Maisha ya mwigizaji Lulu katika namba

 

Imepakiwa - Thursday, May 17  2018 at  14:26

Kwa Muhtasari

Elizabeth Michael maarufu Lulu ni jina lilitajika sana kabla na baada ya kifo cha Steven Kanumba. Akiwa mwigizaji kinda wa tamthilia za Gharika, Dira na Baragumu na pia mtangazaji wa kipindi cha Watoto Wetu kilichokuwa kikirushwa ITV.

 

Elizabeth Michael maarufu Lulu ni jina lilitajika sana kabla na baada ya kifo cha Steven Kanumba. Akiwa mwigizaji kinda wa tamthilia za Gharika, Dira na Baragumu na pia mtangazaji wa kipindi cha Watoto Wetu kilichokuwa kikirushwa ITV.

23

Ndiyo umri wa binti huyu aliyejipatia umaarufu katika uchezaji wa filamu na utangazaji. Alizaliwa Aprili 16, 1995

5

Alianza kuigiza filamu akiwa mtoto wa miaka mitano. Mwigizaji nguli Mahsein Awadhi maarufu Dk Cheni ndiye aliyevumbua kipaji chake wakati akisaka waigizaji wapya.

2

Idadi ya vipindi vya televisheni alivyowahi kuongoza Lulu kati ya mwaka 2005-2015. Amewahi kuwa mtangazaji wa vipindi vya Watoto Wetu na Tanzania Movie Talent (TMT).

11

Idadi ya tamthilia alizowahi kuigiza zikiwamo Baragumu, Zizimo, Gharika, Sayari, Tufani, Tetemo, Jahazi, Dira, Demokrasia, Taswira na Sarafu ambayo alianza kuigiza miezi michache kabla ya kuhukumiwa.

4

Lulu amewahi kushinda tuzo kubwa nne ndani na nje ya nchi ambazo ni Zanzibar International Film Festival, Africa Magic Viewers Choice Awards, Swahili Fashion Week Awards na Tanzania People’s Choice Awards.

17

Ndiyo umri aliokuwa nao wakati anaingia matatani kwa tuhuma za kumuua mwigizaji mwenzake Steven Kanumba ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka 28. Ilidaiwa kuwa Aprili 7, 2012 mwigizaji huyo alimuua bila kukusudia Kanumba aliyekuwa mpenzi wake.

494

Idadi y a siku alizopaswa kukaa gerezani baada ya kuhukumiwa kifungo cha miaka miwili jela. Mwigizaji huyu alihukumiwa Novemba 12 mwaka jana na adhabu yake ingeisha Machi 12, 2019.

120

Hii ni idadi ya siku alizopunguziwa katika msamaha wa Rais John Magufuli aliotoa kwa wafungwa mbalimbali wakati wa sherehe za Muungano mwaka huu. Kufuatia msamaha wa Rais, Lulu angetoka gerezani Novemba 12 mwaka huu badala ya Machi 13, 2019.

512

Saa ambazo Lulu atazitumia kufanya kazi ikiwa ni mbadala wa kifungo cha gerezani. Kila siku kwa siku 184, mwigizaji huyu atatumia saa nne kufanya kazi za kijamii kwa kufanya usafi wa mazingira katika ofisi za Wizara ya Mambo ya Ndani jijini Dar es Salaam.

182

Katika siku 182 zilizosalia katika kifungo chake, Lulu afanya kazi siku 128 tu ambayo ni sawa na saa 512 au dakika 262,080. Katika kipindi huku atapumzika Jumamosi 27, Jumapili 26 na sikukuu tatu za Eid El Fitr, Nane Nane na Eid el- Adha.