Wamiliki wa bunduki walilia Boinnet na Nkaissery

Ceska Zbrojovka.

Bastola aina ya Ceska Zbrojovka. Picha/ HISANI 

Na BENSON MATHEKA

Imepakiwa - Thursday, January 5   2017 at  14:32

Kwa Mukhtasari

CHAMA cha Wamiliki wa Bunduki nchini (NGAO Kenya), sasa kinawataka Waziri wa Usalama wa Ndani Joseph Nkaissery na Inspekta Jenerali wa Polisi Joseph Boinnet kuwachukulia hatua kali wote wanaotumia vibaya bunduki na kupokonywa leseni za kuzimiliki.

 

Katika taarifa kwa vyombo vya habari, chama hicho kinawataka wakuu wa usalama kuwakagua wanaomiliki bunduki mara kwa mara ili kuepuka visa vya matumizi mabaya ya silaha ambavyo vimekuwa vikishuhudiwa nchini.

Katibu Mkuu wa chama hicho, Kapteni Alex Migwi alisema kwenye taarifa kwamba, hatua hiyo ni muhimu ili kuhakikisha wanaopatiwa leseni za kumiliki bunduki wanazitumia kwa kuzingatia sheria.

“Tunaunga ukaguzi wa mara kwa mara wa wote wanaomiliki bunduki ili kuhakikisha yeyote anayepewa leseni ya kumiliki silaha anaitumia kwa vitendo vinavyofaa,” alisema.

Wito wa chama hicho unajiri siku chache baada ya mfanyabiashara wa Nairobi kudaiwa kumtisha dereva mmoja nje ya kilabu, eneo la Kilimani Nairobi. Ilisemekana haikuwa mara ya kwanza kwa mfanyabiashara huyo kutumia bastola yake kutisha raia bila kuchokozwa.

Jumatano, Kapteni Migwi alisema bunduki zinapasa kutumiwa iwapo anayeimiliki yuko katika hatari kuu. “Lengo la kumiliki bastola sio kusuluhisha mizozo ya nyumbani au ya barabarani,” alisema Kapteni Migwi.