http://www.swahilihub.com/image/view/-/3475296/medRes/1247498/-/e60ndvz/-/353965-01-02%25286%2529.jpg

 

Dhana ya lugha

Vitabu

Vitabu vikiuzwa awali. Picha/AFP 

Na MARY WANGARI

Imepakiwa - Thursday, November 15  2018 at  07:07

Kwa Muhtasari

Iwapo lugha ni chombo tu cha mawasiliano, basi inamaanisha kwamba hakuna tofauti yoyote kati ya kuzungumza na milio mbalimbali mathalani filimbi ya refa uwanjani, kengele shuleni, honi ya gari au hata mtu anapobisha mlango.

 

KATIKA makala ya leo tutashughulikia swali kutoka kwa msomaji wetu kwa namna ifuatavyo:

Je, ni nadharia zipi zinaeleza chimbuko la lugha ya binadamu. Kutokana na sauti za asili, za furaha na ishara za mwili zinazotokana na mazingira ya binadamu?

Kabla ya kuangazia kwa kina swali hili, ni vyema kutanguliza kwa kufafanua dhana ya lugha ili tupate ufahamu bora.

Maana ya lugha

Dhana ya lugha inaweza kufasiliwa kwa kutumia mitazamo miwili jinsi ifuatavyo:

 

Mtazamo finyu

Kwa kuegemea mtazamo huu, lugha inafafanuliwa kama chombo cha mawasiliano.

Hata hivyo, kuiangazia lugha kama tu chombo cha mawasiliano kunawezesha ufahamu wa kawaida.

Ni bayana kwamba mtazamo huu unaacha taarifa muhimu hivyo basi kuwa na udhaifu ufuatao:

Kufafanua lugha kama chombo cha mawasiliano ni kueleza kazi ya lugha na sio lugha yenyewe.

Vilevile, mawasiliano yanaweza pia kufanyika kwa kutumia nyenzo kama vile mtu anaweza kupiga ngoma au kengele ili kuwaita watu na watu wakaja basi milio ya ngoma au kengele  itakuwa ni lugha. Hivyo basi, kwa maelezo haya, kila kitakachowawezesha watu kuwasiliana kitakuwa ni lugha.

Iwapo lugha ni chombo tu cha mawasiliano, basi inamaanisha kwamba hakuna tofauti yoyote kati ya kuzungumza na milio mbalimbali mathalani filimbi ya refa uwanjani, kengele shuleni, honi ya gari au hata mtu anapobisha mlango.

Dhana hii si kweli na linatupeleka mbali zaidi na kutufanya tuanze kuitazama fasili ya lugha kwa mtazamo tofauti zaidi.

Mtazamo mpana

Katika mtazamo huu, tutachambua dhana ya lugha kwa mujibu wa wanaisimu chungunzima ambao wamejaribu kufafanua dhana ya luigha kwa kutoa fasili anuai jinsi ifuatavyo:

 

Kamusi Sanifu ya Isimu na Lugha (1990), inafafanua lugha kama mfumo wa sauti nasibu zinazotumiwa na watu wa jamii wenye utamaduni unaofanana ili kuwasiliana.

 

Kulingana na Cook (1969), "lugha ni mfumo wa sauti nasibu na ishara za kisarufi ambazo kutokana nazo watu wa jamii fulani ya lugha huwasiliana na kupokezana utamaduni wao." uk. 15

Todd (1987), anasema lugha ni mfumo wa ishara ambazo kupitia kwazo watu huwasiliana.

 

Bloch na Trager (1942) wanaeleza lugha kama mfumo wa sauti za nasibu ambazo kupitia kwake makundi ya kijamii hushirikiana.

 

MAREJEO:

Chomsky, N. (1957). Syntactic Structures. The Hague: Mouton.

Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (Tuki) (1990). Kamusi Sanifu ya Isimu na Lugha. Dar es Salaam: Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.