http://www.swahilihub.com/image/view/-/1610654/medRes/345875/-/5ii55mz/-/Johoo.jpg

 

Kumbe Joho alipokonywa walinzi kwa kumsuta rais!

Ali Hassan Joho

Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho. Picha/MAKTABA 

Na CHARLES WASONGA na GALGALO BOCHA

Imepakiwa - Sunday, January 8  2017 at  13:49

Kwa Mukhtasari

SERIKALI Jumamosi iliwaondoa walinzi 20 wa magavana Hassan Joho (Mombasa) na mwenzake wa Kilifi Amason Kingi kwa njia isiyoeleweka.

 

Hatua hiyo inajiri chini ya saa 48 baada ya Gavana Joho kumtaka Rais Uhuru Kenyatta kuonyesha miradi iliyoanzishwa na serikali yake katika eneo la Pwani.

Mnamo Ijumaa, Bw Kingi vilevile alimuonya Rais Kenyatta dhidi ya kutembelea Kaunti ya Kilifi kuzindua 'miradi hewa’.
Kufuatia hatua hiyo, wabunge sita wa chama cha ODM katika eneo la Pwani wamempa Waziri wa Usalama Joseph Nkaissery makataa ya siku mbili kuwarejeshea viongozi hao walinzi wao.

Wakingozwa na mbunge wa Mvita Abdhulswamad Nasir, wabunge hao walisema Bw Nkaissery akikataa kuwarejeshea viongozi hao walinzi, 'demokrasia itachukua mkondo wake’

“Jambo lolote likiwakumba magavana hao au familia zao, wale waliotoa amri za kuondolewa kwa walinzi wao watawajibika,” alisema Bw Nasir.

Maafisa hao wanaotoka katika vitengo vya polisi vya General Service Unit (GSU) na Utawala, waliamrishwa kuondoka katika afisi za magavana hao na makazi yao Jumamosi asubuhi.

Wengine walioandamana na Bw Nasir ni pamoja na Rashid Betsimba (Kisauni), Badi Twalib (Jomvu), Suleiman Dor (Msambweni) na Mishi Mboko (Mombasa).

“Mwendo wa saa nane alasiri, kwa njia ya kiajabu, maafisa hao walipigiwa simu moja kwa moja warejee katika vituo vyao. Hapakuwa na njia rasmi ya kuwarejesha ila makamanda wao waliwapigia simu tu,” alisema Betsimba.
Hii ni mara ya pili kwa Gavana Joho kupokonywa walinzi.

Mwaka 2016, Gavana huyo alipokonywa walinzi kwa madai ya kuwatumia kusababisha utovu wa usalama wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa Malindi.

Baadaye mahakama ilibatilisha hatua hiyo na kisha Gavana Joho akarejeshewa walinzi na bunduki zao.

Dhuluma

ODM imeghabishwa na mtindo wa kumdhulumu Gavana Joho kwa kumpokonya walinzi kila mwaka huku ikitaka walinzi hao warejeshwe mara moja.

Chama hicho jana kilisema kuwa hatua hiyo “ambayo ni kinyume cha sheria” imekuwa ikichukuliwa dhidi ya Bw Joho kila mwaka Rais Uhuru Kenyatta anapozuru Pwani kwa likizo ya Krismasi na Mwaka Mpya kwa lengo la kumtisha ili ahamie Jubilee.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, Mkurugenzi wa Masuala ya Uchaguzi katika ODM Junet Mohammed alisema hatua ya Bw Joho aliye Naibu Kiongozi wa chama hicho kusimama kidete katika ODM ndiyo imekuwa ikimghadhabisha rais.

“Joho amekuwa akimwambia Rais ukweli anapojaribu kuhujumu viongozi wa ODM na miradi ya maendeleo iliyoanzisha na Joho ili kusaka uungwaji mkono kutoka kwa wakazi,” akasema.

Hasira

Rais hupandwa na hasira na baada hatua haramu ya kumpokonya Joho ulinzi hufuatia. Baadaye mahakama hubatilisha hatua hizo na kuamuru gavana huyo arejeshewe walinzi,” akasema Bw Mohammed ambaye ni Mbunge wa Suna Mashariki.

“Kama ODM tungependa kukariri kuwa hatua ya kumpokonya walinzi Gavana Joho ni kinyume cha mahitaji ya kipengee cha sita cha Katiba kinachosema kuwa viongozi wakuu wa hadhi ya Joho wanapasa kupewa ulinzi wa saa 24,” Mohammed akasema.

“Kwa hivyo, tunaitaka serikali kumrejeshea Gavana Joho walinzi wake mara moja. Na endapo hatari yoyote itampata kiongozi huyo serikali ndio itakuwa wa kulaumiwa,” akasema Bw Junet.

Awali akijibizana na Rais Kenyatta Joho alisema, “Lakini serikali kuu imekuwa na mtindo mbaya wa kujihusisha na miradi iliyotekelezwa na serikali za kaunti kusudi ijiimarishe kisiasa kwa wakazi,” akasema Bw Joho.

Lakini Rais alijibu kwa kukariri kuwa serikali yake imekuwa ikianzisha miradi kote nchini bila ubaguzi, kazi ambayo alisema itaendelea.

Amri ya kumpokonya Joho mwaka huu imetolewa chini ya saa 72 baada yake kujibizana hadharani na Rais Kenyatta.

Gavana Joho yuko nchini Ghana ambapo ameandamana kiongozi wa ODM Raila Odinga kuhudhuria sherehe ya kuapishwa kwa rais mteule wa nchi hiyo Bw Nana Akufo Addo.