Rais Magufuli amaliza sakata la mafuta ya uto

Rais  John  Magufuli, akigawa mapapai na ndizi kwa wananchi nje ya eneo lenye matanki ya kuhifadhia mafuta ya kula baada ya kushushwa melini alipofanya ziara ya ghafla kwa ajili ya kukagua uingizwaji, ugawaji na ulipiaji wa ushuru   kwenye Bandari ya Dar es salaam jana. Picha na Ikulu  

Imepakiwa - Wednesday, May 16  2018 at  14:51

Kwa Muhtasari

Sakata la uhaba wa mafuta ya kula nchini lililodumu kwa takriban siku 10 limemalizwa na Rais John Magufuli baada ya kuagiza kampuni tatu za mafuta kulipia ushuru wa matanki 43 ya bidhaa hiyo

 

Dar es Salaam. Sakata la uhaba wa mafuta ya kula nchini lililodumu kwa takriban siku 10 limemalizwa na Rais John Magufuli baada ya kuagiza kampuni tatu za mafuta kulipia ushuru wa matanki 43 ya bidhaa hiyo yaliyokuwa yamekwama katika Bandari ya Dar es Salaam na kutoa agizo la kufanyika haraka kwa marekebisho ya sheria juu ya uingizaji wa mafuta ghafi.

Jana, Rais Magufuli alifanya ziara ya kushtukiza bandarini hapo ambako alikagua matenki ya mafuta na kupokea ripoti ya uchunguzi uliofanywa na taasisi za Serikali ambayo imebainisha kuwa matanki 36 yana mafuta ghafi, safi kiasi (yaliyoboreshwa kiasi) na malighafi za kutengenezea sabuni na kuagiza kampuni hizo zilipie asilimia 10 ya ushuru kwa mujibu wa sheria, lakini matenki mengine saba yalibainika kuwa na mafuta safi hivyo kuagiza yalipie ushuru wa asilimia 25 na kwa kwa waliodanganya kuwa na mafuta ghafi wakati ni safi watozwe faini.

Kuhusu sheria, amemtaka Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage kupeleka bungeni marekebisho ya Sheria ya Kodi ili mafuta ghafi yanayoingia nchini yatozwe kodi kubwa kwa ajili ya kulinda wafanyabiashara na viwanda vya ndani.

Kumekuwa na mvutano mkubwa wa ushuru baada ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuzuia tani 62,000 za mafuta hayo katika bandari hiyo kwa madai kwamba ni safi kwa matumizi na hivyo kutaka yalipiwe asilimia 25 huku Shirika la Viwango Tanzania (TBS) likisema ni mafuta ghafi na hivyo kustahili kulipiwa asilimia 10.

Mvutano huo ambao ulielezwa kusababisha kupanda kwa bei ya mafuta uliibuka bungeni mwanzoni mwa wiki iliyopita baada ya wabunge kuhoji na kuitaka Serikali kutoa majibu, ikiwamo kuzuiwa kwa meli zenye shehena hiyo bandarini katika sakata hilo, Waziri Mwijage alibanwa na wabunge na majibu yake hayakumridhisha Spika Job Ndugai ambaye aliitaka Serikali kutoa majibu ya uhakika.

Mei 9, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza bungeni alitoa siku tatu kwa wafanyabiashara na wenye viwanda kutoa mafuta hayo ghalani na kuyaingiza sokoni huku Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro akisema kuwa amewaagiza makamanda wa polisi nchini kujiandaa kutekeleza operesheni hiyo.

Matanki saba

Rais Magufuli baada ya kuwasili bandarini hapo, alianza kusikiliza maelezo ya ukaguzi wa matanki hayo uliofanywa na maofisa kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, TBS na TRA wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Profesa Joseph Buchweishaija.

“Tatizo tulilonalo katika mafuta yetu, mafuta ghafi yanachajiwa asilimia 10, mafuta yaliyosafishwa yanachajiwa asilimia 10 na yale yaliyo tayari kwa matumizi yanachajiwa asilimia 25. Wanachokifanya wafanyabiashara wetu ni kuchanganya mafuta yote wanaweka kwenye debe na kuwauzia watu,” alisema Rais.

