http://www.swahilihub.com/image/view/-/3425694/medRes/940615/-/100tp1a/-/DNCOTU1910.jpg

 

Atwoli: Mimi ni KANU damu

Francis Atwoli

Francis Atwoli akihutubia wanahabari afisini mwake awali. Picha/MAKTABA 

Na BENSON MATHEKA

Imepakiwa - Wednesday, January 4  2017 at  13:28

Kwa Mukhtasari

KATIBU Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi nchini (Cotu) Bw Francis Atwoli, jana alifichua kuwa yenye ni mwanachama wa chama cha Kanu damu na hawezi kuingilia masuala ya chama kingine cha kisiasa.

 

Bw Atwoli alisema alijiunga na Kanu kabla ya kujiunga na Cotu na angali mwanachama wa maisha wa chama hicho kilichotawala Kenya tangu uhuru kwa miaka 40.

“Chama changu kimekuwa Kanu ambacho ningali mwanachama wa maisha na ambacho nilijiunga nacho kabla ya kuwa katibu mkuu wa Cotu,” alisema Bw Atwoli kwenye taarifa.

Alisema kila wakati akishirikiana na chama chochote cha kisiasa nchini na katika shughuli zozote za kisiasa, huwa anapata idhini kutoka kwa Bodi Simamizi ya Cotu.

Jumamosi, Bw Atwoli aliongoza mkutano mkubwa wa kisiasa katika uwanja wa Bukhungu mjini Kakamega ambapo alimtawaza kiongozi wa chama cha Amani National Congress Musalia Mudavadi kuwa msemaji wa jamii ya Waluhya.

“Huwa sishiriki shughuli za kisiasa bila ruhusa kutoka kwa Bodi Simamizi ya Cotu,” alisema Bw Atwoli.

“Ningetaka ieleweke kwamba mimi binafsi niliomba ruhusa kutoka kwa Bodi Simamizi ya Cotu na ikaniruhusu kushiriki siasa za kumtafuta msemaji wa eneo la Magharibi shughuli ambayo nilikamilisha kikamilifu Desemba 31, 2016 na sasa nimerejelea majukumu yangu kama Katibu Mkuu wa Cotu,” alisema.

Bw Atwoli alikanusha kwamba aliahidi kumpigia debe mgombeaji wa Muungano Mkuu wa Upinzani (Nasa) eneo bunge la Malava uchaguzi mdogo ukiitishwa baada ya mbunge Moses Malulu kufukuzwa katika chama cha Maendeleo Democratic Party of Kenya.

“Nimerejelea majukumu yangu katika Cotu kikamilifu na mtu yeyote hafai kunihusisha na chama chochote cha kisiasa kwa sasa. Ninasisitiza kuwa mimi sihusiki na siasa kwa wakati huu,” alisema Bw Atwoli.