http://www.swahilihub.com/image/view/-/3504318/medRes/1124708/-/l60ocaz/-/KAMWANA.jpg

 

Uhuru: Imeshindikana kumaliza mgomo wa madaktari

Uhuru Kenyatta

Rais Uhuru Kenyatta (kushoto) akihutubia taifa awali. Picha/PSCU 

Na LUCY KILALO

Imepakiwa - Monday, January 2  2017 at  11:16

Kwa Mukhtasari

RAIS Uhuru Kenyatta alikosa kutoa mwelekeo mwafaka kuhusiana na mgomo wa madaktari ambao umekuwa ukiendelea kwa zaidi ya mwezi moja sasa, huku akisema kuwa serikali imejaribu kila iwezalo, hali inayoibua shaka ikiwa suluhisho litapatikana.

 

“Wakenya wenzangu, ingawaje tumewekeza pakubwa katika afya na kupunguza vifo vya kina mama wajawazito na watoto, Wakenya wengi wangali wanakufa kutokana na maradhi yanayoweza kuzuiwa na kutibiwa. Nimeowaona wagonjwa wakiteseka madaktari wanapogoma,” alisema.

Aliendelea, “Tumejitahidi kupata suluhisho na madaktari, lakini kuna mipaka ya kile serikali inaweza kumudu,” alisema alipotoa hotuba yake ya kumaliza mwaka katika Ikulu ya Mombasa.

Madaktari wameendelea na mgomo wao wakisema kuwa lazima mkataba waliofanya 2013 utekelezwe. Hali hii imewaathiri Wakenya wengi ambao wamekuwa wakitafuta matibabu katika hospitali za umma.

Hata hivyo, rais aliwahimiza Wakenya wamchague tena ili aweze kukamilisha miradi iliyoanzishwa na serikali yake.

“Tuna uchaguzi katika muda wa miezi michache ijayo na itakuwa heshima kusalia rais wenu kwa kipindi kingine. Sababu yangu ya kuwania ni kukamilisha kazi tuliyoanza na kuhakikisha kuwa taifa linaendelea kuimarika ulimwenguni,” alisema katika hotuba yake.

Rais alijivunia rekodi yake akisema kuwa utawala wake umefanya mengi kushinda zilizotangulia.

Ninajivinia rekodi

“Wakenya wenzangu, ninajivunia rekodi ya utawala wangu, na Agosti, najua itakuwa wazi kwa Wakenya wengi kile tumefaulu kufanya kushinda serikali zilizotangulia, na zaidi kushinda nchi nyingine ambazo tuko katika kiwango kimoja,” alisema alipotoa hotuba yake akiwa Ikulu ya Mombasa.

Pia aliongeza kuhusu juhudi zinazofanywa kukabiliana na ufisadi huku akitaja kuwa tayari amepokea ripoti kuhusiana na kashfa ya michezo ya Olimpiki ya Rio.

“Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma anaangalia faili hiyo kuamua ikiwa kuna ushahidi wa kuchukua hatua zaidi kwa viongozi wa wizara ya michezo. Tuliahidi uwajibikaji na kuna mtu ambaye lazima atawajibika,” alisema.

Alisema kuwa hawataruhusu juhudi zao na za Wakenya ziharibiwe na wanasiasa ambao wanapenda malumbano.

“Walikataa kukubali matokeo ya uchaguzi uliopita na wameendelea na kudai udanganyifu hata ingawaje hakuna mchunguzi yeyote wa kuaminika alikubaliana na hilo,” alisema.