Tahariri tarehe 28th February, 2019 Tumuenzi Ruge kwa kutambua fursa zilizopo

 

Imepakiwa - Thursday, February 28  2019 at  16:40

 

 Watanzania wako katika majonzi ya kuondokewa na Ruge Mutahaba, mtu aliyetoa maisha yake kuendeleza vijana na hasa kuwafundisha ujasiriamali. Aliwaondoa kwenye dhana iliyopitwa na wakati ya kutegemea kuajiriwa serikalini au kwenye kampuni binafsi.

Ruge ambaye amefariki dunia juzi nchini Afrika Kusini alikokuwa amelazwa kwa matibabu, taarifa ya kifo chake imeshtua wengi hasa kutokana na namna alivyokuwa mdau mkubwa wa burudani na ushiriki wake katika kuanzisha matamasha makubwa kama Fiesta, Summer Jam na kuunganisha wasanii katika kampeni mbalimbali za kijamii.

Pia, Ruge ameshiriki mikutano, semina na makongamano katika kuhamasisha vijana wafikiri tofauti, hakupenda wawe walalamishi bali siku zote aliwahimiza kutafuta suluhisho la matatizo yanayowakabili.

Kifo cha Ruge ni pigo kwa vijana hasa waliopita mikononi mwake, wengi wanamlilia hasa kwa kipaji chake cha kutambua fursa na kuzifanyia kazi.

Mara kadhaa alisikika kwenye mikutano akiwaeleza vijana umuhimu wa kuzungumza matatizo yao kama Watanzania, hakupenda tabia ya kumualika mtaalamu wa kigeni kuja nchini kutoa mada kuhusu suluhisho la matatizo yao.

Kuna wakati alionyesha kukerwa na tabia ya baadhi ya wanafunzi wa vyuo vikuu kulalamika kuhusu ajira. Kwake ilikuwa mhitimu wa chuo kikuu hatakiwi kuuliza njia kwani elimu aliyopita ilitosha kumuonyesha fursa ziliko.

Aliamini kwamba hata kama hukupata elimu ya juu, bado kijana anayejitambua anaweza kuzitafuta fursa ziliko kwa kufikiri tofauti.

Ruge sasa hayupo duniani, amefariki dunia, hivyo ni vizuri Watanzania hasa vijana wakamlilia kwa kuyafanya yale aliyokuwa akiyahimiza katika kumkomboa kijana kuondokana na umaskini.

Majonzi tunayoyaonyesha sasa kwa kuondokewa na Ruge tuyatafsiri kwa vitendo. Watu waanze kufikiri tofauti kwa kujitoa kushiriki shughuli za maendeleo badala ya kusubiri kila kitu kifanywe na Serikali.

Vijana wanaomlilia sasa, majonzi yao wayaelekeze katika kutafuta fursa, wafundishane ujasiriamali na waache tabia ya kulalamika pasipo sababu za msingi.

Taifa hivi sasa lina vijana wengi wasomi ambao hawana ajira na watambue kwamba kuendelea kusubiri ajira ni kupoteza muda, hivyo jambo la muhimu kwao ni kufikiri tofauti kwa kuzitafuta fursa ziliko.

Serikali ya awamu ya tano imejielekeza katika uchumi wa viwanda, vijana wenye elimu ya juu na wale wenye kiwango cha kawaida cha elimu waitumie fursa hiyo kujitafutia chanzo cha mapato.

Pia, Tanzania ni mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na jumuiya zingine za kimataifa, huko kuna fursa ambazo zinaweza kutumiwa na vijana wa Kitanzania kujiongezea kipato.

Ujumbe wa Ruge wa kufikiri tofauti umewagusa pia hata waliomo kwenye ajira, kwani bila kuwa mbunifu na mwenye kujituma kwa mwajiri wako, afya ya kiuchumi ya kampuni au shirika haitakuwa madhubuti.

Ni muhimu kwa waajiriwa kutambua kwamba mshahara wanaoupata mwisho wa mwezi ni matokeo ya utendaji wao wa kazi.

Hivyo, wakati tukiendelea kumlilia Ruge tufanye hivyo kwa kuongeza juhudi katika utendaji wa kazi. Pia wasio na ajira watambue kwamba kuna fursa nyingi za kiuchumi zinawasubiri wao kuchangamsha bongo zao.