Alisema katika uchunguzi uliofanywa na taasisi hizo katika kituo cha Vegetable Oil Terminal (VOT) katika matanki 13, mawili kati ya hayo yalikutwa mafuta safi.

“Matanki haya mawili wanapaswa kulipa ushuru wa asilimia 25. Pia walibaini matenki manne yana malighafi za kutengenezea sabuni na wanapaswa kulipia asilimia 10,” alisema.

Alisema kwenye kituo cha Tanzania Liquid Storage, tanki namba tatu lilibainika kuwa na mafuta safi na kutakiwa kulipiwa asilimia 25 ya ushuru.

“Kuna mafuta ya East Coast Oil and Fats Limited, hapa imegundulika mafuta yote yanachajiwa asilimia 10, ila kuna matanki manne ya ECB1, ECB2,ECB9 na ECC3 yale yana mafuta safi na yatalipiwa ushuru wa asilimia 25,” alisema.

Alisema kampuni zilizodanganya kuwa na mafuta ghafi, kubainika ni mafuta safi, zinatakiwa kutozwa faini baada ya kulipa ushuru.

Kubadili sheria

Kuhusu sheria ya kodi alimtaka Waziri Mwijage apeleke mabadiliko ya sheria bungeni ili kuondoa mianya ya ukwepaji wa kodi kwa waagizaji wanaodai mafuta ni ghafi wakati si kweli kwa lengo la kukwepa kulipa kodi halali za Serikali

“Haiwezekani uende Ulaya ukanunue mafuta ghafi. Hakuna mfanyabiashara wa namna hiyo anayeweza kununua mafuta ghafi na kuja nchini kuyabadili kuwa mafuta safi.”

Alisema sheria hiyo ni ya ovyo kwa mafuta ghafi kutozwa ushuru wa asilimia 10.

“Tulifanya makosa kama Serikali. Indonesea na Malaysia ukinunua mafuta ghafi chaji yake ni kubwa mno.”

Kuhusu kuadimika kwa biadhaa hiyo muhimu Rais Magufuli alisema, “Nataka niwahakikishie Watanzania wote na ndugu zangu Waislamu mnaoanza Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, hakutakuwa na upungufu wa mafuta, na wanaofanya mchezo wa kutishia kuadimika kwa mafuta ili waachiwe kuingiza mafuta kwa kukwepa kodi hawataweza, nataka niwahakikishie Serikali ipo makini.”

Pia alisema, “Hatuwezi kuwa tunaibiwa kila siku, tunahitaji kujenga viwanda vyetu… lakini Kwa sababu sisi ni watu wa kuibiwa tulipitisha sheria hii tangu mwaka 2015 na inawezekana ulifanyika mchezo, wabunge walipitisha kitu kingine na kilichokuja kusainiwa kikawa kitu kingine maana kulikuwa na mchezo huo kwenye ofisi ya AG (Mwanasheria Mkuu wa Serikali).”

Alisema wakati huo kulikuwa na mchezo wabunge wakipitisha sheria inafanyiwa mabadiliko na kuwa tofauti na iliyopitishwa na Bunge.

Ofisa TRA aula

Rais Magufuli ambaye alipongeza taasisi zilizofanya uchunguzi huo aliagiza Kaimu Kamishna wa mamlaka hiyo, Ben Usaje Asubisye kupandishwa cheo.

“Wewe unafanya kazi gani (Asubisye),” aliuliza Rais Magufuli na kujibuwa na ofisa huyo, “mimi ni kaimu kamishna,” kisha Rais akasema, “Waziri wa Fedha (Dk Philip Mpango) mpeni huyu maana amesimamia mambo kwa masilahi ya nchi. Katibu mkuu kazungumzeni na mumpe haraka wiki hii. Amesimamia haki yake na haki ya Watanzania kwa niaba ya Watanzania.”

Rais pia alitaka ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kufanya kazi kwa weledi, kama wanachunguza mkono wa mlemavu wa ngozi au dawa za kulevya, majibu yawe halisi na wanachokipima.