HABARI ZA SIASA
Picha/MAKTABA Waziri wa Mazingira John Michuki, akihutubia wanahabari afisini mwake mwaka 2011.
Na JUMA NAMLOLA ( email Mwandishi)
Imepakiwa - Wednesday, February 22 2012 at 14:54Kwa Mukhtasari
Kwa zaidi ya saa nzima, wabunge walisimama na kumtaja Bw John Michuki kuwa mwanasiasa aliyekuwa na msimamo; ndani na nje ya bunge.
BUNGE Jumatano lilitumia muda wa Mawasiliano kutoka kwa Spika kutuma rambirambi kwa ndugu na jamaa ya marehemu John Michuki.
Kwa zaidi ya saa nzima, wabunge walisimama na kumtaja Bw Michuki kuwa mwanasiasa aliyekuwa na msimamo; ndani na nje ya bunge.
Naibu wa Spika Bw Farah Maalim alianza kwa kulifahamisha bunge kuhusu kifo cha Bw Michuki, na kukitaja kuwa msiba mkubwa.
Mbunge wa Dujis Bw Aden Duale alisema kuwa alimtambua Bw Michuki kuwa mpole lakini aliyependa kutoa masharti yake kwa watu aliokaribiana nao.
“Bw Spika, nataka kusema kuwa nimewahi kukaa na marehemu mheshimiwa Michuki. Alikuwa mwepesi wa kukufanyia lolote, mradi utii masharti yake. Angekununulia chai na mzungumze, lakini usitumie simu yako,” akasema.
“Nakumbuka siku moja tulikuwa tunakunywa naye chai na mheshimiwa Keynan kwa kutumia simu yake tukiwa pamoja,” akasema.
Naibu Kiongozi wa shughuli za Serikali Bungeni Bw Amos Kimunya, alisema Bw Michuki hakuwa waziri tu bali rafiki na mtu aliyemshawishi kuingia kwenye siasa.
“Najua Wakenya wengi hawana habari. Mheshimiwa Michuki, Rais Kibaki na mheshimiwa George Muhoho waliniketisha chini Aprili 2002 na kunishawishi niingie katika siasa,” akasema.
Serikali ya kwanza ya muungano
Mbunge huyo wa Kipipiri alisema kwamba mwaka 2008, alishirikiana na Bw Michuki kujadili jinsi ya kubuni serikali ya kwanza ya muungano kwa kuruhusu wabunge wa chama cha ODM Kenya.
“Tuliketi na Bw Michuki tukajadiliana na kukubaliana kubuni muungano huo. Alikuwa mara kwa mara akiniambia kwamba ukiwa kiongozi, huna budi kufanya uamuzi bila kujali kama watu wataukubali au kuukataa. Nataka niseme kuwa nimempoteza rafiki wa kweli,” akasema.
Bw Kimunya ambaye anasimamia wizara ya Uchukuzi, iliyoimarika wakati ikiwa chini ya Bw Michuki, aliwaomba wabunge wawaombee wanasiasa wengine aliosema wanaugua.
“Naomba kila mmoja wetu awaweke katika maombi wanasiasa wengine wote wanaougua,” akasema.
Mbunge wa Manyata Bw Emilio Kathuri alisema alimgahamu Bw Michuki akiwa mfanyibiashara katika sekta ya matatu.
“Kuna siku alikuja Embu na kukutana na wadau katika sekta ya uchukuzi. Hata kabla ya salamu, alitueleza yale aliyoamini kuwa yalikuwa muhimu kwetu,” akasema.
Mbunge huyo alisema kutokana na utendakazi wa Bw Michuki, anaamini kama angelikuwa waziri wa Ulinzi, tatizo la Al-Shabaab lingelikuwa limemalizika kitambo.
Alikuwa mkali na mfuata kanuni
Aliyekuwa wakati mmoja Katibu katika wizara ya Usalama na Utawala wa Mikoa Bw Zakayo Cheruiyot, alisema Bw Michuki alikuwa mtumishi wa umma aliyekuwa mkali lakini aliyefuata kanuni bila mapendeleo.
Bw Cheruiyot anayewakilisha eneo bunge la Kuresoi, alimtaja Bw Michuki kuwa mtu aliyetoa mfano bora wa kuigwa na watumishi wa umma.
“Yeye alikuwa mtu aliyeamini utendakazi usio na kasoro. Alikuwa mkali lakini aliyetenda haki kwa wote,” akasema.
Lakini mbunge wa Gichugu Bi Martha Karua alisema ingawa Bw Michuki alikuwa rafiki na mwandani siku za awali, baadaye walitengana na kila mmoja akawa anafuata sera zake.
“Namtambua kama Mkenya aliyekuwa mchapa kazi. Lakini nataka kukiri kuwa ingawa awali tulikuwa tukisikizana, siku za mwisho wa uhai wake hatukuwa tunapatana kisera,” akasema Bi Karua.
Akichangia muda huo wa kutoa rambirambi, mbunge wa Wundanyi Bw Thomas Mwadeghu alisema waliwahi kuketi na Bw Michuki na kujadiliana kwa kina kuhusu Mswada wa Madini.
“Tulikubaliana kuhusu mswada huo ambao utakuwa na umuhimu mkubwa kwa nchi. Nawaomba wabunge wenzangu, kama heshima zetu kwake, mswada huo ukija hapa bungeni tuupitishe,” akasema.
Wabunge 175 nchini Zimbabwe watapashwa tohara kufikia mwisho wa mwezi ujao katika juhudi za kuhamasisha wanaume
MWANAWE Waziri wa Fedha Njeru Githae anadaiwa kujiua nyumbani kwao Runda, Nairobi. Polisi wameanzisha uchunguzi
Polisi wameanzisha msako mkali kutafuta washukiwa waliotekeleza shambulio la kigaidi katika mkahawa wa Bella Vista,
Ibada mbili tofauti zilifanywa kuadhimisha mwaka mmoja tangu kifo cha bingwa wa marathon katika Olimpiki Samuel