Changamoto mbili zinazowaandama Wakenya 2017

Dkt Ouma Oluga

Katibu mkuu wa chama cha madaktari nchini (KMPDU) Dkt Ouma Oluga ahutubu kwenye kikao na wanahabari kaunti ya Mombasa Desemba 31, 2016. Alisema wako tayari kwa mazungumzo kusitisha mgomo wakitaka kikao maalumu na Rais Uhuru Kenyatta aliye Mombasa. Picha/WINNIE ATIENO 

Na OUMA WANZALA na WINNIE OTIENO

Imepakiwa - Sunday, January 1  2017 at  13:50

Kwa Mukhtasari

HUKU Wakenya wakiulaki Mwaka Mpya wa 2017, kuna changamoto mbili zinazowakodolea macho. Nazo ni mabadiliko katika sekta ya Elimu na mgomo wa madaktari unaoendelea.

 

Jumamosi, chama cha kitaifa cha madaktari (KMPDU) kilitangaza mgomo wao utaendelea hadi matakwa yao yatakapotekelezwa na Serikali ya kitaifa na kaunti.

Kwenye tukio jingine, katibu mkuu Wizara ya Elimu Dkt Belio Kipsang alitangaza kwamba shule ziko tayari kuanza muhula wake wa kwanza Januari 4, 2017 huku maelfu ya wanafunzi wakiwa hawajui la kufanya baada ya leseni za shule nyingi kufutiliwa mbali kwa kuendelea kutoa mafunzo wakati wa likizo ndefu ya miezi miwili kinyume cha agizo la Serikali.

Dkt Kipsang alisema shule ambazo vyeti vyao vilifutiliwa mbali zilipewa muda wa kuandikishwa upya.

“Shule za kibinafsi zilizopigwa kalamu zimeomba kuandikishwa upya ilhali walimu wa shule za kitaifa waliohusika na ukaidi wa agizo hilo watachukuliwa hatua za kinidhamu,” alisema katibu huyo.

Mnamo Novemba, Serikali ilifutilia mbali leseni ya shule ya kibinafsi ya Happyland Preparatory iliyoko katika mtaa wa Harambee, Nairobi kwa kuendelea kutoa mafunzo wakati wa likizo.

Na mjini Kisumu, walimu kadhaa walikamatwa katika shule za MA Junior na St Anne Ahero kwa kuendelea kutoa mafunzo wakati wa likizo.

Serikali imetisha kufutilia mbali kabisa leseni za shule hizi pamoja na nyingine zilizohusika.

Wakizugumza Mombasa, maafisa wa KMPDU wakiongozwa na katibu mkuu Dkt Ouma Oluga waliitaka Serikali itekeleze mkataba iliyotia sahihi na chama hiki kwa kuimarisha hali ya hospitali za umma, kutoa mafunzo kwa wataalam wa masuala mbalimbali ya afya na kufanikisha utafiti.

Maafisa hao walisema madaktari wanaoendelea kupokea mafundisho wanatakiwa kulindwa dhidi ya ukabila.

Walitoa wito kwa Rais Uhuru Kenyatta kuingilia kati na kutatua mzozo uliopo ndipo mgomo ambao umeingia siku ya 28 ufutiliwe mbali.

“Rais Kenyatta, sikiza kilio cha Madaktari. Tuko tayari kufanya mashauri,” alisema Dkt Oluga wakati wa mkutano na madaktari 100 kutoka kaunti sita waliokutana katika uwanja wa Mbaraki Sports Club.