http://www.swahilihub.com/image/view/-/5118014/medRes/2345399/-/8n12kl/-/fedha+pic.jpg

 

Fedha, uhalifu Dampo la Pugu Kinyamwezi

Na  Mwandishi Wetu, Mwananchi

Imepakiwa - Thursday, May 16  2019 at  13:09

 

Dampo la Pugu ni eneo maarufu jijini Dar es Salaam kwa kukusanya taka zote zinazozalishwa na wakazi wa jiji hilo.

Eneo hilo pia lina sifa ya kuogopwa na watu kutokana na sifa yake mbaya ya uhalifu kama kuwapo kwa wavuta bangi na vibaka.

Ziara ya dampo

Ni saa nne asubuhi, nafika eneo hilo baada ya kutahadharishwa sana na baadhi ya watu kuwa mahala hapo sio salama hasa kwa mtoto wa kike kama mimi.

Nafika kushuhudia shughuli zinazofanyika eneo hili ambalo wenyeji ama wenye dampo huliita ‘Mgodi wa dhahabu’.

Mazingira ya nje ya dampo ikiwamo barabara ya lami inayoingia katikati ya dampo hilo inatoa taswira ya awali kwa mwandishi wetu kuwa dampo hilo si dampo la Taka bali ni dampo lililojaa dhahabu (pesa) lakini iliyokaliwa na vibaka, matapeli, wezi, majambazi na wahalifu wa kila aina licha ya uwapo wa raia wema wachache.

Ukiwa hapo ukionacho ni magari yanayoingia na kutoka yakitimua vumbi lililoishia kuwavamia watu walioko pembezoni mwa barabara inayoelekea ndani ya dampo wakiwamo wafanyabiashara na mama lishe.

Vijana maarufu kwa jina la ‘Mazombi wa Dampo’ (mateja) wanapita huku na kule, wapo wengine waliochafuka kupitiliza wakiwa wamebeba mafurushi ya taka yaliyofungwa kwenye mashuka na viroba.

Huku wakiwa peku na bila kuvaa kinga yoyote katika mwili wao,walibeba taka hizo ambazo zilichuruzika uji wa uozo na inzi walionekana wakinyemelea taka hizo kutokana na harufu kali iliyokuwa ikitoka.

Vijana wengine walisimama pembezoni mwa barabara inayoelekea dampo wakivizia magari yanayoingia na kuyadandia, huku kila mmoja akiwahi bahati yake ya kujichukulia taka zilizobebwa katika magari hayo.

Mbali na vijana hao wapo wachuuzi wa bidhaa mbalimbali kama vyakula na vinywaji.

Katikati ya dampo

Mateso ni miongoni mwa watu wanaofanya biashara ya magendo ndani ya dampo hilo, anaongozana nami kunionyesha shughuli mbalimbali zinazofanyika katika eneo hilo lenye milima ya taka. Cha kustaajibisha ni kuwa wakati kwa walio wengi taka ni karaha, hapa watu wanakula bila kujali taka wala uozo wake.

“Unaona humu dampo kama nilivyokueleza kuna kila aina ya biashara,huyo mama tuliyemuona na makundi ya vijana tulioyapita anauza bangi na madawa ya kulevya,kuna kundi tumelipita pale juu(anaonyesha) lile kundi kama umeona kuna makreti ya bia pale wanauza pombe”anasema Mateso.

Dampo hili ni fedha

Jibwa ni miongoni mwa kundi la vijana wanaojulikana kama wababe wa dampo,huyu ndiye anayesimamia waokota taka wote na shughuli mbalimbali za dampo .

“Ukiwa na kilo moja ya chupa za maji kabla hazijapelekwa kiwandani huuzwa Sh 150 hadi Sh200, plastiki kwa maana ya beseni,ndoo,majaba huuzwa Sh600 hadi Sh750 bei ya jumla ,“anasema.

Anaongeza: “Ukiona umeshindwa na kazi yoyote hapa mjini, kimbilia dampo la Pugu Kinyamwezi”.

Jibwa anasema kama Serikali ingejua namna dampo linavyonufaisha watu, ingeweka usimamizi makini.

“Umeona hizo taka zinazokusanywa? Licha ya watu kuzidharau, hao kina mama na vijana wanaopakia taka na wengine wamekaa wana fedha hata kuzidi mtu anayefanya kazi ofisini,’’ anafafanua Jibwa.

Issa Mohamed ni mmoja wa waokota taka ndani ya dampo anasema taka zina faida ikiwa utaamua kujikita kwenye biashara hiyo.

“Huku unaweza kufanya biashara ya kuuza neti na mashuka yaliyotupwa kama taka,”alisema na kudai neti na shuka mbovu uuzwa kati ya sh300 hadi Sh500

 

 

Wanawake na biashara haramu

Si ajabu kukutana na mwanamke akiwa amezungukwa na kundi la vijana wa kiume kwenye vibanda vilivyojengwa kwa matambala katikati ya Dampo la kinyamwezi.

Wenyeji wanaviita vibanda hivyo baa ama gesti. Na kama si mwenyeji wa dampo unaweza usielewe nini maana ya vibanda hivyo labda uwe na jicho la kihabari.

Kwa jicho la kawada unaweza kufikiri vijana na akina mama hao wamepumzika tu kwenye vibanda hivyo.

Kumbe katika vibanda hivyo wanawake hao wanavitumia kama sehemu ya kuuzia dawa za kulevya na pombe aina ya gongo, bia pamoja na biashara ya ngono.

Ni katika wanawake haohao wapo wanaotegemea dampo hilo kusomesha watoto na kutunza familia zao kwa kazi hiyo haramu.

Mmoja wa wanawake hao anasema wanafanya biashara hiyo kwa sababu ya maisha magumu, huku wengi wakiwa wametelekezwa na waume zao.

‘’Wanawake wengi unaowaona humu kila mtu ana historia yake; wapo waliotelekezwa na waume zao, wapo ambao wameolewa lakini wanaume hawatunzi familia na wengine ni wajane”anasema.

Anaongeza: “Maisha yamekuwa magumu dada, siku hizi wanawake ndiyo wamekuwa watunzaji na walezi wa familia,ndio maana unaona wanaamua kujiingiza kwenye biashara hatari kama hizi.’’

Kauli ya uongozi wa jiji

Mkurugenzi wa jiji la Dar es Salaam, Zipola Liana anasema wanatambua yanayoendelea katika dampo hilo.

“Ndiyo tunatambua kinachoendelea lakini tunao askari wetu ambao wanazunguka kukagua na kufanya kazi ya kudhibiti uhalifu wa aina yoyote ndani ya dampo ikiwamo vibaka”alisema.

Liana alipoulizwa kuhusu watu wanaoishi ndani ya dampo licha ya sharia kukataza na kufanya biashara alisema hao watu wamelifuata dampo wenyewe wakati wakijua ni hatari.