Serikali yafuta mtihani wa kidato cha pili Zanzibar

Na MWANDISHI WETU

Imepakiwa - Friday, December 7  2018 at  13:32

Kwa Muhtasari

Necta inasema shule zilifutiwa matokeo baada ya kubainika kufanya udanganyifu kwa kuvujisha mitihani.

 

HATUA ya hivi karibuni ya Serikali ya Zanzibar kufuta mtihani wa kidato cha pili uliokuwa ukiendelea visiwano humo, imeshangaza wengi.

Mshangao uliopo sio tu Zanzibar haina historia ya matukio hayo kwa kiwango cha kufutwa kwa mitihani, lakini ni hivi karibuni tukio kama hilo lilitokea Tanzania Bara. Lakini hatukujifunza.

Oktoba 2018 Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) lilifuta matokeo ya mtihani wa darasa la saba kwa shule zote za Halmashauri ya Wilaya ya Chemba, pamoja na baadhi ya shule katika wilaya za Kondoa, Kinondoni, Ubungo na Halmashauri ya Jiji la Mwanza.

Kwa mujibu wa Necta, shule hizo zilifutiwa matokeo baada ya kubainika kufanya udanganyifu kwa kuvujisha mitihani.

Wapo walioathirika kwa mtihani huo kurudiwa kama wanafunzi, walimu na wazazi. Lakini fauka ya yote ni gharama iliyotumika kurudia mtihani huo ambao, hata hivyo, haikuwahi kuwekwa bayana.

Kwa upande wa Zanzibar, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Riziki Pembe Juma alisema gharama zilizotumika kuandaa mtihani huo ni TSh250 milioni.

Hiki si kiasi kidogo; ni kiasi kinachoweza kutumika katika mambo kadhaa ya msingi kwa maendeleo ya elimu au ya nchi kwa jumla.

Ifike hatua sasa suala hili lifikie kikomo, kwani tunaamini mamlaka husika kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola vina weza kubaini mwanya wowote unaoweza kutumiwa kufanya udanganyifu.

Mwanya huu unaweza kuwapo katika kila hatua ya mchakato mzima kuanzia utungaji wa mitihani, usafirishaji, uhifadhi na usimamizi ndani ya chumba cha mtihani na hata kwenye usahihishaji.

Ni muhimu kufanyia kazi sababu zinazochangia vitendo vya udanganyifu. Kwa mfano, tunapowatishia walimu wakuu na walimu wakuu kuwa wataondolewa katika nafasi zao ikiwa shule zao zitefeli, tunatarajia nini kama sio kujenga mazingira ya ufaulu kutafutwa kwa udi na uvumba ikiwamo kutumia njia za mkato kama kuifanya udanganyifu?

Ni kweli tunahitaji shule zetu kufanya vizuri ili mwishowe tujinasibu na ufaulu mkubwa majukwaani kama mojawapo ya mafanikio ya kielimu, lakini ufaulu huo usiwe wa kulazimisha. Tuache taratibu za kitaaluma zifuate mkondo wake ili hatimaye walimu na wanafunzi wavune walichokipanda.

Tiba

Tunaamini Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako anayo tiba ya kuzuia vitendo hivi.

Sio tu aliwahi kutoa ushauri wa wahusika kuchukuliwa adhabu kali ikiwamo kufungwa magerezani, wakati alipokuwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), lakini udanganyifu kwenye mitihani ni suala ambalo kama mwanataaluma ameshawahi kulifanyia utafiti na hata kulitolea andiko.

Tunapotaka maendeleo ya viwanda au kuwa nchi ya uchumi wa kati kama inavyotamka Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025, hatuna budi kuwa na wananchi wenye elimu bora na sahihi, wenye stadi zinazoendana na dhamira tunayokusudia.

Dhamira hii kamwe haiwezi kufikiwa kama tutaendelea kuwa na nguvu kazi yenye kasoro kubwa ya kiujuzi na kimaarifa kwa sababu ya kuhitimu kwa njia za udanganyifu.