http://www.swahilihub.com/image/view/-/1868744/medRes/520913/-/shl00e/-/bangaala.jpg

 

Serikali yaondoa kesi dhidi ya waliohusika na Bangla-Pesa

Changamwe

Mmoja wa wakazi wa Changamwe akiwa na Bangla-pesa Mei 29, 2013. Picha/MAKTABA 

Na GALGALO BOCHA

Imepakiwa - Friday, August 23  2013 at  17:28

Kwa Mukhtasari

Serikali imeondoa kesi dhidi ya watu waliohusika na mradi wa pesa mbadala za Bangla-Pesa mtaa wa Bangladesh, Mombasa na kusema haioni uhalifu wowote katika mpango huo. DPP Keriako Tobiko amesema hakuna makosa yaliyotekelezwa na washtakiwa baada ya kukagua faili ya kesi yao.

 

SERIKALI Ijumaa iliondoa kesi kuhusu mradi wa Bangla-Pesa na kusema haioni uhalifu wowote katika mpango huo.

Hakimu Mkazi wa Mombasa Vicky Kachuodho, alimwachilia huru msomi kutoka Amerika Bw William Ruddick na Wakenya wengine watano, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, Keriako Tobiko aliposema watano hao hawakuvunja sheria.

Taarifa ya kwanza kuhusu kuwepo kwa Bangla Pesa ilichapishwa na gazeti la Taifa Leo na tovuti ya Swahilihub Mei 28 mwaka huu.

Washtakiwa wengine ni Alfred Sigo Odhiambo, Emma Adhiambo Onyango, Paul Mwania Mwololo, Rose Auma Oloo na Caroline Dama Chirenga.

Kwenye barua iliyowasilishwa mahakamani, Bw Tobiko alikariri kwamba hakuna makosa yaliyotekelezwa na washtakiwa baada ya kukagua faili ya kesi yao.

Miezi miwili iliyopita, Bw Tobiko aliagiza faili ya kesi iwasilishwe mbele yake kwa ukaguzi na pendekezo zaidi, ambapo alisema kwamba angelihitaji taarifa fulani kutoka kwa benki kuu ya Kenya (CBK).

Hapo jana, Hakimu Kachuodho alielezwa kwamba CBK na Mamlaka ya Kodi na Mapato nchini (KRA), zimependekeza kwamba washtakiwa hawajakiuka sheria walipopatikana na stakabadhi zilizofanana na pesa za Kenya.

“CBK imethibitisha kwamba kutokana na maelezo ya kesi hakuna kosa lililofichuliwa chini ya sheria yake na KRA imethibitisha kwamba kutokana na maelezo ya kesi hakuna kosa ilifichuka chini ya Sheria za Ushuru wa Ziada (VAT),” ikaeleza barua kutoka afisi ya DPP.

Barua hiyo ikazidi kueleza: “Ningetaka kuagiza kesi ya uhalifu dhidi ya washtakiwa hao sita iweze kuondolewa chini ya sehemu ya 87(a) ya sheria ya uhalifu."

Hata hivyo, Bw Tobiko alipendekeza stakabadhi ya kesi hiyo iweze kupelekwa kwa idara ya benki ya kitaifa inayosimamia maswala ya sera na sheria kwa ajili ya utengenezaji wa sera kuhusu sheria husika siku za usoni.

Bw Ruddick kupitia wakili wake Leonard Shimaka aliomba mahakama kuagiza polisi kurudisha vitu vyote vilivyotwaliwa kutoka kwake.

Miongoni mwa vitu hivyo ni pamoja na kipatakalishi (laptop) iliyopelekwa kwa makao makuu ya idara ya upelelezi wa jinai jijini Nairobi kwa uchunguzi wa maabara.

Taarifa

Baada ya Taifa Leo kuangazia mradi wa pesa za Bangla mnamo mwezi Mei, polisi walianza kumtafuta Bw Ruddick ambaye alilazimika kujisalimisha katika kituo cha polisi cha Changamwe na kuandikisha taarifa.

Alisisitiza kwamba mradi wake sio ghushi na kwamba umeweza kufanyika katika mataifa kadha duniani kwa ajili ya kuinua maisha ya watu wasiojiweza.

Bw Ruddick ambaye ni mtaalamu wa masuala ya fedha alisema hundi zaidi ya 200 ya fedha za Bangla-Pesa zilizotolewa kwa wakazi wa mtaa duni ya Bangladesh huko Changamwe zilichapishwa jijini Nairobi.

Aidha alisema fedha hizo haina uhusiano wowote na fedha za kitaifa ya Kenya na kupuuzilia mbali madai ya kuvunja sheria.