Dhana ya lugha na isimu katika Kiswahili

Na MARY WANGARI

Imepakiwa - Thursday, June 15  2017 at  09:02

Kwa Mukhtasari

Tunaweza kufasili dhana ya lugha kwa mujibu wa mitazama miwili ifuatayo; Mtazamo finyu (narrow conception) na mtazamo mpana (broad conception).

 

KATIKA makala hii tutaangazia mada kuhusu lugha na isimu kama ifuatavyo;

Dhana ya Lugha

Tunaweza kuangazia kipengele hiki kwa kujiuliza kwanza, lugha ni nini? Ama kwa hakika swali hili linaweza kuchukuliwa kama la kijinga pengine ni kwa sababu huwa hatupendi kutilia maanani katika vitu ambavyo tunachukuliwa kuwa vya kawaida.

Ni jambo nzuri kuwa mambo hayawi kama tunavyoyaona au kuyatafakari.

Kwa mintarafu hiyo tunaweza kufasili dhana ya lugha kwa mujibu wa mitazama miwili ifuatayo;

 

1.       Mtazamo finyu (narrow conception)

2.      Mtazamo mpana (broad conception).

 

1.      Mtazamo Finyu:

Kwa mujibu wa mtazamo finyu, dhana ya lugha inaweza kufasiliwa kama chombo cha mawasiliano.

Fasili hii ya kutazama lugha kama tu chombo cha mawasiliano inawezesha ufahamu wa kawaida.

Hata hivyo, hii ina maana kuwa bado kuna taarifa muhimu zinatengwa katika fasili hii na hivyo basi kusababisha udhaifu huu

Udhaifu/ Upungufu wa Mtazamo Finyu wa Lugha

1.      Kueleza  lugha kama chombo cha mawasiliano ni kueleza dhima au ukipenda kazi ya lugha na wala sio maana ya lugha yenyewe.

2.      Kwa mfano, mtu akipiga ngoma ili kuwaita watu nao watu wakaja basi milio ya ngoma ni lugha vilevile maadamu imewasilisha ujumbe unaokusudiwa. Kwa maana hiyo kila kitu kinachowezesha watu kuwasiliana na kuelewana baina yao basi ni lugha.

Iwapo lugha itafafanuliwa kama chombo tu cha mawasiliano, itamaanisha kuwa hakuna tofauti kati ya mazungumzo baina ya watu na milio mbali mbali kama vile honi ya gari, filimbi ya refa uwanjani, au kengele  kanisani au hata sauti inayotokana na kugonga mlango wakati mtu anabisha hodi.

Hivyo basi dhana hii ni potofu na inatupeleka mbali zaidi na kutufanya tuanze kuitazama fasili ya lugha kwa mtazamo mwingine tofauti zaidi.

 

2.      Mtazamo Mpana.

Kuna wanaisimu wengi wa lugha amabo wamejaribu kutoa fasili mbalimbali kwa misingi ya dhana hii. Baadhi ya fasili hizo ni kama zifuatazo;

Wanavyosema wanaisimu

Todd (1987) Mwanaisimu huyu anaeleza fasili ya lugha kama mfumo wa ishara ambazo kwazo watu huwasiliana.

Kamusi ya Isimu na Lugha (1990) inaeleza kuwa lugha ni mfumo wa sauti nasibu zinazotumiwa na watu wa jamii wenye utamaduni unaofanana ili kuwasiliana.

Cook, 1969:12 Mtaalam huyu wa lugha anasema kuwa lugha ni mfumo wa sauti nasibu na ishara za kisarufi ambazo kwazo watu wa jamii fulani ya lugha huwasiliana na kupokezana utamaduni wao.

Bloch & Trager (1942): Lugha ni mfumo wa sauti za nasibu ambazo kwazo makundi ya kijamii hushirikiana.

Noam Chomsky (1957): Mwanaisimu huyu anasema kuwa lugha ni seti ya idadi ya sentensi zinazojitosheleza, kila idadi inajitosheleza kwa urefu na hujengwa kutokana na seti za elementi zinazojitosheleza.

Michael Halliday (2003): Anaeleza kuwa lugha ni mfumo wa maana; yaani mfumo wa ishara.

Muharrem Ergin (1990): Anafafanua kuwa lugha ni njia ya asili ya kuwezesha mawasiliano miongoni mwa watu, ni chombo hai yaani chenye sheria zake za pekee ambazo kwazo peke yake hujijenga.

Ni  mfumo wa makubaliano ambao misingi yake iliwekwa katika wakati usiojulikana, na ni taasisi ya kijamii ambayo imechangamana na sauti.

Lugha ni mfumo wa sauti za nasibu ambazo tunazitumia kusimba uelewa na uzoefu wetu wa ulimwengu.

Naye Sapir (1921:7 anatoa fasili ya lugha akisema ni njia ya mawasiliano ambayo ni maalumu kwa mwanadamu na ambayo hutumiwa kuwasilisha mawazo, hisia na matakwa kwa kutumia ishara ambazo hutolewa kwa hiari.

Mario Pei & Frank Gaynor (1954) Kamusi ya Isimu, anasema kuwa; Lugha ni mfumo wa mawasiliano kwa njia ya sauti, yaani, kwa kutumia ala za sauti na kusikia, miongoni mwa binadamu wa kundi fulani au jumuiya kwa kutumia ishara-sauti ambazo maana zake hueleweka kwa unasibu tu.