http://www.swahilihub.com/image/view/-/4564686/medRes/1974895/-/15lu1tf/-/New+Document.png

 

Aga Khan yaanzisha mfumo mpya wa kuhifadhi picha za mionzi

Mkurugenzi Msaidizi huduma za uchunguzi wa Magonjwa kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dk Charles Massambu (kushoto) akipokea tuzo kutoka kwa ofisa Mwendeshaji Mkuu wa Taasisi ya Huduma za Afya ya Aga Khan nchini, Sisawo Konteh jijini Dar es Salaam jana kwa kutambua mchango wake baada ya kuzindua mfumo wa utunzaji wa picha za Radiolojia (X-Rays) na mawasiliano (Pacs). Katikati ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Aga Khan, Hussein Kidanto. Picha na Venance Nestory  

Na Ephrahim Bahemu

Imepakiwa - Wednesday, May 16  2018 at  13:26

Kwa Muhtasari

Hospitali ya Aga Khan imezindua mfumo wa kuhifadhi picha na mawasiliano (pacs) pamoja na mfumo wa taarifa za radiolojia (ris), ikiwa ni mkakati wa kuboresha huduma za mionzi kwa ajili ya matibabu.

 

Dar es Salaam. Hospitali ya Aga Khan imezindua mfumo wa kuhifadhi picha na mawasiliano (pacs) pamoja na mfumo wa taarifa za radiolojia (ris), ikiwa ni mkakati wa kuboresha huduma za mionzi kwa ajili ya matibabu.

Akizungumza katika uzinduzi wa mfumo huo jana, mkurugenzi wa Tiba katika hospitali hiyo, Ahmad Jusabani alisema ulianza kujaribiwa mwezi Machi na matokeo yameonyesha utasaidia kurahisisha utoaji wa huduma bora kwa wagonjwa.

Alisema mfumo huo wa kielektroniki una uwezo wa kulinganisha picha ya zamani na ya sasa, hivyo kumrahisishia daktari kujua maendeleo ya mgonjwa.

Kupitia mfumo huo, mionzi ya mgonjwa itaambatanishwa na taarifa zake, itamuonyesha daktari wingi wa watu wanaosubiri huduma na kupunguza muda wa kumhudumia mgonjwa mmoja na kwamba, wagonjwa wengi watahudumiwa kwa wakati mmoja na gharama za huduma zitapungua.

“Sasa mchakato wa picha ya mionzi hatuhitaji tena watu wengi wala kemikali za kusafishia picha, filamu, eneo la kutunzia kumbukumbu za picha na vifaa vya ‘kuprinti’. Eneo ambapo vifaa hivyo hukaa sasa tutaweza kulitumia kwa shughuli nyingine kwa kuwa kompyuta haichukui nafasi kubwa,” alisema Jusabani.

Alisema changamoto kubwa katika mfumo huo ni uwepo wa mtandao wa intaneti wa uhakika kwa kuwa vituo vyao vyote vimeunganishwa katika mfumo mmoja ili kutoa fursa kwa madaktari kujadili kuhusu matibabu.

Mkuu wa operesheni kutoka hospitali hiyo, Sisawo Konteh alisema mfumo huo sio kwa ajili ya wagonjwa wanaotibiwa Aga Khan pekee, bali Watanzania wote.

“Tunaifanya Aga Khan kuwa hospitali ya kisasa zaidi na kutoa huduma za ubora. Ukiachilia mbali Afrika Kusini, Aga Khan (Tanzania) ndiyo yenye mfumo huu wa kisasa unaogharimu mamilioni ya fedha,” alisema Konteh.

Mgeni rasmi katika uzinduzi huo, mkurugenzi msaidizi wa Huduma za Uchunguzi wa Magonjwa kutoka Wizara ya Afya, Dk Charles Massambu alisema Serikali inatambua umuhimu wa huduma bora zinazotolewa na hospitali hiyo ndiyo maana imekuwa ikipata ithibati za kimataifa, hivyo wanapaswa kuongeza bidi.

“Lakini niwape changamoto moja, ubunifu mnaoufanya na ithibati mnazozipata isiwe kigezo cha kuzifanya gharama zenu kuwa ghali. Hospitali za umma na nyingine za binafsi zitatumia mfumo huu mpya kwa njia ya kutoa rufaa kwa wagonjwa,” alisema Massambu.

Alisema kitendo cha kupata ithibati kimataifa inamaanisha kuwa huduma inayopatikana Aga Khan Tanzania ni kama inayopatikana India, Marekani na Serikali ipo kwenye mkakati wa kuhakikisha hospitali zake zinatoa huduma za kisasa.