http://www.swahilihub.com/image/view/-/4842624/medRes/2164324/-/m7lwwiz/-/zainaba.jpg

 

DC wa Pangani sasa ahamia vijijini

Zainab Abdallah

Mkuu wa Wilaya ya Pangani mkoani Tanga, Zainab Abdallah. Picha/MAKTABA 

Na GEORGE NJOGOPA, Mwananchi

Imepakiwa - Thursday, November 8  2018 at  14:21

Kwa Muhtasari

Mkuu wa Wilaya ya Pangani mkoani Tanga, Zainab Abdallah anasema anazungukia vijiji vyote vya wilaya yake akilala huko ili kubaini kero za wananchi na kuzitatua.

 

DAR ES SALAAM, Tanzania

MKUU wa Wilaya ya Pangani mkoani Tanga, Zainab Abdallah amesema amelazimika kuzungukia vijiji vyote vya wilaya yake akilala huko ili kubaini kero za wananchi na kuzitatua.

Alisema ziara yake hiyo ilimsaidia kubaini mengi ikiwamo kujionea namna baadhi ya miradi iliyokuwa ikitekelezwa kwa fedha za Serikali ilivyokosa usimamizi makini.

“Mfano nilipofika Pangani nilikuta mradi mmoja wa ujenzi wa majengo ya sekondari unaogharimu Sh400 milioni lakini nikakuta jengo lake limepasuka nyufa na wataalamu wako pale wanalipwa kwa kufanya kazi hiyo na hakuna hatua zozote wanachukua. Tukaamua kuchukua hatua maana wakati mwingine unaweza ukalazimika kumweka mtu ndani ili iwe fundisho kwa wengine kwa sababu tu wale wanaopewa dhamana katika mambo fulani hawajibiki ipasavyo.”

Alisema yeye na timu yake wamelazimika kuacha mfumo wa zamani wa kufanya kazi kwa mazoea kama ilivyokuwa kwa watangulizi wake waliokuwa wakishinda ofisini bila kuzingatia mahitaji halisi ya wananchi.

“Sisi ni viongozi vijana na tumeamua kutoka ofisini kwenda kuwashirikisha wananchi. Tumeanzisha kampeni yenye lengo la kuwawezesha vijana na awamu ya kwanza tunawatambua kwa kuwaandikisha,” alisema.

Alisema baada ya kuwaandikisha watatambua mahitaji yao na awamu ya mwisho itakuwa kuwajengea uwezo. “Nimewaambia ifikapo mwakani sitaki kuona kijana akiwa kijiweni.”

Vijana ni asilimia 55

Alisema wilaya hiyo inayokadiriwa kuwa na wakazi 60,000, asilimia 55 wakiwa vijana, inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwamo barabara na masoko ya uhakika ya mazao ambazo alisema zitakuwa historia baada ya serikali kudhamiria kujenga barabara kwa kiwango cha lami kutoka Tanga kwenda Pangani na Wizara ya Mifugo na Uvuvi ipo mbioni kujenga soko la kisasa la mazao ya bahari.

“Soko kubwa la kisasa litajengwa katika eneo la dagaa Kipumbwe ambalo litakuwa la aina yake katika eneo la Afrika Mashariki. Kwa maana hiyo wananchi wa eneo hilo watakuwa na fursa kubwa ya kuuza bidhaa zao,” alisema Zainab ambaye ni DC mwenye umri mdogo kuliko wote walioteuliwa katika utawala wa Awamu ya Tano.

Ingawa hakuwa tayari kubainisha umri wake, lakini alisema katika uteuzi wa wakuu wa wilaya uliofanywa mwaka 2016, yeye ndiye mwenye umri mdogo zaidi.

“Ni kweli kabisa mimi ndiye DC mwenye umri mdogo kabisa katika wakuu wa wilaya wote nchini,” alisema