Tahariri tarehe 1st Machi, 2019 Kila mmoja achukue tahadhari ugonjwa wa kimeta

Ngo'mbe mwenye ugonjwa wa kimeta 

Imepakiwa - Friday, March 1  2019 at  10:45

 

 Ugonjwa wa kimeta umelipuka katika baadhi ya maeneo nchini. Mpaka sasa takriban watu sita wameripotiwa kufariki dunia kwa kula nyama ya ng’ombe walioathirika na ugonjwa huo.

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, kimeta ni ugonjwa wa mlipuko utokanao na vimelea vya bakteria vinavyojulikana kitaalamu kwa jina la ‘bacillus anthracis’.

Ni ugonjwa unaowakumba wanyama na unaweza kuwaambukiza binadamu ama kwa kula na kunywa nyama na maziwa ya mnyama aliyeathirika au hata kumgusa.

Wanasema majimaji yanayotoka kwenye mzoga wa mnyama aliyeugua kimeta yanaweza kuhifadhi vimelea vya ugonjwa huo kwa miaka mingi. Kama hautotibiwa mapema, ugonjwa huo si tu unaweza kusababisha kifo kwa binadamu aliyeathirika, lakini anaweza kuwaambukiza wengine kwa kugusana ngozi.

Mtu anayeugua ugonjwa huo huwa na dalili kama vile kutokwa na damu maeneo mbalimbali ya mwili hasa yaliyo wazi. Dalili nyingine ni kuhara damu, kuhisi kichefuchefu na maumivu makali tumboni.

Sababu kubwa ya binadamu kuathirika na hadi kufa kwa kimeta ni kula nyama ya mnyama aliyeathirika na ugonjwa.

Hiki ndicho kilichotokea mkoani Songwe kwa watu wanne kufariki dunia huku wengine 81 wakiugua. Si Songwe pekee, watu wawili nao wakafariki mkoani Kilimanjaro kwa kula mzoga wa ng’ombe aliyekuwa na kimeta.

Tukubali baadhi yetu hatujali afya zetu, ndio maana hatuoni kama ni tatizo kula vibudu au wanyama waliochinjwa kiholela.

Urahisi wa gharama nao unatuponza. Kilichotokea Songwe ni kuwa watu hawakujiuliza mara mbilimbili iweje kilo moja ya nyama ambayo kwa kawaida huuzwa kwa bei ya Sh 4,000, iuzwe Sh500 tena pande kubwa.

Ni kweli tunaweza kudai ugumu wa maisha, lakini hakuna ugumu wa maisha mbele ya ulinzi wa uhai wa mtu. Na wala uchu wa nyama usiwe chanzo cha kugharimu maisha yetu. Tunapohanikiza Serikali na wadau wa afya kwa jumla kushupalia ugonjwa huu, tunaamini wajibu mkubwa wa kuepuka madhara ya kimeta upo kwa wananchi wenyewe. Kikubwa ni wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya kila kitu kinachoweza kuathiri afya zetu.

Tukitambua kuwa nyama ni kitoweo kikubwa na kinachopendwa na walio wengi, tunawasihi wananchi wenzetu kujenga tabia ya kula nyama zinazouzwa katika maeneo rasmi yanayotambulika kisheria kama vile mabucha sambamba na kupimwa na wataalamu wa mifugo.

Aidha, zipo baadhi ya mila zinazoruhusu watu kula mizoga ya wanyama waliokufa kwa kimeta kama kinga ya ugonjwa huo. Hatupaswi kukumbatia aina hii ya mila na ni lazima sote tuikemee kwa ustawi wa wananchi. Kwa Serikali hasa kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi, haina budi kuendelea na jitihada zake za kutoa chanjo dhidi ya ugonjwa huo.

Huu unapaswa kuwa wajibu mkubwa wa Serikali na vyombo vyake, huku ikiendelea pia kuhimiza utoaji wa elimu kwa umma.

Tunaamini Serikali ikitimiza wajibu wake nasi wananchi tukachukua tahadhari ya kuuthamini na kuulinda uhai wetu, ugonjwa huu unaweza kulipuka pasipo kuathiri wanyama wala binadamu.