Fasihi na Falsafa ya Kiafrika

Na JENITHA WALTER

Imepakiwa - Wednesday, April 11  2018 at  15:38

Kwa Mukhtasari

Falsafa ni taaluma inayohusika na kutumia na kuchambua fikra, kuchunguza matumizi ya dhana, kupima vitendo, kutathimini ushahidi wa hoja zinazojengwa. Falsafa kama mtazamo ni namna mtu au jamii inavyouona na kuutafsiri ulimwengu, dhana na nadharia mbalimbali zinazohusu maisha.

 

FALSAFA ni taaluma inayohusika na kutumia na kuchambua fikra, kuchunguza matumizi ya dhana, kupima vitendo, kutathimini ushahidi wa hoja zinazojengwa. Falsafa kama mtazamo ni namna mtu au jamii inavyouona na kuutafsiri ulimwengu, dhana na nadharia mbalimbali zinazohusu maisha.

Kwa mujibu wa Mbiti mwaka 2011 anaeleza kuwa falsafa ya kiafrika inahusu uelewa, mantiki, mitazamo ya kiulimwengu na jinsi Waafrika wanavyofikiri, wanavyotenda na kuelezea fikra mbalimbali.

Fasihi na falsafa ni kitu kimoja, hazitengwanishwi, zimefungamana. Zote zinahusu maisha ya binadamu na jitihada za mwanadamu katika kuendeleza ulimwengu.

Placid Temples katika kitabu chake cha The Bantu Philosophy cha mwaka 1959 anaeleza kuwa tabia za Waafrika zinaongozwa na mantiki, nguvu hai katika darajia, wanahofu uhai na kifo, wanathamini vitu nyenye umbo la duara, wanaamini uchawi na ushirikina.

Riwaya ya KURWA na DOTO; maelezo ya wakazi katika kijiji cha Unguja, imeandikwa na Muhammad Saleh Farsy na kuchapishwa na Kenya Literature Bureau mwaka 1990. Riwaya hii inajaribu kugusia falsafa ya Kiafrika kama ilivyoelezwa na Temples.

1. (a) Uduara wa maisha

Uduara wa maisha unajitokeza ambapo maisha aliyoyapitia mama yake Kurwa anakuja kuyapitia mwanae, Kurwa kwa namna tofauti kidogo. Mama yake Kurwa alitakiwa kuolewa na ndugu mkubwa lakini hakuolewa naye badala yake mtoto aliyekuwa akilelewa nyumbani aliolewa na ndugu huyo. Kurwa naye alitakiwa kuolewa na Faki lakini kwaajili ya bashasha za Doto, Faki anaamua kumuoa Doto. Uduara wa maisha unathibitika baada ya mfumo wa maisha wa mzazi kujirudia kwa mtoto na kuendelea kizazi hata kizazi.

Alimwambia ya kuwa katika mipango iliyopangwa yeye alikuwa aolewe na ndugu mkubwa, na mtoto aliyekuwa akilelewa nyumbani kwao aolewe na ndugu mdogo … kwa kuwa alikuwa na pesa mkononi alimuoa yule binti aliyekuwa akilelewa nyumbani kwani yeye alikuwa kesha fungishwa hatuba ya huyo bwana uk 13.

(b) Uduara wa makazi

Mara nyingi kama siyo mara zote, mtu anapotoka kwao na kwenda sehemu nyingine kusalimia au kuanza maisha lazima arudi kwao kusalimia au kurudishwa akiwa maiti ili azikwe katika ardhi aliyozaliwa. Katika makazi uduara unathibitika ambapo ulipozaliwa na kuishi kwa muda, utarejea baada ya kufanya mizunguko ya maisha kwa kupenda au kutokupenda.

Baada ya sherehe, maharusi walikwenda kutembea nchi za nje ambako walikaa siku nyingi. Waliporudi matembezi walifikia kwa mama yao ambako walikaa siku chache uk 20.

Siku moja Kurwa na mama yake walipokuwa nyumbani, waliona milango inafunguliwa na Doto kuingia. Watu hao walifurai walipomuona Doto ambaye kwa miaka hajaonekana uk 33.

Miezi ilipokaribia Kurwa alitaka warudi kwao. Safari ilitengenezwa na habari zilipelekwa kuwa wanarudi na wanatumaini kufika siku fulani uk 51.

(c) Uduara wa majina

Watu wengi hupenda kuwarithisha watoto wao majina yao au majina ya wapendwa wao ili watakapokufa waishi kupitia majina hayo. Hivyo majina hayo huthibitisha uduara kwa kuwa hayapotei bali yanajirudia katika vizazi na vizazi.

Furaha zao zilizidi walipoona wamewaita watoto wao kwa majina yao kuwa ni ukumbusho uk 56.

Vumbwe baada ya kusitasita alimwita mtoto wao Kurwa kuwa ni ukumbusho wa Kurwa wake wa kadimi uk 56.

Kurwa akasema kwa ajili ya ukumbusho, napenda mmoja aitwe Doto kwa jina la mpenzi ndugu yake na wa pili aitwe Vumbwe kwa jina la mtu ambaye amemwokota, kwa mapenzi, kite na imani, alipokuwa yu mpweke uk 52.

Wengine hujenga majengo, kununua mashamba na viwanja na kuandika majina ya wapendwa wao kama ishara ya kuwakumbuka na kuthamini mchango wao katika maisha yao.

Pamoja na kusaidiwa na watu wengine, wakajenga madrasa kwa jina la Doto, kuwa ni sadaka na wakfu wake waliomwachilia duniani uk 40.

