http://www.swahilihub.com/image/view/-/5071980/medRes/2313155/-/121ibr4/-/act+pic.jpg

 

ACT- Wazalendo wachimbua yao ripoti ya CAG

Na Fidelis Butahe, Mwananchi fbutahe@mwananchi.co.tz

Imepakiwa - Monday, April 15  2019 at  09:02

 

Dodoma. Chama cha ACT- Wazalendo jana kilibainisha kasoro kadhaa katika makusanyo na udhibiti wa fedha za umma, kikiungana na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kutaka kuundwa kwa mifumo thabiti ya usuluhishi wa fedha kutoka maeneo tofauti.

Chama hicho, pia kimetaka Serikali iwasilishe bungeni majibu ya kasoro kadhaa zilizobainishwa katika ripoti ya CAG kwa mwaka 2017/18 iliyowasilishwa bungeni katikati ya wiki iliyopita.

Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe aliwaambia waandishi wa habari mjini Dodoma jana kuwa mchanganuo wa chama hicho katika ripoti ya CAG umebainisha kasoro kadhaa, huku kikitoa tuhuma kadhaa dhidi ya matumizi ya fedha bila ya kupitia mfuko mkuu wa Serikali.

Ripoti hiyo, mbali na kuonyesha asilimia 97 ya taasisi zimepata hati safi, bado ufisadi, ukiukwaji wa taratibu za fedha na utendaji mbovu, umetamalaki.

“Katika ukaguzi wa CAG wa bajeti ya mwaka 2017/18 ameonyesha katika bajeti ya Sh31.7 trilioni iliyoidhinishwa na Bunge, Serikali iliweza kukusanya Sh27.7 trilioni tu kutoka kwenye vyanzo vyote vya kodi, vyanzo visivyo vya kodi, mikopo ya ndani na nje, na misaada ya wahisani na washirika wa maendeleo,” alisema.

“Serikali ilishindwa kukusanya Sh4 trilioni kama ilivyokuwa mwaka uliopita ingawa sasa ni sawa na asilimia 13 ya Bajeti yote ya mwaka 2016/17. Hata hivyo CAG anaonyesha kuwa Sh26.9 trilioni tu ndio zilitolewa kutoka mfuko mkuu wa Serikali na kwenda kutumika.

“Hivyo Sh800 bilioni kati ya Sh27.7 trilioni zilizokusanywa kutokujulikana ziliko.”

Zitto pia alinukuu ukurasa wa 91 wa ripoti ya CAG kwamba ‘ikilinganishwa taarifa ya kutoa fedha (exchequer issue report) na taarifa ya fedha zilizopokelewa na kuripotiwa katika taarifa za fedha za mafungu husika pamoja na barua za kukiri mapokezi ya fedha kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, imebaini tofauti ya taarifa zilizoripotiwa”.

Zitto alisema CAG alieleza kuwa tofauti hiyo imesababishwa na kutokuwepo kwa mifumo thabiti ya usuluhishi kati ya fedha zilizotolewa na Hazina na fedha zilizotolewa na wahisani wa maendeleo moja kwa moja kwenye miradi ya maendeleo katika wizara.

Alidai kuwa kuna fedha ambazo makusanyo yake hayakuingizwa mfuko mkuu wa Serikali.

“Suala la udhaifu wa mifumo Hazina pia limeelezwa kwa kina katika taarifa ya CAG ya uhakiki wa tofauti ya Sh1.5trilioni mwaka wa Fedha 2016/17, bado udhaifu huu unaendelea,” alisema Zitto.

Alisema ripoti hiyo pia inaeleza kuwa Sh678bilioni hazikupelekwa katika taasisi zilizokusanya.

“Kwa mwaka 2017/18, CAG amebaini Sh678 bilioni zilizokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa niaba ya taasisi nyingine hazikuhamishwa kwenda taasisi husika, na badala yake zilihamishiwa kwa Katibu Mkuu Hazina ambapo huko hazikuonekana kwenye ukaguzi kama sheria inavyotaka.”

Alisema fedha hizo ni Sh169 bilioni za Shirika la Reli (TRC), Sh 168bilioni za wadau wa korosho nchini na Sh6bilioni za Wakala wa Umeme Vijijini (Rea).

“Kwa mara nyingine, CAG amependekeza sheria iheshimiwe kuhusu matumizi ya fedha hizi za taasisi mbalimbali,” alisema Zitto.

Alisema jambo jingine ni CAG kueleza kuwa asilimia 40 ya bajeti kutegemea misaada na mikopo.

“Hii ni tofauti na tunavyoelezwa na Serikali kila wakati kuwa nchi yetu inaondoa utegemezi kwenye bajeti. Kwa mwaka 2016/17 utegemezi wetu uliongezeka kwa asilimia 27 na kwa mwaka 2017/18 utegemezi wetu umeongozeka kwa asilimia 22,” alisema Zitto.

Ripoti hizo zitafanyiwa kazi na kamati za Bunge za Hesabu za Serikali (PAC) na ile inayohusu serikali za mitaa ya LAAC.