Dhana ya lugha kulingana na fasili za wataalamu mbalimbali

Na MARY WANGARI

Imepakiwa - Wednesday, November 14  2018 at  18:15

Kwa Muhtasari

Chomsky (1957) anasema lugha ni seti ya idadi ya sentensi zinazojitosheleza, kila idadi inajitosheleza kwa urefu na hujengwa kutokana na seti za elementi zinazojitosheleza.

 

NOAM Chomsky (1957) anasema lugha ni seti ya idadi ya sentensi zinazojitosheleza, kila idadi inajitosheleza kwa urefu na hujengwa kutokana na seti za elementi zinazojitosheleza.

Michael Halliday (2003): Anafafanua lugha kama mfumo wa maana, yaani mfumo wa ishara.

Muharrem Ergin(1990): Kwa mujibu wa mtaalamu huyu, lugha ni njia ya asili ya kuwezesha mawasiliano miongoni mwa watu, ni chombo kilicho hai chenye kanuni zake za pekee ambazo pekee yake hujijenga. Ni mfumo wa makubaliano ambao misingi yake iliwekwa katika wakati usiojulikana na ni taasisi ya kijamii ambayo imechangamana na sauti.

Sapir (1921:7) Kulingana naye, lugha ni njia ya mawasiliano ambayo ni maalumu kwa mwanadamu na ambayo hutumiwa kuwasilisha mawazo, hisia na matakwa kwa kutumia ishara ambazo hutolewa kwa hiari.

Mario Pei & Frank Gaynor (1954) Wanasema lugha ni mfumo wa mawasiliano kwa njia ya sauti, yaani, kwa kutumia alasauti nakusikia, miongoni mwa binadamu wa kundi fulani au jumui ya kwa kutumia ishara-sauti ambazo maana zake hueleweka kwa unasibu tu.

Ni dhahiri kutokana na fasili hizo za wanaisimu mbalimbali kwamba kuna maana mbalimbali za lugha.kulingana na taaluma, mazoea, mazingira au hata mahali mtu alipobobea kitaaluma.

Hata hivyo, kando tofauti hizi mbalimbali zinazojitokeza, ni bayana kwamba kuna sifa kadha za kimsingi ambazo tariban wataalam wote wanaafikiana katika fasili zao za dhana ya lugha.

Lugha ina sifa bainifu zifuatazo:

  1. Lugha huzaliwa - huchipuka kutokana nalugha nyingine moja au zaidi zilizotangulia kuwepo.kupitia  kuongezeka kwa maneno, kuongezeka kwa idadi ya wazungumzaji, kuwa na mawanda mapana, kusanifiwa.
  2. Lugha hutohoa:-  lugha ina tabia ya kuchukua au kukopa maneno kutoka lugha nyingine.

  3. Lugha hufundishika: - mtu yeyote anaweza kujifunza angalau kiasi lugha yoyote hata kwa njia ya ufundishaji.

  4. Lugha huathiriana - lugha yoyote inaweza kuathiriwa na lugha nyingine.

  5. Lugha lazima ijitosheleze - kila lugha inajitosheleza kulingana na mahitaji ya jamii inayotumia lugha yenyewe.

  6. Lugha zina ubora - lugha zote ni bora hakuna lugha bora kuliko nyingine zote.

  7. Lugha hurithiwa-  jamii hurithi lugha kutoka kizazi hadi kizazi.

  8. Lugha hufa - inapozidi mno kubadilika hadi mwishoni inakuwa tofauti kabisa, au inapokosa kutumika kabisa kwa kuwa wahusika wanapendelea lugha nyingine.