Mbona urembo na imani wala havihusiani jamani!

 

Imepakiwa - Thursday, May 17  2018 at  15:27

Kwa Muhtasari

SAUTI yenye ushawishi. Sauti ya dhahabu. Sauti yenye mvuto na upako inayotiririka kwenye nyimbo za Injili. Ni sauti ya Christina Shusho.

 

SAUTI yenye ushawishi. Sauti ya dhahabu. Sauti yenye mvuto na upako inayotiririka kwenye nyimbo za Injili. Ni sauti ya Christina Shusho.

Mwanadada huyu ameshika hatamu kwenye nyimbo za injili nchini. Ametoa nyimbo nyingi. Amefanya matamasha mengi na bado anaendelea kufanya. Tangu ameanza kuimba miaka zaidi ya 14 iliyopita, hajachuja mpaka sasa. Inafurahisha sana.

Uchunguzi uliofanywa na Mwanaspoti mwaka jana ulibaini kuwa Mwanadada huyu anauza. Sura yake inapokaa kwenye kava la CD inampa mteja hamu ya kutoa pesa yake kununua, hasa nchini Kenya.

Hata kwa upande wa tungo zake, mara nyingi zinagusa maisha ya kawaida na yale ya kiroho. Nyimbo zake zimekuwa kivutio kikubwa kwa mashabiki wa muziki wa Injili hasa na kutokana na sauti yake nzuri utakayopenda kuisikia mara kwa mara.

Sasa huyo Shusho unaambiwa siku hizi kanenepa hatari, lakini rangi yake imeendelea kuwa ile ile yenye mvuto wa kipekee.

Pia sio mtu wa skendo kama wale waimbaji wengine ambao kila siku utasikia mara hili, mara lile.

Mwanaspoti ambalo ndiyo gazeti pekee la Michezo linalochapwa kwa Kiswahili nchini Tanzania na Kenya, limefanya mahojiano mafupi na Mwimbaji huyo ambaye amekuwa akifanya kazi zake katika nchi hizo mbili.

Mwanaspoti: Habari yako Madam Christina?

Christina Shusho: Nzuri tu

Mwanaspoti: Naomba tuzungumze machache hasa kuhusu muziki wako.

Chiristina Shusho: Sawa haina neno, karibu.

Mwanaspoti: Changamoto gani unazozipata katika muziki?

Christina Shusho: Ni kuwa mfano mzuri katika jamii.

Mwanaspoti: Inadaiwa una maringo na unapenda kujitenga na wanamuziki wenzako wa Injili, hizi habari ni za kweli?

Christina Shusho: Huwa nasikia hizo habari kuwa naringa. Ngoja niweke wazi hili suala, mimi sina tabia ya kuringa na wanaosema hivyo hawajanizoea na hawako karibu na mimi. Ni kawaida kwamba nikiwa ugenini huwa sio mtu wakuongea ongea sana ndio maana naambiwa naringa.

Kwa upande wa kujitenga na wasanii wenzangu, hilo sio kweli, ila sijajua watu wanataka muda wote tuwe tunaongozana au vipi?

Mwanaspoti: Ni mwimbaji gani wa Injili unayemkubali zaidi?

Christina Shusho: Wote walionitangulia katika muziki wa Injili, nawakubali sana.

Mwanaspoti: Unaweza kuwataja baadhi yao?

Christina Shusho: Ndio, kuna Bahati Bukuku, Rose Muhando, Flora Mbasha na wengine wengi walionitangulia, nawakubali.

Mwanaspoti: Umewahi kusalitiwa katika mapenzi?

Christina Shusho: Duu! Hapana siwezi jibu hili swali, ila kusalitiwa katika mambo ya kawaida nilishasalitiwa na hiyo ni kawaida kwa kila mtu.

Mwanaspoti: Huwa unasikiliza muziki mwingine tofauti na Injili?

Christina Shusho: Ndio, tena wanangu wanapenda pia muziki wa Bongofleva.

Mwanaspoti: Unaimba Injili kama kazi ya Mungu au unatafuta pesa?

Christina Shusho: Naimba kama kazi ya Mungu, na pia suala la pesa linakuja pale unapofunga albamu. Hapo inaingia suala la soko halafu biashara, hivyo kwa upande mwingine pesa inaingia katika uimbaji wangu na inakuwa imebarikiwa na Mungu.

Mwanaspoti: Wewe ni mpenzi wa timu gani ya soka hapa Tanzania?

Christina Shusho: Aisee! Sina timu, ila napenda sana soka.

Mwanaspoti: Watu wanasema wewe sio Mtanzania, ni kweli?

Christina Shusho: Mimi ni Mtanzania halisi sema watu wanashindwa kunitenga na nchi nyingine hasa Kenya kutokana na kufanya nao kazi mara kwa mara.

Mwanaspoti: Watu wengi wana imani ya kuwa, ukiwa Mcha Mungu haitakiwi ujihusishe ma urembo na makanisa yanakataa urembo, wewe unazungumziaje hili?

Christina Shusho: Mh! Kwanza mimi imani yangu haikatazi kuwa mrembo, hivyo inategemea kila mtu na imani yake kwa kweli, ndio maana mimi unaniona siko nyuma na urembo.

Mwanaspoti: Wimbo gani unaoupenda katika nyimbo zako zote?

Christina Shusho: Wimbo wa Nangoja

Mwanaspoti: Kwanini?

Christina Shusho: Kwa sababu maneno yake kwenye huo wimbo huwa yananipa moyo sana na yanafunza mtu asikate tamaa.

Mwanaspoti: Asante sana

Christina Shusho: Haya karibu tena.