http://www.swahilihub.com/image/view/-/3354792/medRes/345333/-/lca58uz/-/DNODM2503c.jpg

 

Raila sasa ataka matokeo ya #KCSE2016 yachunguzwe

Waziri Mkuu Raila Odinga

Mwaniaji urais wa NASA Raila Odinga. Picha/MAKTABA 

Na CHARLES WASONGA

Imepakiwa - Sunday, January 8  2017 at  14:06

Kwa Mukhtasari

KIONGOZI wa upinzani Raila Odinga, sasa anataka tume ibuniwe kuchunguza sababu zilizochangia matokeo mabaya katika Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE) ya mwaka 2016.

 

Kwenye taarifa aliyotuma kwa vyombo vya habari Jumamosi, Bw Odinga ambaye yuko nchini Ghana kuhusu hafla ya kuapishwa kwa Rais mteule Nana Akufo Addo, alisema idadi kubwa ya wanafunzi waliofeli mtihani huo ni kiashirio kwamba kasoro zilitokea katika usimamizi wa mtihano huo.

Kauli ya Bw Odinga anajiri siku moja baada ya Chama cha Kitaifa cha Walimu (Knut) kuhoji uhalali wa matokeo hayo na kupendekeza kuchunguzwa kwa usahihishaji wa mtihani huo ambayo matokeo yake yalitangazwa Desemba 29, 2017.

“Matokeo ya mtihani wa KCSE ya 2016 yanayoonyesha kuwa asilimia 85 (sawa na watahiniwa 489,000) hawakupata alama za kuwawezesha kujiunga na vyuo vikuu yanashtua. Isitoshe, inashangaza kuwa ni wanafunzi 141 pekee walipata alama ya “A” huku wenzao 33,399 wakipta alama ya “E”

Hata hivyo, Bw Odinga aliwapongeza Waziri wa Elimu Dkt Fred Matiang’i na Mwenyekiti wa Baraza la Mitihani Nchini (NEC) kwa kuanzisha sheria zilizozima wizi wa mitihani ambayo imekuwa kero katika sekta ya elimu kwa miaka mingi.

Mwanasiasa huyo alielezea hofu kuwa mtindo huo wa idadi kubwa ya wanafunzi kufeli ukiendelea, taifa hili litakosa wataalamu katika nyanja mbalimbali za uchumi.