Historia pamoja na changamoto zinazokabili ufundishaji wa isimu kwa Kiswahili

Na MARY WANGARI

Imepakiwa - Tuesday, July 11  2017 at  19:38

Kwa Mukhtasari

Kiswahili kinakabiliwa na changamoto tele katika ufundishaji wa isimu ikiwemo katika nyanja za usawazishaji wa istilahi, tafsiri, mfumo au ukipenda kozi nzito.

 

KATIKA makala ya awali tuliangazia mada ya dhana kuhusu ujuzi wa lugha na mjua lugha.

Baada ya kuchambua na kuchanganua tawi la isimu katika Kiswahili, hii leo ni vyema tuangazie kuhusu matatizo yaanayokumba Kiswahili kama lugha ya kufunza isimu.

Kiswahili kinakabiliwa na changamoto tele katika ufundishaji wa isimu ikiwemo katika nyanja za usawazishaji wa istilahi, tafsiri, mfumo au ukipenda kozi nzito.

Ni muhimu kufahamu kuwa lugha ya Kiswahili kando na kuwa lugha ya Taifa na lugha rasmi nchini, vilevile hufundishwa kama taaluma katika vyuo vikuu vote nchini pamoja na vyuo vishiriki.

HISTORIA YA UFUNDISHAJI ISIMU NCHINI KENYA

Idara ya ufunzaji isimu nchini ilianzishwa mnamo 1969 katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

Baadaye vyuo vikuu vingine mathalan Chuo Kikuu cha Kenyatta na Chuo Kikuu cha Egerton, vilianzisha idara za Kiswahili ambapo lugha na isimu hufunzwa.

Chuo kikuu cha Moi kilipoanzishwa mnamo 1987, kilianza kufundisha Kiswahili mara moja

Kwa mujibu wa ripoti ya Mackay iliyopendekeza kuanzishwa kwa chuo kikuu cha pili, ripoti hii ilipendekeza kwamba Kiswahili kifundishwe katika chuo chote kwa wanafunzi wote

Si ajabu kwamba wanafunzi wa mwanzo 1990/91 wote walifundishwa Kiswahili. Licha ya kufundisha Kiswahili,lugha za Kiafrika hugusiwa kwa kiasi kufanikisha mafunzo ya isimu.

Pamoja na kufundisha lugha ya Kiswahili, chuo kikuu cha Maseno kilianza idara inayojisimamia lugha za Kiafrika.

Lugha zinazofundishwa ni pamoja na Ekegusii, Kikalenjin, Kiluhyia na Kidholuo.

Katika vyuo hivi vyote Kiswahili hufundishwa katika viwango vya shahada ya digrii, shahada ya uzamili pamoja na shahada ya uzamifu.

Jinsi tunavyofahamu kufikia sasa ni kwamba, somo la isimu na lugha limeathiriwa na ufunzaji wa masomo mengine.

Hii inatokana na sababu kwamba, idara nyingine za isimu katika baadhi ya vyuo vikuu hivi ndizo kwa sasa zinashughulikia isimu ya lugha nyinginezo ikiwamo Kiingereza, Kiarabu, Kijerumani, Kifaransa na kadhalika.

Vyuo vikuu kama Moi na Maseno vina idara ya Kiswahili inayoshughulikia somo la lugha, fasihi na isimu.

Katika Chuo Kikuu cha Egerton na chuo cha Laikipia taaluma zinazofundishwa ni pamoja na lugha, isimu na fasihi katika idara moja.

Jambo muimu la kufahamu ni kuwa, karuibu katika vyuo vikuu hivi vyote,isimu ya Kiswahili ilifundishwa kwa lugha ya Kiingereza pengine isipokuwa katika Chuo Kikuu cha Moi na Maseno.

Changamoto kuu inayojitokeza ni kuwa yamkini mpangilio uliopo umeiweka isimu ya Kiswahili pembeni na kutilia maanani zaidi isimu ya lugha nyinginezo za kigeni.

Matatizo yanayokabili somo la isimu kwa Kiswahili

1. Ukosefu wa vipindi vya kutosha

Akilalamikia kuhusu ufundishaji wa Kiswahili kwa jumla katika vyuo vikuu Kitsao (1978:74) anatoa hoja kwamba; hakuna vipindi vya mafunzo ya Kiswahili kwa sababu tunachukulia kwamba wanafunzi wa Kiswahili watakuwa tayari wamepata msingi wa kutosha wa lugha ya Kiswahili katika elimu yao kabla ya kujiunga na chuo kikuu.

Hivyo basi, kuwafundisha Kiswahili kwa kina darasani kutakuwa ni kama kuwapotezea wakati kwa mambo 'wanayoyajua'.

Si ajabu basi kwamba asilimia kubwa ya wanafunzi wa lugha ya Kiswahili vyuoni huwa hawafanyi vyema katika somo la isimu ikilinganishwa na masomo mengine yanayofundishwa na idara nyingine za Kiswahili na lugha nyinginezo za Kiafrika.

2. Idadi chache ya somo kuhusu uchanganuzi wa lugha

Katika ufundishaji wa lugha ya Kiswahili vyuoni, baadhi ya kozi huwa ni za lazima huku nyingine zikiwa za hiari.

Kwa kutazama kwa kina, utagundua kuwa kozi zinazohusu uchanganuzi wa lugha ni chache mno zikilinganishwa na zile za ufundishaji wa fasihi na vipengele vinginevyo.

3. Kupuuza misingi ya Nadharia

Aidha, ni bayana kwamba masomo yanayohusu uchanganuzi wa nadharia hayatiliwi mkazo inavyofaa ikilinganishw ana uchanganuzi wa nadharia za tawi la fasihi.

Kozi zinazolenga isimu ya Kiswahili na uchanganuzi wa lugha ya Kiswahili moja kwa moja ni chache na zinafaa kupanuliwa na kuchunguzwa upya.

MAREJELEO

King'ei, Kitula. 2000 Research in African Languages.

Massamba, D., Y Kihore & L Hokororo. 1999. Sarufi Miundo ya Kiswahili Sanifu.. Dar e Salaam: TUKI

Unalo swali? Muulize mwandishi kupitia anwani:marya.wangari@gmail.com