Dhuluma: Mke aukata uume wa mumewe kwa panga

Na ERIC WAINAINA

Imepakiwa - Monday, July 17  2017 at  18:32

Kwa Mukhtasari

MWANAMUME katika Kaunti ya Kiambu anauguza majeraha mabaya katika uume wake baada ya mkewe kudaiwa kumshambulia akidai kuwa mumewe anamsengenya kwa wanawake wengine kijijini.

 

Bw Andrew Kamau, 49, kutoka kijiji cha Githirioni, kaunti ndogo ya Lari amelazwa katika hospitali ya Misheni ya Kijabe, baada ya mkewe Hannah Wanjiru kudaiwa kumshambulia kwa upanga.

Kulingana na Bw Kamau, alipokea simu kutoka kwa mwanakijiji mwanamke, wanayefahamiana, na ambaye alikuwa akitumia simu ya mkewe, na kudai ilikuwa imeokotwa barabarani na watoto. Pia alimtaka amueleze mkewe aende akaichukue kwake.

Lakini alipomaliza kuongea kwa simu, mkewe ambaye alikuwa kando yake alidai kuwa alikuwa akimsengenya kwa simu na mwanamke mwingine na kutaka kujua kwa nini alikuwa akifanya hivyo.

Bw Kamau ambaye hufanya vibarua kujipatia kujikimu alisema alijaribu kumuelezea mkewe mazungumzo hayo yalihusu nini lakini hakufaulu.

“Vita vilianza na nilifaulu kumwangusha chini. Niliwacha kumpiga na kisha kumuonya dhidi ya kuibua shtuma zisizokuwa na msingi, na kutumia nafasi hiyo kumuelezea nilichokuwa nikiongea kwa simu,” alisema.

Lakini akiwa anaendelea na mazungumzo na mkewe akiwa chini, mwanae wa kiume alichukua upanga na kumgonga nao nyuma ya kichwa, na kumfanya apoteze fahamu. Hata hivyo, alidai kuwa mkewe alichukua panga kutoka kwa mwanae na kumkata sehemu nyeti kabla ya kutoroka.

“Nilipopata fahamu nilihisi maumivu makali na kugundua nilikuwa nikivuja damu kichwani na katika sehemu nyeti, kabla ya kugundua walikuwa wamenikata na kuniumiza vibaya,” alisema akiongeza kuwa alipotazama alimuona mkewe na mwanae wakitoroka.

Hata hivyo, alifaulu kupiga kamsa zilizovutia majirani ambao pia walimwandama mkewe, na pia kumpeleka Bw Kamau kwa kliniki ya Kanisa la Presbyterian Church of East Africa Uplands kabla ya baadaye kuhamishwa hospitali ya Kijabe.

Baadhi ya wakazi kisha walimpeleka mkewe hadi kwa kituo cha polisi cha Uplands ambapo anazuiliwa, na kaimu afisa mkuu wa polisi, Bw Stanley Mutungi akithibitisha tukio hilo alisema uchunguzi unaendelea. Pia alisema kuwa mshukiwa atafikishwa mahakamani muda uchunguzi utakapokamilika.

Kadhalika, madaktari walisema Bw Kamay hayuko hatarini sasa na kuwa baada ya ya matibabu atapona kanisa na viungo vyake kufanya kazi kama kawaida.