http://www.swahilihub.com/image/view/-/1736832/medRes/485081/-/icjedy/-/FurikoNyando.jpg

 

Watu sita wafariki baada ya kusombwa na mafuriko

Jane Achieng

Bi Jane Achieng, mmoja wa walioathiriwa na mafuriko kijiji cha Kojiem, Nyando Aprili 1, 2013. Picha/TOM OTIENO 

Na WAANDISHI WETU

Imepakiwa - Tuesday, April 2  2013 at  07:40

Kwa Muhtasari

Watu sita walikufa baada ya kusombwa na mafuriko katika visa tofauti  kaunti ya Kajiado kufuatia mvua kubwa inayoendelea kunyesha kote nchini.

 

WATU sita walikufa baada ya kusombwa na mafuriko katika visa tofauti  kaunti ya Kajiado kufuatia mvua kubwa inayoendelea kunyesha kote nchini.

Katika kisa cha kwanza watu watatu waliangamia matatu aina ya Nissan liliposombwa na maji mto Kandisi eneo la Kiserian ulipofurika.

Katika kisa cha pili mita chache kutoka mto huo abiria katika matatu iliyotoka Kiserian kuelekea Ongata Rongai walinusurika kifo baada ya gari hilo kuzuiliwa na kuta katika mto wa Lemalepo iliposombwa na maji.

Magari mawili yaliharibiwa na mafuriko  kwenye barabara ya Magadi hatua chache kutoka eneo hilo.

“Tumejitahidi kutafuta miili ya waliosombwa usiku wote,” alisema dereva wa matatu,” Bw  Albert Ndege.

Alisema dereva wa matatu iliyosombwa eneo la Kandisi aliepuka kifo baada ya kukwama kwenye mti.

“Dereva alituambia kwamba kulikuwa na watu wanne katika gari hili mkasa huo ulipotokea. Walikuwa wakisubiri maji yapungue lakini mambo yakabadilika,” alisema Bw  Ndege.

“Mafuriko yalitokea ghafula na kusomba gari yao. Miili mitatu ya mtoto, mwanaume na mwanamke ilitolewa takriban kilomita mbili kutoka eneo la mkasa ilhali mwili wa mtu mmoja haujapatikana,” akasema Bw Ndege.

Mvua hiyo ilisababisha uharibifu mkubwa kwenye mashamba ya watu huku ua za nyumba za makazi karibu na mto huo zikiharibiwa pia.

Huko Magadi mwanaume kwa jina Mwangi Wamae 40, alikufa akijaribu kuvuka mto  Entasapia huku miili miwili ikipatikana eneo la  Veterinary mjini Ngong baada ya kusombwa na maji ya mto Ngong. Mkuu wa wilaya ya Kajiado kaskazini Bw Mwangi Kahiro alisikitishwa na vifo hivyo akisema maeneo mengi ya wilaya yaliathiriwa na mvua kubwa.

Mbunge wa Kajiado kaskazini Bw Joseph Manje alisema eneo hilo hukubwa na mafuriko kila mwaka na kuwataka wakazi kuwa waangalifu kwa sababu mafuriko katika mito hiyo yamekuwa yakiwaua watu kila mwaka.  Naye seneta wa kaunti hiyo Bw  Peter Mositet alilaumu daraja duni katika mito hiyo kwa kusababisha vifo vya wakazi.

“Mwaka jana watu wanne walipoteza maisha  mto wa  Kandisi ulipofurika. Hatua zilizochukuliwa na wizara ya barabara hazitoshi kwa sababu tatizo hilo limerejea tena,” alisema Bw Mositet.

Katika kaunti ya Kisumu wakazi wa wilaya ya  Nyando walitaka serikali ijenge matuta na vituo vya kukimbilia wakati wa mafuriko.. Mzee wa eneo hilo Bw Stephen Ochieng Ondiek, alisema ingawa waziri wa mipango maalumu Bi  Esther Murugi amewataka wahamie maeneo ya miinuko, maeneo hayo hayapo. Alisema wizara ilishirikiana na ile ya Japan kujenga  kituo cha kukimbilia lakini hakitoshi kwa sababu kina vyoo viwili na zahanati ya vyumba viwili ambayo haiwezi kuwatosha wakazi wa eneo hilo.

Mei

“Kuta zilizojengwa na serikali mto Nyando zimebomoka na kufanya mto kufurika wakati wa mvua,” alisema Bw Ondiek.

Na huku Pwani maafisa wa idara ya hewa walisema mvua kubwa iliponda kaunti za  Mombasa, Tana River na Kwale na itaendelea hadi Mei.

Mvua hiyo ilisababisha maji kukusanyika katika mitaa iliyo na watu wengi kama Kisauni na Likoni kutokana na ukosefu wa mitaro ya kutosha ya kupitisha maji.

Idara ya hali ya hewa ilisema kwenye tovuti yake kwamba maeneo ya pwani na magharibi yatapata mvua kubwa kati ya Machi na Mei.

Idara hiyo ilisema Kaunti ya Lamu, sehemu za Kilifi, Mombasa na Kwale ni baadhi ya yatakayopata mvua nyingi kuliko kiasi. Katika kaunti ya Elgeyo Marakwet watu wanaoishi maeneo yanayokubwa na maporomoko ya ardhi waliagizwa wahamie maeneo salama kuepuka mikasa.

Naibu kamishna wa eneo hilo Bw Moses Lilan alisema serikali ilitoa agizo hilo kabla ya msimu wa mvua kuanza.