http://www.swahilihub.com/image/view/-/5123486/medRes/2349301/-/2os4mt/-/fursa+pic.jpg

 

Fursa mpya kwa viwanda, kilimo wakulima wakubwa, wadogo TADB

Na Elias Msuya, Mwananchi emsuya@mwananchi.co.tz

Imepakiwa - Monday, May 20  2019 at  13:30

 

Dar es Salaam. Licha ya kuajiri zaidi ya asilimia 60 ya Watanzania, kilimo kimekuwa cha kujikimu zaidi, kikichangia chini ya asilimia 30 ya Pato la Taifa.

Miongoni mwa changamoto za kilimo ni ukosefu wa mitaji. Kwa kujua mahitaji hayo, Serikali ilianzisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) ili kutoa mikopo na mitaji kwa wakulima.

Hivi karibuni, Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Japheth Justine aliiambia Mwananchi kuwa benki hiyo inalenga kuhamasisha utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Kilimo (ASDP 2) katika mitaji.

Anasema tangu ilipoanzishwa, TADB imeshatoa mikopo ya zaidi ya Sh102 bilioni ikitekeleza miradi 84 inayogusa zaidi ya watu milioni moja.

“Mwaka tulioanza kutoa mikopo kwa nguvu ni Julai 2017. Hii benki bado mpya, huu ni mwaka wa nne, tumeshazalisha Sh7 bilioni yaani faida na ndiyo zimeongezeka kwenye mtaji tuliopewa wa Sh60 bilioni,” anasema. “Kazi yetu ni kuchachusha mnyororo wa thamani kama viwanda au mazao. Mikopo yetu ina riba ndogo, wakati benki zinatoa riba asilimia 19 hadi 20 sisi ni 12, 10 mpaka 8.”

Justine anataja kilimo cha pamba ambacho anasema katika msimu uliopita TADB ilitoa mkopo wa Sh6.6 bilioni kuchangia ununuzi wa viuatilifu.

Anasema ununuzi huo ulichangia kuongezeka mavuno kutoka tani 130,000 hadi 220,000. Mpaka mwisho wa mwaka 2018 TADB imetoa mikopo kwa viwanda vinne vikiwamo vya mafuta ya alizeti mkoani Singida ambavyo anasema vimekopeshwa Sh5 bilioni.

Jinsi ya kukopa

Akifafanua mkopaji anayetaka kuanzisha kiwanda anavyoweza kunufaika, Justine anasema benki husaidia kununua mashine, “ukienda mabenki mengine watakupa miaka mitano, sisi tutakupa miaka 10. Kwa hiyo tunakurahisishia zile gharama ambazo ungeingia kununua mitambo.”

Akieleza jinsi mkulima anavyoweza kukopa, anasema sharti la kwanza ni kuonyesha soko la mradi wa kilimo anachotaka kukifanya. “Siyo mtu anakuja kutaka mkopo anapata. Nina majina ya vyama vya ushirika vinane tulivyokopesha, sita havilipi,” anasema.

Justine pia anasema benki hiyo imetoa Sh30 bilioni kusaidia zao la kahawa mkoani Kagera mwaka 2018. Walisaidia vyama vya ushirika vilivyokuwa na hali mbaya kutokana na mikopo ya nyuma isiyolipika vikiwamo Kagera District Cooperative Union (KDCU), Kagera Cooperative Union na Ngara Farmers’ Cooperative Union (KCU).

“KDCU, KCU vilikuwa na uwezo wa kununua asilimia 10 tu ya kahawa inayozalishwa Kagera, lakini baada ya kuwezeshwa na TADB, KDCU, KCU viliweza kununua kahawa yote asilimia 100. Baada ya mkopo wa Sh30 bilioni vimeondokana na madeni ya awali,’’ anasema.

Mikopo ya vihenge

Justine anasema kuna mkopo wa kujenga maghala maarufu kama vihenge, ili kukabiliana na upotevu wa mazao baada ya mavuno kati ya asilimia 30 hadi 40 hupotea kutokana na njia hafifu za uhifadhi.

“TADB inataka kuondokana na upotevu huo kwa kusaidia kuweka mpango wa kusaidia miradi midogo na ya kati ya kilimo kuwekeza katika ununuzi na usimikaji wa maghala ya chuma na mashine za kisasa za kusindika mazao ya kilimo ili yasipotee,” anasema..

Kuhusu namna ya kupata mkopo huo, Justine anasema mwombaji anapaswa kuwa na asilimia 30 ya mtaji anaotaka kukopa, kisha TADB itaongezea asilimia 70.

“Baada ya kupata mkopo, utatakiwa kulipa asilimia 70 tu ya mkopo. TADB itamalizia asilimia 30 iliyobaki,’’ anasema Justine.