http://www.swahilihub.com/image/view/-/4737690/medRes/2095643/-/134k6d2/-/kesia.jpg

 

Dkt Shein ajadiliana na mabalozi wa nchi tatu

Ali Mohamed Shein

Rais wa Zanzibar, Dkt Ali Mohamed Shein. Picha/MAKTABA 

Na HAJI MTUMWA, Mwananchi

Imepakiwa - Wednesday, January 30  2019 at  12:22

Kwa Muhtasari

Rais wa Zanzibar Dkt Ali Mohamed Shein amejadiliana na mabalozi wa nchi tatu za Kuwait, Ethiopia na Misri; yakijikita katika masuala ya uchumi, uwekezaji na kuimarisha uhusiano.

 

UNGUJA

RAIS wa Zanzibar Dkt Ali Mohamed Shein amefanya mazungumzo na mabalozi wa nchi tatu za Kuwait, Ethiopia na Misri yaliyojikita zaidi katika masuala ya uchumi, uwekezaji na kuimarisha uhusiano.

Mazungumzo hayo yalifanyika kwa nyakati tofauti Ikulu mjini Zanzibar juzi, ambapo mabalozi hao walifika kwa ajili ya kujitambulisha kwa Dkt Shein.

Mabalozi hao ni Mubarak Mohammed wa Kuwait, Yonas Yosef wa Ethiopia na Gaber Mohamed wa Misri.

Mabalozi hao walipongeza mafanikio yaliyofikiwa na Zanzibar na kuahidi kuendelea kuyaunga mkono, huku wakitumia fursa hiyo kutoa pongezi maalumu kwa Dkt Shein pamoja na wananchi wa Zanzibar kwa kuadhimisha miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964.

Akizungumza na Balozi Mohammed wa Kuwait, Dk Shein alisema Kuwait imekuwa ikisaidia kuimarisha sekta za maendeleo ikiwemo afya, elimu, kilimo na nyingine na kutoa wito kwa wawekezaji wa nchi hiyo kuwekeza Zanzibar.

Naye Balozi Mohammed alieleza azma ya nchi yake kuendelea kusaidia sekta za afya, elimu na kilimo.

Kwa upande wake, Balozi Yosef wa Ethiopia alimueleza Dkt Shein mafanikio yaliofikiwa na nchi yake kiuchumi, kisiasa na kijamii ikiwa pamoja na kukua kwa shirika la ndege la nchi hiyo (Ethiopia Airlines) na kurejea uhusiano kati ya nchi hiyo Eritrea.

Kufungua ubalozi mdogo

Dkt Shein alitoa wito kwa nchi hiyo kufungua ubalozi mdogo Zanzibar ili kuimarisha zaidi uhusiano wa pande hizo mbili.

Balozi wa Misri alimueleza Dkt Shein kuwa nchi yake itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika sekta za maendeleo ikiwamo kilimo, mafunzo na uwezeshaji wa programu mbalimbali kupitia sekta hiyo.