Na SIMON SIELE ( email Mwandishi)
Imepakiwa - Monday, January 9 2012 at 10:47
Idara ya polisi imewataka wakuu wa vikosi hivyo kuvunjilia mbali 'mgomo baridi' unaoendelea miongoni mwa maafisa wa vyeo vya chini kupinga uhamisho hadi sehemu nyingine za nchi. Taarifa kutoka Vigilance House inawataka makamanda kuwafafanulia maafisa hao zaidi ya 1000 wenye vyeo vya konstebo ili kuelewa kwamba uhamisho wao ni wa kawaida na wala haunuii kuwadhulumu kwa vyovyote vile.
Msemaji Mkuu wa kikosi hicho, Bw Eric Kiraithe, aliiambia Taifa Leo kwa simu kwamba ingawa watakaohusika na uhamisho huo hawajalipwa marupurupu yao, “swala hilo litashughulikiwa
hivi punde.”
Hata hivyo, baadhi ya polisi waliohojiwa walilalamika kwamba kuna ubaguzi katika
kuwatambua watakaohamishwa. “Wakubwa wetu wanataka kutuhamisha kwenda sehemu zilizo na mazingira magumu ya kufanyia kazi, huku wakikosa kushughulikia marupurupu yetu,” akalalamika mmoja wa waasiriwa hao. Lakini Bw Kiraithe alipuuzilia mbali matamshi ya maafisa hao, huku akisisitiza kwamba uhamisho wa maafisa hao ni kati ya mbinu za kikosi hicho kudhibiti usalama wa nchi, hasa wakati huu ambapo Serikali imeanzisha 'Operesheni Linda Nchi'
dhidi ya Alshabaab. “Kenya inakabiliwa na vitisho vya kigaidi, ndiposa tunataka kuongeza maafisa wa polisi katika maeneo hayo na pia kama mbinu ya kukabiliana na changamoto za kiusalama wakati nchi hii inapojitayarisha kwa uchaguzi mkuu ujao,” Bw Kiraithe alisema.
Baadhi ya polisi walidai kwamba hatua hiyo haijapokelewa vyema, "kwani wengine wetu wanasalimishwa kwenda ughaibuni baada ya kufaulu kukabili visa vya utovu wa usalama katika sehemu mbali mbali, hasa kaunti ya Nakuru, ambapo wizi wa magari na bidhaa zinazosafirishwa kupitia barabara kuu ya Nairobi hadi nchi jirani, umekithiri.”