Mobetto aweka wazi staili yake mpya

 

Imepakiwa - Friday, May 18  2018 at  09:51

 

HAMISA Mobetto ambaye ni mzazi mwenza wa nyota wa Bongo Fleva, Diamond Platinumz, amesema kwa sasa ameamua kukaa kimya licha ya watu wengi wamekuwa wakifuatilia maisha yake na kumsema vibaya.

“Sishtushwi na wala sijibizani na mtu. Ila wajue sitarudi nyuma kwa maneno maneno ya watu, hao wenye kazi ya kufuatilia maisha yangu hawanibabaishi,” alisema.

Kauli ya mwanamitindo huyo maarufu ambaye pia ni muuza sura katika video za Bongo Fleva, imekuja baada ya kuulizwa juu ya madai ya kupigwa na Mama wa Diamond, Bi. Sandra.

Hamisa alisema hawezi kuzungumza chochote kuhusu madai hayo, ila maisha anayoishi kipindi hiki ni ya kukomaa kivyake kuliko kuchunguza ya mtu mwingine.

Alisema kila kukicha anafikiria afanye nini ili aweze kupambana na maisha ya sasa, ukizingatia ana watoto wawili wanaohitaji malezi na elimu bora, hata kama baba zao wanawalea.

“Hizo habari achana nazo, sasa napambana na maisha yangu. Sina muda wa kuhangaika na maisha ya mtu mwingine wala kuyajua yasiyonihusu au yanayosemwa,” alisema mrembo huyo ambaye mtoto wake wa kwanza amezaa na mmoja wa vigogo wa EFM na TV E, Majizo.