Fasili za wataalamu mbalimbali kuhusu dhana ya Fonetiki

Na MARY WANGARI

Imepakiwa - Tuesday, December 4  2018 at  11:03

Kwa Muhtasari

Fonetiki ni taaluma ya kisayansi inayochunguza sauti za lugha ya mwanadamu bila kujiegemeza kwa lugha yoyote mahususi.

 

KWA mujibu wa Habwe na Karanja (2004), fonetiki ni taaluma ya kisayansi inayochunguza sauti za lugha ya mwanadamu.

Fonetiki hutimiza jukumu hili kwa kuchunguza sauti za lugha ya mwanadamu jinsi zinavyotamkwa, kusafirisha katika kinywa cha mnenaji na sikio la msikilizaji na jinsi zinavyofasiliwa katika ubongo wa msikilizaji.

Ni vyema kutilia maanani kuwa fonetiki hushughulikia sauti zile za lugha ya mwanadamu zinazowezesha mazungumzo kwa ujumla wake bila kujali sauti hizi ni za lugha gani.

Nao Massamba et al (2007), wanasema katika Taaluma ya Isimu, fonetiki ni tawi ambalo hujishughulisha na uchunguzi na uchambuzi wa taratibu zote zinazohusiana na kutoa, kutamka, kusafirisha, kusikia na kufasili sauti za lugha za binadamu kwa ujumla.

Jambo la msingi katika tawi hili ni kuchunguza maumbo mbalimbali ya sauti zinazoweza kutolewa na alasauti, namna maumbo hayo yanavyoweza kutolewa, yanavyoweza kumfikia msikilizaji (yanavyosikika) na yanavyofasiliwa katika ubongo; bila kujali kama sauti hizo zinatumika katika lugha fulani.

Mwanafonetiki huchunguza pia maumbo ya mawimbi ya sauti kwa kuangalia namna maumbo hayo yanavyoathiri hewa wakati wa utoaji wa sauti. Katika harakati hizi mwanafonetiki huweza kutoa sifa mbali mbali za sauti na kuzitambulisha.

Sifa au nduni bainifu – Hizi ni sifa zinazotumika katika kutambulisha sauti mbalimbali za lugha.

 

 

Tanzu au Matawi Fonetiki

Jinsi tulivyotaja awali, taaluma ya fonetiki inasheheni matawi madogomadogo manne tutakayoyaangazia kwa kina jinsi ifuatavyo; tukianza na aina mbili:

1. Fonetiki Matamshi

Tawi hili huchunguza na kupambanua jinsi sauti mbalimbali za lugha zinavyotamkwa kwa kutumia alasauti.

Aidha, tawi hili hubainisha sauti za lugha kwa kuchunguza harakati za alasauti zinazohusika.

 

2. Fonetiki Akustika (Fonetiki Mawimbi-Sauti)

Ni utanzu wa fonetiki unaochunguza namna na jinsi sauti inavyosafiri hewani.

Habwe na  Karanja, (2007) wanaeleza kuwa, wakati wa utamkaji kuna namna mawimbi ya sauti yanavyoathiri hewa na kufanya mawimbi yanayowakilisha muundo-mawimbi wa sauti inayohusika.

Kazi ya mwanafonetiki ni kuchunguza mawimbi-sauti haya kwa kufanya uchunguzi katika maabara ya lugha kwa kutumia vifaa maalumu mathalan spektogramu.

 

Marejeo

 

Whiteley, W.H., (1969). Swahili: The Rise of a National Language. London: Methuen and Company Limited.

Chiraghdin, S., & Mnyampala, M. (1977). Historia ya Kiswahili. Nairobi: Oxford University Press.

Richards, C. (1984), Error Analysis Perspectives on Second LanguageAcquisition, London, Longman Group Ltd.

Wardhaugh, R., (1986). An Introduction to Socio- Linguistics. New York: Blackwell Publishers.