http://www.swahilihub.com/image/view/-/3503772/medRes/1525159/-/tgn8loz/-/TOO.jpg

 

Mark Too alitiliwa sumu, wakili adai

Mark Too

Mbunge wa zamani Bw Mark Too. Picha/MAKTABA 

Na DENNIS LUBANGA

Imepakiwa - Wednesday, January 4  2017 at  13:22

Kwa Mukhtasari

KIINI cha kifo cha aliyekuwa mbunge Maalum wa chama cha Kanu, Bw Mark Too, kimechukua mkondo mpya huku wakili mmoja akidai kuwa aliuawa.

 

Aliyekuwa mwenyekiti wa Chama cha Mawakili Kenya (LSK) tawi la North Rift, Bw Simon Lilan ametaka uchunguzi huru wa maiti uendeshwe na mtaalam ili ukweli uweze kubainishwa.

Akihutubia wanahabari mjini Eldoret Jumanne, Bw Lilan alidai kuwa Bw Too alikuwa mjomba wake na kuhusisha kifo chake na siasa na mali nyingi aliyo nayo kote nchini.

“Marehemu Mark Too alikuwa ameanza kumtayarisha mwanawe Moses kuwania ubunge wa Kapseret. Tulipokutana mara ya mwisho alinieleza kuwa alikuwa anapanga kuuza kipande chake cha ardhi Nakuru ili asaidie kampeni ya mwanawe,” Bw Lilan alisema.

Alisema yuko tayari kuandikisha taarifa kwa polisi kuhusiana na madai yake.

Alieleza kuwa hatakaa kimya wakati wanaume kutoka jamii ya Nandi wanaendelea kuuawa, akitaja mauaji ya Isaac Kipsang Muge aliyekuwa kwa kanisa la Kianglikana.

Lakini mnamo Jumatatu, familia ya Bw Too ilitaka umma uwache kuzua uvumi kuhusu kifo chake na kupuuza madai kwenye mitandao ya kijamii kuwa alifariki kutokana na sumu.

Mkewe, Bi Sophie Too alihusisha kifo hicho na tatizo la moyo sababu ambayo ilielezwa na daktari wa marehemu, Prof Sylvester Kimaiyo.
Bw Too aliaga dunia katika hospitali ya St Lukes mjini Eldoret Jumapili akiwa anapokea matibabu.

Kuficha ukweli

Wakati huo huo, Bw Lilan alikosoa uamuzi wa kusafirisha mwili wa marehemu hadi kwa mochari ya Lee Funeral Home, Nairobi kabla ya mazishi yake, akidai kuwa hiyo ni njia moja wapo ya kuficha ukweli kuhusiana na kifo chake.

Alishangaa kwa nini mipango ya kusafirisha mwili Nairobi ilifanywa kwa haraka hata ingawaje hospitali ya Rufaa ya Moi Eldoret, ilikuwa imetengea mwili wake sehemu baada ya kufahamishwa kuhusu kifo chake.

Akithibitisha kuhusu kifo chake, daktari wake mwanasiasa huyo mkongwe Ahmed Faraj, alisema marehemu alitibiwa kipindi cha Krismasi baada ya kupata matatizo ya tumbo.

Mapema, siku aliyofariki, Dkt Faraj alisema marehemu alionekana kuwa na furaha na hata kuzungumza na wafanyakazi wake katika shamba lake la Kapseret karibu na Uwanja wa Kimataifa wa Eldoret.