Wito wa amani kwenye kampeni za 2017

Rais Uhuru Kenyatta

Rais Uhuru Kenyatta akihutubu katika Ikulu ya Nairobi.. Picha/MAKTABA 

Na LUCY KILALO, IRENE MUGO, JOEL REIYA, STANLEY KIMUGE,WYCLIFFE KIPSANG, BENSON AMADALA, TIMOTHY KEMEI, MAGATI OBEBO na ELGAR MACHUKA

Imepakiwa - Monday, January 2  2017 at  10:36

Kwa Mukhtasari

WAKENYA walikaribisha na kuadhimisha sherehe za Mwaka Mpya kwa mbwembwe na shamrashamra nyingi, huku viongozi wa kisiasa na kidini wakihimiza amani nchini hasa mwaka huu ambapo Uchaguzi Mkuu unatarajiwa kufanyika Agosti.

 

Kwenye hotuba yake kwa Wakenya, Rais Uhuru Kenyatta aliwataka Wakenya kudumisha amani na kuwakataa viongozi wanaozua ghasia.

“Tunapoingia kipindi cha uchaguzi, nawauliza Wakenya wote wawe wenye amani na viongozi wote kuhubiri amani wakati wa kampeni. Wacheni nirudie hili. Tutafanya uchaguzi Agosti 2017,” alisema Rais akiwa katika Ikulu ya Mombasa.

Aliongeza, “Uchaguzi utakuwa huru, wenye usawa na uwazi. Tunatarajia washindani wote kukubali matokeo na kutekeleza wajibu wao katika kujenga Kenya ya siku za usoni.”

Naibu Rais William Ruto aliyeungana na Magavana Salim Mvurya wa Kwale, Jackson Mandago wa Uasin Gishu na Cleophas Lagat  wa Nandi kukaribisha mwaka mjini Eldoret, aliwataka Wakenya kujiepusha na ghasia na chuki.

Kiongozi wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, pia alihimiza serikali ya Jubilee kuhakikisha uchaguzi mkuu ujao utakuwa huru, wa haki na amani.

Alisema bado kuna matumaini nchini hata ingawa Kenya ilishuhudia changamoto nyingi mwaka uliopita ikiwa ni pamoja na ufisadi.

“Kwa hivyo ninawahimiza Wakenya wote wanaothamini demokrasia na uongozi bora kujisajili kwa wingi na kuchagua serikali ya Wiper/Cord,” alisema.

Kiongozi wa ODM Raila Odinga kwenye makala yaliyochapishwa magazetini aliwataka Wakenya kuondoa Jubilee mamlakani kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Jijini Nairobi Askofu Mkuu wa Kanisa la Kianglikana nchini Jackson ole Sapit aliwataka wanasiasa kujadiliana kuzuia taharuki nchi inapojiandaa kwa uchaguzi mkuu wa Agosti 8 mwaka huu.

Katika Kaunti ya Kisii viongozi wa makanisa walitoa ujumbe wa amani nchi inapojiandaa kwa uchaguzi mkuu.

Kuepuka ghasia

Padre Jeremiah Nyakundi wa kanisa Katoliki mjini Kisii aliwataka wakazi kuishi kwa amani na kuombea nchi na viongozi ili maovu ya zamani yasitokee Mwaka Mpya. Aidha, aliwahimiza wanasiasa kuepuka matamshi yanayoweza kuzua taharuki kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Kiongozi wa kanisa la Seventh Day Adventist mjini Kisii, Zebedeo Mongare, pia aliwahimiza Wakristo kuomba uchaguzi uwe wa amani.

Gavana wa Kaunti hiyo, Bw James Ongwae aliwaongoza wakazi kukaribisha mwaka mpya katika uwanja wa Gusii alipowashambulia wanasiasa wa eneo hilo kwa kutotambua rekodi yake ya maendeleo.

Katika Kaunti ya Kericho Gavana Paul Chepkwony na Naibu wake Susan Kikwai waliwaongoza wakazi zaidi ya 3,000 kuahidi kudumisha amani.

Gavana Chepkwony alisema serikali yake itahakikisha kuna amani wakati wa kampeni za uchaguzi.

Kwenye ujumbe wake wa Mwaka Mpya Askofu Beneah Salala Okumu wa Kanisa Kiangilikana Kakamega aliwahimiza Wakenya kuhubiri amani nchi inapokaribia uchaguzi mkuu.

Imamu Hamza Ismail wa msikiti wa Jamia mjini Mumias pia aliwataka wanasiasa kujali maslahi ya Wakenya kwanza ili kuepuka ghasia.

Kwingineko, wakazi wa Kaunti ya Taita Taveta wakiongozwa na Gavana John Mruttu, waliadhimisha mwaka mpya kwa kutumbuziwa na waimbaji mbali mbali wa nyimbo za injili akiwemo Rose Muhando kutoka Tanzania.

Vile vile, ilikuwa furaha kwa wafugaji katika Kaunti ya Trans Mara mvua iliponyesha mkesha wa mwaka mpya.