HABARI ZA SIASA

Nchi yaomboleza kufuatia kifo cha Michuki

Waziri John Michuki

Picha/MAKTABA Waziri wa Mazingira John Michuki, akihutubia wanahabari afisini mwake mwaka 2011. 

Na MWANGI MUIRURI  ( email Mwandishi)

Imepakiwa - Wednesday, February 22  2012  at 15:3

Kwa Mukhtasari

Rais Mwai Kibaki, alimtaja kama “rafiki wa ndani, mshauri wa kuaminika na kiungo thabiti katika Serikali yangu.” Wabunge nao walitumia takriban saa nzima kumuomboleza.

BIWI la simanzi lilitanda kote nchini Jumatano habari za kifo cha Waziri wa Mazingira John Michuki huku wengi wakieleza masikitiko yao kutokana na tanzia yake.

Rais Mwai Kibaki, alimtaja kama “rafiki wa ndani, mshauri wa kuaminika na kiungo thabiti katika Serikali yangu.”

Hadi kifo chake, alikuwa amemuidhinisha Bw Uhuru Kenyatta, kama mrithi mwafaka wa Rais Kibaki, hali ambayo iligeuza mkondo wa kisiasa kuwa na upinzani mkali kwa wagombezi wengine katika eneo hilo.

Wabunge walitumia takriban saa nzima kumuomboleza.

Majonzi aidha yalitanda katika Kaunti ya Murang’a na viunga vyake huku vyombo vya habari vinavyotangaza kwa lugha ya Kikikuyu ikiwemo Kangema FM aliyokuwa akimilki vikitoa mitambo yao ili wananchi watume risala zao za rabirabi kwa mwendazake.

Bw Michuki akiwa na umri wa miaka 80 na ambaye pia alikuwa Waziri wa Mazingira aliaga dunia usiku wa kuamkia Jumatano mwendo wa saa tatu kutokana na maradhi ya moyo.

“Sitaki kuamini habari hizo ni za ukweli. Lakini kwa upande mwingine vyombo vya habari haviwezi kunidanganya haswa ikiwa ni Rais Mwai Kibaki amethibitisha habari hizo. Nitamkosa. Mungu aiweke roho ya mbunge wangu mahali pema peponi,”  akasema Bi Mary Karanja, mkazi wa Kangema.

Katika eneo bunge la Kangema, majonzi yalitanda katika nyumba nyingi ikizingatiwa kuwa zaidi ya asilimia 50 ya wenyeji  hujumuika kama familia yake.

Hali hiyo inatokana na kuwa, babake Michuki Mzee Michuki Kagwi alikuwa na mabibi 47 na ambapo yeye alikuwa kifungua mimba wa Bi Marion Wanjiku ambaye alikuwa bibi nambari 45.

Umaarufu na kupendwa kwa marehemu Michuki kulijidhihirisha wazi, huku shughuli za kawaida katika maeneo mengi zikikwama watu walipojikusanya vikundivikundi kujadili suala hilo.

Miongoni mwa masuala yaliyomshidia umaarufu katika eneo hilo ni rekodi yake ya maendeleo, kutositasita kwake kukabiliana na masuala nyeti ya jamii, kuwa aliyejitokeza kuungana na watu wake wakati wa sherehe mbalimbali na pia misimamo yake mikali ya mujibu wa sheria.

Ulainishaji wa sekta ya matatu kupitia Sheria za Michuki na pia kusambaza maji na umeme kote katika eneo bunge lake kulimfanya awe kiongozi wa hadhi kuu katika jamii za Mlima Kenya na taifa lote kwa jumla.

Wengi walimpenda kwa kuwaondolea jinamizi la Mungiki, kundi haramu ambalo kwa wakati mrefu lilikuwa limewahangaisha kwa kuwatoza kodi haramu na pia kutekeleza mauaji ya kiholela kupitia kuwakata vichwa waathiriwa.

