http://www.swahilihub.com/image/view/-/2465982/medRes/838331/-/491gigz/-/SNKibwana0305d.jpg

 

Tunataka kura ya kielektroniki, magavana wasisitiza

Kivutha Kibwana

Gavana wa Makueni Prof Kivutha Kibwana ambaye pia ni mwenyekiti wa chama cha Wiper. Picha/JACOB OWITI 

Na BENSON MATHEKA Na DENNIS ODUNGA

Imepakiwa - Wednesday, January 4  2017 at  14:18

Kwa Mukhtasari

MAGAVANA Jumanne walikataa mfumo wa kupiga kura usiokuwa wa kielektroniki na kuunga mkono matumizi ya tekinolojia kwenye uchaguzi ujao.

 

Magavana watatu waliofika kutoa maoni yao mbele ya kamati ya sheria ya seneti walitofautiana na mwanasheria mkuu Profesa Githu Muigai aliyeunga matumizi ya sajili isiyokuwa ya kieletroniki.

Gavana wa Bomet Isaac Ruto, mwenzake wa Makueni Profesa Kivutha Kibwana na John Mruttu wa Taita Taveta walisema inawezekana kutumia tekinolojia kubuni sajili ya wapigakura.

Gavana Ruto alisema sheria iliyopitishwa na bunge kufanyia mabadiliko sheria ya uchaguzi inaweza kuzua mzozo nchini.

“Tunaunga mfumo wa kutumia tekinolojia kwa sababu hii sheria iliyopitishwa inaweza kusababisha utata nchini,” alisema.

Kamati hiyo inayosimamiwa na seneta wa Busia Amos Wako ilikamilisha kupokea maoni jana. Seneti inatarajiwa kujadili sheria hiyo kwenye kikao maalumu Jumatano.

Spika wa seneti Ekwee Ethuro wiki jana aliagiza kamati hiyo kukusanya maoni ya umma kabla ya kujadili sheria hiyo iliyopitishwa na bunge katika kikao kilichokumbwa na vurumai.

Upinzani umepinga sheria hiyo ukisema Jubilee inapanga kutumia sajili isiyotumia tekinolojia kuiba kura.

Jumanne, Gavana Kivutha alisema nchi haifai kurejelea mfumo wa kutambua wapiga kura wa zamani ilhali imepiga hatua katika maendeleo ya tekinolojia ya kisasa.

Kamati hiyo pia ilipokea maoni kutoka kwa wamiliki wa vyombo vya habari na mashirika ya kijamii.

Gavana Mruttu alisema uadilifu wa sajili ya wapigakura ni muhimu katika uchaguzi.
Profesa Muigai aliunga sajili mbadala isiyotumia tekinolojia kwenye uchaguzi mkuu ujao akisema ile ya kielektroniki inaweza kukwama.

Alisema kinyume na wanaokosoa sheria hiyo, Kenya haitumii mfumo wa kieletroniki katika uchaguzi.

Hata hivyo, alikosolewa na Seneta wa Mombasa Hassan Omar, aliyesema kwamba madai hayo yalikuwa ya uongo.

Wapiga kura hewa

“Hatutaki wapigakura waliokufa kupiga kura. Tunataka kumaliza ujanja kupitia mfumo wa kielektroniki,” alisema Seneta Omar.

Alisema kwamba sheria za uchaguzi ziliundwa kupitia majadiliano na mrengo mmoja wa kisiasa hauwezi kuzibadilisha bila kuhusisha mwingine.

Seneta Omar alisema hatua ya serikali ya kubadilisha sheria hiyo imezua shaka na taharuki.

Lakini Naibu Spika wa seneti Kembi Gitura na seneta wa Nandi Stephen Sang’ walimuunga Profesa Muigai wakisema sajili kutambua wapigakura isiyokuwa ya kielektroniki ni muhimu.

Muungano wa vyama vya wafanyakazi wa serikali TUC- Kenya kwenye taarifa uliunga sajili ya kielektroniki ya wapigakura ukisema Kenya imepiga hatua kubwa kitekinolojia.

Katibu mkuu wa Muungano huo Bw Wilson Sosion alisema matumizi ya tekinolojia yatahakikisha uchaguzi huru na wa haki na amani.