii ni pamoja na vya Wamisri, Wababiloni, na Wahindi.

Kisasili cha Mnara wa Babeli

Kwa mujibu wa kisasili hiki cha Wababiloni, ni kwamba hapo kale Mfalme wa Babeli aliamrisha kujengwa kwa mnara mrefu ulioitwa Mnara wa Babeli ili kumfikia Mungu.

Kwa lengo hilo Mungu alikasirishwa sana akaamua kuwachanganya lugha wajenzi wa mnara huo hivyo wakashindwa kuzunguma kwa sauti moja na wakakosa kuelewana na hatimaye azma yao ikasitishwa.

Hivyo basi, kutokana na imani hiyo waumini wengine wanakubali kuwa yawezekana lugha nyingi zinazoonekana leo ni tokeo la mnara wa Babeli.

Isitoshe, Wamisri wanatilia mkazo zaidi nadharia hii kwa kuwa na Mungu wao aliyeitwa Thoth ambaye ni Mungu wa Lugha.

Wahindu walihusisha uwezo wa mwanadamu wa kuzungumza na 'mungu wao aliyeitwa Brahma'.

Kulingana na imani ya Kihindi Brahma ndiye Mungu aliyeumba ulimwengu lakini lugha akapatiwa mwanadamu kutoka kwa mke wake aliyeitwa Sarasvati.

Marejeo:

Cook, V.J. (1969), 'The analogy between first and second language learning', International Review of Applied Linguistics, VII/3, 207-216

Habwe, J., na Karanja, P. (2004). Misingi ya Sarufi ya Kiswahili. Nairobi: Phoenix Publishers.

Halliday, M.A.K. (2003). On Language and Linguistics, Jonathan Webster (ed.), Continuum International Publishing.

King’ei, K. (2010). Misingi ya Isimu Jamii. Taasisi ya Taaluma za Kiswahili: Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Tanzania.

Mario A. P. and Gaynor, F. (1954). A Dictionary of Linguistics Philosophical Library. New York