MCA ni mmoja wa wanaofanya KCPE

Na TOM MATOKE

Imepakiwa - Wednesday, November 5  2014 at  09:36

Kwa Muhtasari

Mwakilishi wa Wadi (MCA) katika kaunti ya Nandi ni mmoja wa watahiniwa wanaofanya mtihani wa kitaifa wa darasa la nane (KCPE) mjini Kapsabet.

 

MWAKILISHI wa Wadi (MCA) katika kaunti ya Nandi ni mmoja wa watahiniwa wanaofanya mtihani wa kitaifa wa darasa la nane (KCPE) mjini Kapsabet.

Fred Kipkemboi, 39, ambaye ni mwakilishi wa wadi ya Kapsabet na rafiki wa karibu wa Naibu Rais William Ruto, ni mtahiniwa wa kibinafsi.

Ni miongoni mwa watahiniwa 226 wa kibinafsi waliofanya mtihani huo katika shule ya msingi ya Nandi mjini Kapsabet hiyo Jumatatu.

Bw Kipkemboi, anayejulikana kwa utani na wakazi kama “Hussler” kutokana na uhusiano wake wa karibu na Bw Ruto, alisema aliamua kurudi shuleni ili kupata ufahamu wa kuelewa zaidi taratibu za Bunge.

“Niliamua kurudi shuleni kwa sababu ni vigumu kuelewa taratibu za Bunge la Kaunti na kwa sababu ya dhihaka nimekuwa nikipokea kutoka kwa umma na baadhi ya wawakilishi wenzangu,’’ alisema.

Aliambia Taifa Leo kuwa kila anapohudhuria mikutano, watu, wakiwemo baadhi ya viongozi wenzake, humtolea matamshi ya kumdhalilisha kama vile “Msiwe wajinga kama MCA Fred.”