Jamii ya Wamaasai yaitaka serikali iirudishie ardhi yake

Wajumbe wa jamii ya Maasai wawasili katika jumba la Orange House

Wajumbe wa jamii ya Maasai wawasili katika jumba la Orange House kwa mkutano maalum na Kiongozi wa Chama cha ODM Bw Raila Odinga Novemba 29, 2016. Picha/VALENTINE OBARA 

Na GEORGE SAYAGIE

Imepakiwa - Monday, January 2  2017 at  17:39

Kwa Mukhtasari

VIONGOZI wa jamii ya Wamaasai katika Kaunti ya Narok, wameitaka serikali irudishe ardhi ya jamii hiyo iliyopata kutoka kwa mababu zao.

 

Viongozi hao walidai kuwa walipoteza ardhi hiyo kabla na baada ya uhuru.

Wakiongozwa na msemaji wa kundi la wawaniaji wa ubunge Narok, Bw Keri Olale, viongozi hao walidai kuwa jamii ilipoteza zaidi ya ekari 1.5 milioni za ardhi katika miaka hiyo, na wanastahili kurudishiwa ardhi ama kufidiwa.

Bw Olale alikuwa akihutubia wachimbaji mchanga katika kituo cha biashara cha Suswa, ambapo alisema kuwa Wamaasai wanataka kuombwa radhi na serikali ya Uingereza kwa makosa ya kihistoria wakati wa ukoloni, na kwamba ardhi yote iliyotwaliwa kimakosa irudishwe.

Alisema jamii hiyo itafikiria upya msimamo wake kuhusu yule itakayemuunga mkono katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Walitoa makataa kwa Rais Uhuru Kenyatta kuhakikisha kuwa ardhi kubwa Naivasha ambazo ni pamoja na renchi ya Kedong, Lord Dalamere na nyingine kaunti ya Laikipia chini ya Waingereza zinarudishwa.

Pia waliwataka viongozi waliochaguliwa katika kaunti wakiongozwa na Gavana Samuel ole Tunai waende kwa mahakama ya Kimataifa ya Haki na kudai fidia dhidi ya ukosefu wa haki kwa jamii ya Wamaasai.

Mwaka 2016, marehemu waziri wa zamani William ole Ntimama alianzisha mjadala huo akisema kuwa Maafikiano ya Ardhi ya Maasai ya 1904 na 1911 yanastahili kuangaliwa upya akisema muda wake wa kukodi wa miaka 100 ulimalizika 2004 na 2011.