Amrouche kutangaza kikosi cha Cecafa Jumapili

Na JOHN ASHIHUNDU

Imepakiwa - Wednesday, November 13  2013 at  17:22

Kwa Muhtasari

Kocha wa Harambee Stars, Adel Amrouche mnamo Jumapili atataja kikosi kitakachowakilisha Kenya kwenye mechi za Cecafa Senior Challenge Cup.

 

KOCHA wa Harambee Stars, Adel Amrouche mnamo Jumapili atataja kikosi kitakachowakilisha Kenya kwenye mechi za Cecafa Senior Challenge Cup.

Kocha huyo atataja kikosi hicho baada ya fainali ya GOtv baina ya mahasimu wa kandanda nchini Gor Mahia na AFC Leopards.

Baadhi ya wachezaji wa mataifa ya nje ambao huenda wakatajwa kujiunga na timu hiyo ni pamoja na Nahodha Victor Wanyama wa timu ya Southampton ya Uingereza, Arnold Origi, Brian Mandela na Patrick Osiako.

Katibu mkuu wa shirikisho la kandanda (FKF), Michael Esakwa ametangaza kwamba timu hiyo imepangiwa kuanza mazoezi Jumatatu kwa ajili ya mashindano hayo ambapo Uganda Cranes watetezi.

Wakati huo huo, Esakwa amedokeza kuwa timu hiyo imealikwa kwa mechi mmoja ya kirafiki dhidi ya Tanzania Taifa Stars mnamo Novemba 19 mjini Dar es salaam.

Mechi hiyo ni moja ya mechi za kimatifa zilizopangwa kuchezwa na shirikisho la kandanda duniani (FIFA). “Tumepata mwaliko huo kutoka kwa majirani zetu wa Tanzania.

Tumethibitisha tuko tayari na tungali tunangojea kupata majibu ili tujue wanataka wachezaji wangapi na mpangilio wao wa ziara hiyo,” Esakwa alieleza.

Uganda

Mashindano hayo ya Cecafa yatazinduliwa rasmi Ijumaa mjini Nairobi ambapo wafadhili kadha ambao wamekubali kushirikiana na FKF pamoja na CECAFA watatangazwa rasmi.

Wakati huo, mabingwa watetezi Uganda Cranes walitazamiwa kuanza mazoezi yake ya kutetejea taji hilo jana katika uwanja maarufu wa Nelson Mandela Namboole, mjini Kampala.

Cranes ambao juzi wakipata udhamini kutoka kwa kampuni ya mtandao wa simu ya Airtel, wanatazamiwa kuwakaribisha majirani zao wa Rwanda (Amavubi) kwenye mechi ya kirafiki. Kocha wa Uganda Micho Sredejovic amefichua kwamba atataja kikosi thabiti baada ya kutazamamechi hiyo ya kirafiki dhidi ya Rwanda itakayochezwa Jumamosi.