Uhuru njoo kabla nife - Joe Kadenge

 Joe Kadenge

Mwanasoka shupavu wa timu ya taifa ya Kenya katika miaka ya sitini na sabini Joe Kandege. PICHA/ MAKTABA 

Na BENSON MATHEKA na DAVID KWALIMWA

Imepakiwa - Wednesday, January 4  2017 at  13:03

Kwa Mukhtasari

ALIYEKUWA mwanasoka shupavu wa timu ya taifa ya Kenya miaka ya sitini na sabini Joe Kadenge anayeugua, amemwomba Rais Uhuru Kenyatta amtembelee kabla hajalemewa na ugonjwa.

 

Kwenye kanda ya video inayosambazwa katika mitandao ya kijamii, Bw Kadenge ambaye afya yake imedorora mno alimsihi Rais Kenyatta kumjulia hali kabla hajafa.

“Ningetaka kukutana naye kabla sijakufa,” alisema Bw Kadenge kwenye ujumbe ulionaswa katika kanda hiyo.Mwanasoka huyo mtajika alimtakia mema Rais Kenyatta na kumshauri kuongoza Kenya ili ipate ustawi mkubwa.

“Inaonekana mwili wangu haunitaki tena,” anasema Kadenge, anayesifika kama mmoja wa Wakenya waliokuwa na vipawa vya kipekee katika soka, kwenye video hiyo.

“Kuna watu katika serikali ambao ningetaka kukutana nao. Kwanza kabisa, ni Rais Uhuru Kenyatta. Ningetaka kukutana na marais wastaafu pia. Unawakumbuka wazee hao (Moi/Kibaki).”

Kisha Kadenge anaongeza matamshi yanayogusa moyo: “Ningetaka kukutana nao niwaambie kwaheri ili Mungu akiniita leo, nitakuwa nimepata fursa ya kuwaaga.”

Akiwa na umri wa miaka 80, jina la Kadenge limekuwa kwenye kumbukumbu za historia kutokana na weledi wake wa kusakata soka siku za ujana wake akiwa mchezaji wa timu ya taifa Harambee Stars na AFC Leopards.

Aliwahi kuchezea kilabu kilichojulikana kama Maragoli United.

Katika kitabu kuhusu maisha yake, “Joe Kadenge – the Life of a Football Legend,” mwanahabari wa BBC, John Nene anamtaja kama mchezaji mweledi na mtumbuizaji aliyewachenga walinzi kwa urahisi na kwa wepesi.

Bw Nene anaandika kwamba, ustadi wake ulitokana na uzoefu wake akiwa mwanariadha katika shule ya upili ya Musingu, Kakamega.

Kadenge na mpira

Weledi wake katika soka ulivumishwa na kibwagizo cha mtangazaji mashuhuri wa soka, Leonard Mambo Mbotela cha “Kadenge na mpira.”

Gwiji huyo wa mpira ambaye wanawe wawili Francis na Oscar pia walikuwa wanasoka mashuhuri amekuwa akilazwa hospitalini akiugua maradhi mbali mbali.

Juhudi za kumsaidia kupitia mitandao ya kijamii zinazoongozwa na watu kadhaa, akiwemo aliyekuwa mwanasoka wa kulipwa Sammy Shollei, aliyekuwa mwenyekiti wa Shirikisho la Soka nchini (FKF) Sam Nyamweya na wanahabari John Nene, Carol Radull, Elias Makori na Omulo Okoth zimefaulu kukusanya takriban Sh 500,000.

Pesa hizo zimetumiwa kulipa bili za hospitali na kumtunza Bw Kadenge ambaye amekuwa akiendesha teksi jijini Nairobi kwa miaka mingi baada ya kustaafu kucheza soka.

Marafiki na jamaa wamepanga harambee kubwa ya kumsaidia jijini Nairobi Ijumaa wiki hii. Japo anaonekana mgonjwa kwenye kanda hiyo, Bw Kadenge anaonyesha ujasiri wa kupambana na maradhi na hata kusema amepata nafuu.