Na AGGREY MUTAMBO ( email Mwandishi)
Imepakiwa - Tuesday, February 21 2012 at 11:41Kwa Mukhtasari
Mudavadi asema alihudhuria hafla hiyo nyumbani kwa Waziri Mkuu, Bondo, kama afisa wa serikali wala sio mwanachama wa ODM.
Naibu Waziri Mkuu Musalia Mudavadi amekanusha madai kwamba alifanya kikao cha faragha na Rais Yoweri Museveni wa Uganda kuzungumzia siasa za ODM, na uhasama wa kisiasa kati yake na Waziri Mkuu Raila Odinga.
Jumatatu, Bw Mudavadi aliambia wanahabari katika Kaunti ya Kiambu kuwa alihudhuria hafla hiyo nyumbani kwa Waziri Mkuu, Bondo, kama afisa wa serikali wala sio mwanachama wa ODM.
Mudavadi alisema ilikuwa kawaida kwake, akiwa afisa mkuu wa serikali, kuhudhuria hafla ya kiongozi wa taifa lingine aliyezuru Kenya.
“Kwa kawaida, kiongozi wa taifa lingine anapotembelea nchi hii, maafisa wa Serikali kama mimi na wengine hutarajiwa kuhudhuria hafla anazohudhuria ili tuwe sehemu ya ziara hiyo na pia kuhakikisha Kenya imewakilishwa,” akaeleza.
Bw Mudavadi aliongeza kuwa suala la mgogoro kati yake na Bw Odinga halikuzungumziwa wakati wa hafla hiyo ya Jumamosi.
“Tulijadili masuala mengi yanayohusu nchi zote mbili na ni hayo tu. Kwa hakika, Museveni hangeweza kuingilia siasa za ODM. Alizungumzia masuala yanayoathiri Jumuiya ya Afrika Mashariki,” akasema Mudavadi. “Nataka tuheshimu hilo kwa sababu tunamzungumza kuhusu kiongozi wa taifa.
Itakuwa vibaya kuripoti uvumi kuhusu kiongozi wa taifa jirani.”
Kuonyesha umoja katika ODM
Taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari kutoka kwa Idara ya Habari ya Waziri Mkuu baada ya hafla hiyo ilisema kuwa Mudavadi alihudhuria hafla hiyo kuonyesha umoja wa chama cha ODM na kuondoa dhana ambao imeenea miongoni mwa watu wengi, kwamba kuna mgogoro wa kisiasa kati yao.
Lakini msemaji wa Bw Mudavadi, Bw Kibisu Kabatesi, alituma taarifa nyingine kwa vyombo vya habari, akisema mkutano huo haukuhusu chama cha ODM.
Hapo jana, Bw Mudavadi alikiri kuwa aliruhusu taarifa hiyo itumwe kwa vyombo vya habari, lakini akasema hakuna mgogoro wowote katika chama cha ODM kutokana na nia yake ya kuwania tiketi ya urais kwa chama hicho.
Wakati huo huo, Bw Mudavadi alisema wanachama wengi wa ODM wanaunga mkono ushindani kati yake na Bw Odinga, na akakanusha madai kwamba baadhi ya wabunge wa ODM walimwendea wiki jana wakimtaka amwachie waziri mkuu nafasi hiyo.
“Nafikiri ripoti hiyo haikuwa sahihi, kwa sababu, ingawa sikuhudhuria mkutano wa awali, baadhi ya wanachama waliohudhuria mkutano huo walitaja hatua hii kuwa muhimu sana kwa demokrasia na uthabiti wa chama.
“Wanachotaka kuona ni uchaguzi wa heshima, ambao hautamalizika kwa mtu kumtukana mwingine, kwa kuwa tuko kwenye chama kimoja na ni lazima sote tujaribu kuwashawishi wajumbe. Atakayefaulu kushawishi wengi ndiye atakayepata tiketi hiyo.”
Alikutana na wajumbe
Bw Mudavadi alikuwa akizungumza mjini Ruiru, ambako alikutana na wajumbe kutoka maeneo bunge 8, huku akiendelea kuvumisha sera zake.
Hata hivyo, baadhi ya wajumbe walimtaka amalize mgawanyiko baina yake na mpinzani wake, Bw Odinga.
Wakati wa mkutano huo, mwenyekiti ODM, tawi la Kaunti ya Kiambu, Marion Mbugua, alisema kuna hatari ya mgawanyiko huo kutatanisha wafuasi wa ODM katika eneo hilo. “Ni lazima tudumishe umoja Kenya, chini ya chama cha ODM. Ni lazima pia ODM ibaki chama kimoja chini ya uongozi wa Musalia na Odinga hadi tutakapopiga kura mwisho wa mwaka huu. Msipofanya hivyo hatutajua pa kuegemea,” akasema.
Wabunge 175 nchini Zimbabwe watapashwa tohara kufikia mwisho wa mwezi ujao katika juhudi za kuhamasisha wanaume
MWANAWE Waziri wa Fedha Njeru Githae anadaiwa kujiua nyumbani kwao Runda, Nairobi. Polisi wameanzisha uchunguzi
Polisi wameanzisha msako mkali kutafuta washukiwa waliotekeleza shambulio la kigaidi katika mkahawa wa Bella Vista,
Ibada mbili tofauti zilifanywa kuadhimisha mwaka mmoja tangu kifo cha bingwa wa marathon katika Olimpiki Samuel