http://www.swahilihub.com/image/view/-/3450846/medRes/338086/-/9ci9j1z/-/DNNakuruNurses0103j.jpg

 

Uwezekano wa kumalizika kwa mgomo wadidimia

Wauguzi wakiandamana

Wauguzi katika Hospitali ya Mkoa wa Bonde la Ufa ya Nakuru wakiandamana awali. Picha/SULEIMAN MBATIAH 

Na LEONARD ONYANGO

Imepakiwa - Wednesday, January 4  2017 at  12:52

Kwa Mukhtasari

MAZUNGUMZO baina ya madaktari na serikali yanatarajiwa kurejelewa Jumatano huku uwezekano wa kumalizika kwa mgomo huo unaoingia wiki ya tano sasa ukiwa mfinyu baada ya Rais Uhuru Kenyatta kushikilia kuwa hakuna fedha za kuwalipa wahudumu hao wa afya.

 

Madaktari watakutana na baraza la magavana pamoja maafisa wa wizara ya Afya alasiri.

Mkutano huo utakuwa wa kwanza tangu madaktari kuondoka kwenye mkutano na magavana baada ya kutofautiana vikali katikati mwa mwezi uliopita.

Mkurugenzi wa Baraza la Magavana Jacqueline Mogeni alithibitisha kuweko kwa kikao cha leo.

“Ni kweli magavana watakutana na madaktari pamoja na maafsia wa wizara ya Afya Jumatano (leo) saa tisa mchana,” akasema Bi Mogeni.

Mazungumzo hayo hata hivyo, huenda yasizae matunda baada ya pande zote kushikilia msimamo mkali.

Katika hotuba yake ya heri njema ya Mwaka Mpya kwa Wakenya, Rais Kenyatta alisema kuwa matakwa ya madaktari ya kutaka kupewa nyongeza ya asilimia 300 ya mishahara yao hayatatekelezwa kutokana na uhaba wa fedha.

“Tunafahamu kuwa mgomo wa madaktari umesababisha maumivu na mahangaiko miongoni mwa Wakenya lakini serikali imefikia mwisho haina fedha za kuwalipa,” akasema Rais Kenyatta.

Mazungumzo baina ya madaktari na wizara ya Afya yalisambaratika mwezi uliopita baada ya jaji wa mahakama ya kushughulikia mizozo ya wafanyakazi Hellen Wasilwa kutoa kibali cha kukamatwa kwa viongozi wa chama cha matabibu hao kwa kuendeleza mgomo haramu.

Sharti wizara ya Afya itii

Katibu mkuu wa Chama cha Madaktari (KMPDU) Ouma Oluga ameshikilia kuwa ni sharti wizara ya Afya itii Mkataba wa Makubaliano wa 2013.

Iwapo mkataba huo wa makubaliano hayo utatekelezwa, daktari wa daraja la chini zaidi atapokea mshahara wa Sh325,000 kutoka Sh127,000 kila mwezi.

Nao magavana wamepuuzilia mbali mkataba huo huku wakisema kuwa ulitiwa saini kabla ya huduma za afya kugatuliwa kwa serikali za kaunti.

Mvutano baina ya madaktari na serikali unaendelea kusababisha maumivu huku maelfu ya Wakenya wanaotegemea hospitali za umma wakiendelea kuhangaika.

Baadhi ya familia zimeamua kuondoa jamaa zao hospitali na kuwarudisha nyumbani kutokana na ukosefu wa madaktari.

Wakati huo huo, mbunge wa Seme James Nyikal ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Bunge kuhusu Afya ameshutumu serikali kwa kuwahadaa madaktari.

Dkt Nyikal ambaye amewahi kuhudumu kama mkurugenzi wa huduma za matibabu katika wizara ya Afya, alionya kuwa huenda madaktari wa Kenya wakahamia katika mataifa ya kigeni endapo serikali itafeli kutii mkataba wa 2013.