Kwa wakati mmoja mwaka wa 2007 akiwa katika ibada ya kanisa la Kianglikana la Nyakahura, Bw Michuki alisisitiza kuwa hakuna vile “vijana waliopotoka na kuwa wenda wazimu wangekubaliwa kuhangaisha watu wakidai kubebelezwa eti ulikuwa mwaka wa uchaguzi.”

“Nataka niseme hapa waziwazi kuwa afadhali mtunyime kura zenu lakini hakuna vile tutabadilishana kura na maisha ya watu. Kuanzia leo, mtakuwa mnasikia kuhusu mazishi ya vijana hao,” akasema akiwa amesimama mbele ya waumini hao.

Mkuu wa Wilaya ya Murang’a Bw George Natembeya ambaye kabla ya kuteuliwa kwake wadhifa huo alikuwa msaidizi wa Bw Michuki katika Wizara ya Usalama wa ndani alimtambua marehemu kama “mwadilifu, asiyependa njia za mkato na ambaye hakuwa na huruma kwa maafisa wazembe.”

Bw Natembeya alisema Bw Michuki alikuwa na msimamo mmoja tu katika kushuruhisha suala lolote.

“Alikuwa akiuliza vile sheria inasema kuhusu suala hilo. Ukitambua hivyo, anakwambia ufuate na utekeleze sheria hiyo. Ukilalamika sheria hiyo ni mbovu alikuwa anakwambia ndiyo iliyoko itumike mpaka wabunge wagundue inafaa kurekebishwa,” akasema.

Katibu Mkuu katika Wizara ya Ustawi wa Mifugo Bw Ken Lusaka ambaye pia alihudumu mwaka wa 2004 hadi 2008 katika Wilaya ya Murang’a alimtaja Bw Michuki kama “raslimali ya kitaifa ambayo imetupotea.”

“Alikuwa kiongozi wa vitendo na alikuwa akisisitiza majadiliano katika suala lolote. Alichukia uongo kwa nafsi yake yote. Naomboleza pakubwa kupoteza rafiki, mwandani na aliyenisaidia kukwea mlima wa utumishi kwa umma,” akasema.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Garissa Bw Albert Kimathi ambaye pia alihudumu katika Wilaya ya Murang’a chini ya Ubunge wa Michuki alisema taifa limepoteza “mzalendo na mpenda maendeleo.”

Bw Kimathi ndiye alikuwa akishirikisha vita dhidi ya Mungiki mwaka wa 2007 ambapo takriban washukiwa 600 waliuawa.

“Bw Michuki alikuwa akinipigia simu kila asubuhi akitaka kujua tumefikisha wapi vita hivyo. Alikuwa akivitaja kama vita vya kukomboa jamii kutokana na ufidhuli wa magaidi,” akasema.

Bw Kimathi alifichua kuwa kwa mwaka huo wote ambao vita hivyo vilidumu, Bw Michuki alikuwa akitembelea eneo hilo kila wiki kuhimiza wananchi waunge mkono vita hivyo kwa manufaa yao wenyewe.

“Leo hii, sina shaka yoyote kuwa kaunti ya Murang’a inajivunia usalama na utulivu kufuatia kuangamizwa kwa kundi hilo. Lilikuwa hata linadai mahari kwa niamba ya wazazi wa eneo hilo huku biashara nyingi zikifungwa,” akasema.

 

Most Popular

Wabunge 175 kutahiriwa Zimbabwe

Wabunge 175 nchini Zimbabwe watapashwa tohara kufikia mwisho wa mwezi ujao katika juhudi za kuhamasisha wanaume

Mwanawe Waziri wa Fedha ajitia kitanzi

MWANAWE Waziri wa Fedha Njeru Githae anadaiwa kujiua nyumbani kwao Runda, Nairobi. Polisi wameanzisha uchunguzi

Polisi waendelea kusaka walioshambulia Mombasa

Polisi wameanzisha msako mkali kutafuta washukiwa waliotekeleza shambulio la kigaidi katika mkahawa wa Bella Vista,

Utengano wakumba ukumbusho wa Wanjiru

Ibada mbili tofauti zilifanywa kuadhimisha mwaka mmoja tangu kifo cha bingwa wa marathon katika Olimpiki Samuel