Nyumba na mashamba yake ya hapo aliyaandika wakfu kwa jina la Doto na akayaita Doto uk 42.

Kwa mtu ambaye hajabahatika kupata mtoto, atakapokufa atasahaulika mapema kwa kuwa hajaacha kumbukumbu yake. Jambo hili linathibitishwa na msanii kama ifuatavyo:

Masikini Doto! Katutoka kana kwamba hajakuwepo! Huo ndio mwisho wa mwanadamu; kufa na kusahaulika, kama hajaacha ukumbusho wa jina lake uk 38.

(d) Uduara wa uzazi

Uduara wa uzazi unathibitika pale ambapo mtoto anakua na uzazi na kuzaa kama yeye alivyozaliwa. Mara nyingi uduara wa uzazi unathibitika zaidi kwa vizazi pacha. Kwa waliozaliwa mapacha nao kuzaa pacha.

Kurwa alijifungua. Asili haikumwacha ila na yeye alizaa watoto wawili kama mama yake, lakini alizaa mke na mume uk 52.

(e) Uduara wa mapenzi

Wahenga walisema “Penzi la kweli halifi”, kauli hii au uduara huu hujitokeza pale ambapo waliokuwa wapezi kutengana kutokana na sababu mbalimbali na baadaye kurudiana na mapenzi kuchipua tena zaidi ya mwanzo.

Faki akijitahidi kumfurahisha na kumpoza. Kwa njia hiyo mapenzi yao ya asili yalianza kuchipua kidogokidogo, kwani yalitiliwa maji na kupaliliwa. Mapenzi hayo hayakufa bali yalisita na kudumaa, sasa yalianza kustawi tena uk 43.

2. Uzazi

Mimba ni chanzo cha uhai. Waafrika wanapenda na kuthamini sana watoto. Mwanamke mwenye uwezo wa kuzaa huthaminiwa na kupendwa sana katika ndoa tofauti na mwanamke ambaye hana uwezo wa kuzaa.

Baada ya miaka kupita, yule bibi akashika mimba. Haya yaliwafurahisha sana kwani hawajawahi kuroja kuzaa. Mimba ikalelewa kwa kila tunu na tamasha uk 1.

Mwanamke huyo alishika mimba. Sehemu ya Vumbwe iliyokuwa tumboni mwa mwanamke huyo ilikuwa mbegu ya kuanzisha mti wa mapenzi uk 55.

Usichana haukumdirikisha Kurwa kwani siku zilezile alionesha ishara ya kuchukua mimba. Kwa hakika mimba aliichukulia paziani. Faki akimletea cha tunu na cha tamasha, alichotamani na asichotamani uk 50.

3. Hofu ya kifo

Watu wengi huwa na hofu ya kifo. Kila siku asubuhi watu husalimiana na kutembeleana ili kujuliana hali. Wanapokuwa na mgonjwa, watu humtembelea na kumwombea dua ili apone kwa kuwa wana hofu ya kifo. Hakuna mtu anayependa kumpoteza mpendwa wake kwasababu ya kifo. Kuna vifo vingi vinavyosababishwa na uzazi, mjamzito apatapo uchungu wa kujifungua, ndugu, jamaa na marafiki humuomba Mungu ili mzazi ajifungue salama.

Uchungu ulipofika, wakunga waliitwa, na watu kujaa nyumba tele, wengine wakisoma Kuruani, wengine Maulid, wengine wakileta nyiradi, na wengine wakimsaidia mzazi kuugua. Bwana mwenye nyumba alikuwa kafadhaika na kubabaika, hajui, hajitambui kwa fikra na mawazo uk 2.

Kurwa alipokuwa na uchungu wa kugeuza, paliitwa waganga na waganguzi, mashehe na masharifu, wakunga na walimu; kumtazama na kumwombea Mungu amsalimu, salama uk 52.

4. Mapenzi na ndoa

Kwa tamaduni za Kiafrika, mwanamwali huchumbiwa, kutolewa posa na kuozwa. Mila, desturi na kanuni zinakataa wapenzi kuishi bila ya kufunga ndoa. Hivyo, wapenzi hupewa baraka na kufungishwa ndoa kabla ya kujuana kimwili.

Doto aliposwa. Mamaye na nduguye asione neno, kwani hayo ni madaraka ya mwanadamu hawezi kuyaepuka. Landikwalo ndilo liwalo mja hana hiari uk 19.
Siku ya pili Faki alikuja mwenyewe kuleta posa, naye alipokelewa kwa kichwa na miguu akawekwa ndani ya mboni za macho. Posa zilikubaliwa na harusi kubwa ikafanywa uk 19.

Ilisadifu kuwa huu ni mwezi wa mfungo sita; mwezi wa baraka na Maulidi. Kupata baraka za mwezi mtukufu, walitaka harusi ifanywe mwezi huohuo. Shauri ilikubaliwa. Palifanywa matengenezo machache na hotuba ikafungwa uk 49.

5. Uganga

Waganga huaminika na kutumiwa kuchunguza chanzo cha tatizo na kuponya wagonjwa.

Waganga waliitwa kumputia Kurwa. Kila mmoja alikuwa akila riziki yake … Mwali aliokotwa kwa ada na uganga ukesha uk 29.

Hali yake iliwahuzunisha na kuwatia wahka wote; uganga na uganguzi, kafala na mitishamba iliisha, na mapepo kushikwa sikio lakini Kurwa baada ya kupata hujambo akizidi kudhoofu uk 40.