Dhana ya Upwa wa Afrika Mashariki ikiwemo maenezi ya Kiswahili

Na MARY WANGARI

Imepakiwa - Monday, December 3  2018 at  11:29

Kwa Muhtasari

Ipo dhana kwamba Kiswahili kilitokana na jina la Upwa wa Afrika Mashariki.

 

TUNAPOENDELEA kufafanua kuhusu asili ya Kiswahili, ipo dhana kwamba Kiswahili kilitokana na jina la Upwa wa Afrika Mashariki.

Wazo la pili ni kwamba Kiswahili kilitokana na wageni waliuoita upwa wa Afrika Mashariki Sahil, wingi wake ukiwa Sawahili kwa maana ya pwani.

Kiambishi ‘’ki’’ kiliongezwa kuonyesha lugha na kuwa Kisuaili na hatimaye Kiswahili, jina ambalo lilianza kutumika Kaskazini mwa Kenya karibu na Lamu katika karne ya saba na nane baada ya kuzaliwa Kristo.

Aidha, ushahidi wa kihistoria unaonyesha kuwa katika Karne ya Kwanza ya Kristo, neno ‘Azania’’ limetajwa katika kitabu cha Maelezo ya Bahari Hindi (Periplus of Erythrean Sea) kutaja sehemu za Afrika Mashariki.

 

Wasafiri wengine waliozungumza juu ya lugha hii katika Afrika Mashariki ni Ibn Batuta, Ibn Masud na Al-Idris. Baadhi ya wasafiri hao wa kale walinukuliwa kutaja maneno ya Kiswahili kama vile ‘mkono wa tembo’ na ‘kisukari’ yaliyokuwa majina ya ndizi.Majina haya hata sasa yanatumika.

 

Maenezi ya Kiswahili

Misafara ya biashara iliyokuwa ikitoka pwani ya Afrika Mashariki kwenda bara ilisaidia kueneza Kiswahili. Mwanzo kabisa safari hizi zilikuwa zikifanywa baina ya Waafrika wa pwani na wale wa bara.

Kundi la pili lilikuwa la wafanyabiashara wa Kiarabu walioingia bara kutafuta pembe za ndovu na watumwa. Waarabu hawa hawakuja na ujuzi wa lugha hii

Walifundishwa na wenyeji wa pwani na bara ambao walikuwa wapagazi wao. Misafara hiyo ndio iliyoeneza Kiswahili Kongo na lahaja ya Kingwana ilizuka huko Kongo.

Maenezi ya pili yalifanywa na wamishenari. Dini za kigeni zina nafasi muhimu katika maenezi ya Kiswahili. Kwanza kabisa, Waarabu walipokuja iliwabidi kuhubiri dini yao (Kiislamu) katika lugha ya Kiarabu. Kwa kuwa wenyeji hawakujua Kiarabu, ilibidi wageni wajifunze Kiswahili ili waweze kueneza dini yao vilivyo.

Mashehe na maulama walianzisha matumizi ya maandishi ya Kiswahili wakitumia abjadi za Kiarabu.

Wamishenari kutoka Ulaya walipokuja hawakutumia Kiswahili sana kwa sababu kilihusishwa na dini ya Kiislamu. Wao walitumia zaidi lugha za kienyeji, lakini baadaye walibadilisha mtindo huo. Kwanza kabisa, ilionekana wangefanikiwa zaidi iwapo wangetumia lugha ya Kiswahili.

 

Marejeo:

Mehrabian na Ferris (1967). "Inference of Attitude from Nonverbal Communication in Two Channels". Katika: The Journal of Counselling Psychology Vol.31, 1967, uk.248-52.

Witzany, G. (2006 Plant Communication from Biosemiotic Perspective. Plant Signaling na Behavior 1 (4): 169-178