http://www.swahilihub.com/image/view/-/1465132/medRes/351464/-/4xi4jbz/-/dnWanjiru2.jpg

 

Kifo kilimwandama Wanjiru saa 24

Samwel Wanjiru

Aliyekuwa bingwa wa mbio za Marathon Samwel Wanjiru baada ya kushinda dhahabu katika mbio za Olimpiki, Beijing Uchina. Alifariki Mei 15, 2011. Picha/MAKTABA 

Na MIKE KALAMA

Imepakiwa - Saturday, July 28  2012 at  10:22

Kwa Muhtasari

Kifo cha aliyekuwa bingwa wa Marathon na Olimpiki, Samuel Wanjiru ni kama kilikuwa kinamwandama saa 24 kabla ya kuaga dunia Mei 15 mwaka jana, kitabu kipya kuhusu maisha yake kinasimulia.

 

KIFO cha aliyekuwa bingwa wa Marathon na Olimpiki, Samuel Wanjiru ni kama kilikuwa kinamwandama saa 24 kabla ya kuaga dunia Mei 15 mwaka jana, kitabu kipya kuhusu maisha yake kinasimulia.

Kulingana na mwandishi wa kitabu kinachoitwa Running on Empty, Frits Conijin, siku ya kifo chake, Wanjiru alifanya mazoezi yake ya kawaida mjini Eldoret akiwa na meneja wake, Federico Rosa na kocha wake, Claudio Berardelli kabla ya kuanza safari ya kuelekea nyumbani kwake mjini Nyahururu.

Wanjiru aliamua kwenda nyumbani baada ya mkewe Triza Wanjiru kumpigia simu akimweleza kuwa hakuwa anajihisi vyema. Aidha Bi Wanjiru alihitaji gari lake ambalo alikuwa amemwazima mumewe ili asafirie kwenda Eldoret kwa mazoezi.

Wanjiru pia alinuia kuwasili Nyahururu ili kushughulikia kesi yake ya umiliki wa bunduki kinyume na sheria ambayo ilikuwa imemsumbua. Kocha wake alimpa malipo ya mapema ya takriban Sh2.1 milioni ambazo alinuia kuzitumia kuitoa kesi hiyo kutoka mahakamani.

Kabla ya kuondoka Eldoret, Wajiru alimuaga kocha wake ambaye alikuwa amechoshwa na tabia zake na kumuahidi kuwa angekuwa na nidhamu. Hata hivyo kulingana na kitabu hicho, ahadi ya Wanjiru haikudumu.

Baada ya kusafiri takriban kilomita 20, Wanjiru, ambaye aliandamana na mkiambiaji mwenzake, Daniel Gatheru, alisimamisha gari na kuingia kwenye baa moja ambapo alikunywa bia kadhaa na kubeba zingine alizoendelea kuzinywa akiendesha gari.

Kwa muda wa wiki mbili, Wanjiru alikuwa hajakunywa pombe kutokana na sheria kali alizowekewa na meneja na kocha wake katika kambi ya mazoezi ya Eldoret.

Baada ya kusafiri kwa kama kilomita 150, Wanjiru aliamua kupitia Nakuru ambako kulikuwa nyumbani kwa Judy Wambui, mmoja ya wapenzi wake.

“Alikunywa pombe zaidi alipofika nyumbani kwa Wambui kabla ya wawili hao kuingia kwenye chumba cha kulala ambako walikaa kwa muda,” anasema Conijin.

Gatheru aliamua kumgoja Wajiru sebuleni. Saa moja usiku Wanjiru alitoka kwenye chumba cha kulala akiwa mwenye hasira. Alimuaga mpenziwe haraka na kuendelea na safari ya Nyahururu.

Wanjiru alikuwa amelewa nusura apigane na mhudumu katika kituo cha mafuta ambaye alimshtumu kuwa alikuwa amemuwekea mafuta kidogo. Gatheru ndiye aliyemtuliza mkimbiaji huyo ili kuiwezesha safari yao kuendelea.

Safari iliendelea bila kisa chochote. Wawili hao waliwasili nyumbani kwa Wanjiru saa tatu usiku ambapo baada ya kuagana, Gatheru alienda zake kulala.

Nyumbani kwake kulikuwa kimya kwani mkewe na wanawe hawakupo. Hapo ndipo alipoamua kuwapigia simu marafiki zake ambao walikutana katika klabu ya Jim Rock katikati ya mji wa Nyahururu, ambapo walisherekea kwa kunywa pombe iliyonunuliwa na Wanjiru.

Kuchoshwa na baa

Hata hivyo, Wanjiru alipojisikia kuchoshwa na baa hiyo aliondoka pamoja na marafiki zake na kuelekea Water Resort, iliyo karibu na Maporomoko ya maji ya Thompsons.

Baada ya kunywa kuwa muda, kwa ghafla Wajiru alionekana kukasirika bila sababu.

Wanjiru alisema kuwa haoni tena maana ya kuishi na hata akatisha kujirusha kwenye maporomoko ya maji.

Alisema kuwa watu wanataka tu pesa zake, chakula na nguo na hakuna mtu ambaye alimjali. “Fikiria kuhusu wanao na pesa zako,” marafiki zake walijaribu kumbembeleza. Juhudi zao hatimaye zilizaa matunda wakati Wanjiru alipopata fahamu zake tena.

Alipokuwa akitoka kwenye baa hiyo, Wanjiru aligonga lango, jambo ambalo lilipekea wasimamizi wa baa hiyo kuwaita polisi. Maafisa wa polisi hata hivyo hawakumchukulia hatua yoyote wakisema kuwa alikuwa mlevi.

 “Kama saa nne unusu usiku, Wanjiru ambaye alikuwa mlevi sana aliingia kwenye gari lake na kuelekea katika Mkahawa wa Kawa Falls. Hii ilikuwa mara yake ya mwisho kuingia kwenye baa,” anasema mwandishi huyo.