Dhana ya vikoa vya maana katika semantiki ya Kiswahili

Na MARY WANGARI

Imepakiwa - Monday, September 11  2017 at  12:30

Kwa Mukhtasari

Vikoa vya maana ni seti ya msamiati ambayo viambajengo vyake vinahusiana kiwima na kisilisila (kimlalo).

 

VIKOA vya maana ni seti ya msamiati ambayo viambajengo vyake vinahusiana kiwima na kisilisila (kimlalo).

Kuna aina mbili za mahusiano ya maneno. Visawe vya maana vinahusiana zaidi na mahusiano ya kiwima.

Mfano wa vikoa vya maana ni kama vile wanyama: punda, ng‘ombe, mbuzi, na kadhalika (yanayohusiana)

Magonjwa: maradhi ya zinaa kama vile kaswende, kisonono na kadhalika.

Kikoa cha Rangi

Wataalamu wawili, Berlin na Kay walifanya utafiti katika lugha 98 na katika utafiti wao walijikita katika rangi zinazojulikana katika lugha mbalimbali.
Baada ya hapo waliangaziaya lugha 20 zinazoshiriki rangi mbalimbali. Katika utafiti wao waliandika kitabu chenye anwani Basic Colour terms mwaka 1969. Majumuisho yalikuwa kwamba;

Kuna jumla ya rangi 11 ambazo zipo katika vikoa sita na kwamba kila lugha duniani huteua rangi zake miongoni mwa 11

Rangi hizi hupangiliwa kwa namna ambavyo rangi zinazotangulia upande wa kushoto ndizo za msingi zaidi kuliko zile za upande wa kulia.

Hivyo iwapo lugha itakuwa na rangi fulani upande wa kulia basi lugha hiyo itakuwa na rangi zote zilizotangulia. Mfano wake

1. Nyeupe nyeusi

2. Ukufu

3. Kijani njano

4. Samawati

5. Kahawia

6. Zambarau, kijivu, machungwa na kadhalika

Watoto hujifunza rangi kwa kufuata utaratibu huo na hapo watoto hujifunza rangi nyeupe na nyeusi haraka.

Hii inatokana na ukweli kwamba rangi hizi ziko tofauti na zingine na wala hazikaribiani.

Rangi za mwisho kujifunza kwa watoto ni zile zilizomo katika kikoa cha sita. Hii inatokana na ukweli kwamba ni vigumu sana kuzitofautisha rangi hizo na rangi zingine.

Ni mpaka watu wazima tu ndio wanaoweza kuzitofautisha zaidi.

Sifa za vikoa vya maana

Maneno yaliyo katika vikoa vya maana yana uhusiano unaokinzana hii inamaanisha kuwa yanahusiana na wakati huo huo yanatofautiana. Kwa mfano;
matunda, wanyama, samani.

Hivi ni vikoa. Kikoa kimoja kikubwa huweza kujumuisha vikoa vingine vidogo vidogo. Kwa ujumla maneno katika kikoa kimoja hayana mpangilio maalum.

Kwa mfano; hakuna mpangilio maalumu katika kikoa cha matunda, yaani unaweza kuanza na tunda lolote tu.

Hata hivyo kuna vigairi, kwa mfano namba 1,2,3,4…. , siku za wiki, miezi ya mwaka na kadhalika. Hizi zote zina mpangilio maalumu.

Ukivuruga mpangilio huu unaharibu.

Mahusiano ya kifahiwa

Haya ni yale mahusiano yaliyopo baina ya maneno yanayounda kikoa fulani cha maana. Kuna aina zake kama ifuatavyo:

Usinonimia (usawe),
Uantonimia (unyume),
Uhomonimia (neno moja maana tofauti zisizohusiana),
Upolisemia

USINONIMIA
Ni hala inayojitokeza au iliyopo pale ambapo maneno mawili au zaidi yenye maumbo tofauti na maana moja au maana inayokaribiana.

Maneno ambayo yanakaribiana au kuwa sawa huitwa sinonimia au visawe. Kwa mfano

i. Pesa, hela, fedha
ii. Shimo, tundu, tobo
iii. Mapenzi,mahaba, kupendwa
iv. Mjinga, bwege, mpumbavu, fala, pimbi
v. Ulimwengu, dunia

Aina za sinonimia
Kuna aina mbalimbali za sinonimia, lakini hatutajadili zote bali chache tu jinsi ifuatavyo:

1. Sinonimia ya Kimantiki (Logical Synonymy)
Sinonimia hizi hutokea pale ambapo mofimu mbili au zaidi huweza kubadilishana nafasi katika sentensi arifu zote pasipo kuathiri masharti ya ukweli. Kwa mfano:-
Harakaharaka-wanguwangu-upesiupesi
Kusudi-nia-lengo
Anuai-mbalimbali-tofauti tofauti

2. Sinonimia kuntu
Kwa mujibu wa Lyons (1977) anasema sinonimia kuntu hutokea pale ambapo leksimu mbili au zaidi kuweza kubadilishana nafasi katika miktadha yote bila athari yoyote kimaana. Hata hivyo wanaisimu wengi wanadai kwamba hadi sasa hakuna lugha yoyote duniani ambayo imethibitika kuwa na sinonimia kuntu.

Kwa mujibu wa mtaalam Al Ullumani (1994) anaeleza kuwa eneo moja ambalo linaweza kuwa na usinonimia kuntu. Ni eneo la usilabi. Kwa mfano:-

Nazali na ving‘ong‘o
Irabu na vokali
Jitihada na juhudi

Vyanzo vya Sinonimia
Kuna mambo mbalimbali yanayoweza kusababisha kutokea kwa sinonimia.
Baadhi ya mambo hayo ni:-

1. Ukopaji wa msamiati
Iwapo lugha itakopa maneno au msamiati kutoka kwenye lugha mbalimbali kuna uwezekano kuwa na maneno tofauti au mbalimbali yanayorejelea dhana moja.
Kwa mfano;

Shule-limetoka katika Kijerumani
Skuli-linatoka katika Kiingereza

Maneno haya yanaonekana kuwa ni sinonimia lakini sababu yake ni utohoaji wa maneno kutoka katika lugha nyingine.

MAREJEO
Habwe, J. na Karanja, P. (2004) Misingi ya sarufi ya Kiswahili, Phoenix Publishers Ltd. Nairobi-Kenya.

TUKI (2004) Kamusi ya Kiswahili Sanifu, Oxford University Press, Dar es Salaam.

Wasiliana na mwandishi kupitia anwani:marya.wangari@gmail.com